Tuesday 19 November 2013

CUF YAKIRI DK SHEIN NDIYE MSEMAJI WA SMZ

Mwinyi Sadallah – Zanzibar
CHAMA cha Wananchi (CUF), kimesema kinaunga mkono kauli ya Rais wa Zanzibar Dk Ali Mohamed Shein kuwa yeye ndiye msemaji wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, na yaliyosemwa na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad ni mtazamo wake binafsi, kama kiongozi wa kisiasa. Msimamo huo umewekwa wazi na Naibu Katibu Mkuu wa CUF Zanzibar, Hamad Masoud Hamad katika mahojiano maalumu na Gazeti la Mwananchi, Mtendeni mjini Unguja jana. Hatua hiyo ya Hamad imekuja siku chache baada ya Rais wa Zanzibar, Dk Shein kuwaambia waandishi wa habari kuwa hakuna mwenye mamlaka ya kuizungumzia Zanzibar, isipokuwa yeye. Hamad alisema Makamu wa Kwanza wa Rais anapozungumza na kutoa msimamo wake juu ya mambo ya Muungano na siasa, hufanya hivyo kama kiongozi wa CUF ndiyo maana hutumia jukwaa la kisiasa kuzungumza na wafuasi pamoja na wanachama wa chama hicho:
“Rais wa Zanzibar ndiye msemaji wa Serikali na kiongozi mkuu, lakini Makamu wa Kwanza anapozungumza katika jukwaa na wafuasi wake, hutoa msimamo wa chama chake kama kiongozi wa juu,” alisema Hamad. Maelezo hayo ya Naibu Katibu Mkuu wa CUF Zanzibar, yamekuja kufuatia tofauti ya kimtazamo na kimsimamo iliyojitokeza kuhusu ni nani mwenye mamlaka ya kuizungumzia Zanzibar. Akizungumzia tathmini yake ya miaka mitatu ya Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar (SUK), Hamad alisema kimsingi imefanikiwa kudumisha amani na kuondoa mivutano ya kisiasa na malumbano yaliyochangia kurudisha nyuma maendeleo ya Zanzibar. Hata hivyo, alisema muundo wa SUK unahitaji kuangaliwa upya kwa ngazi ya watendaji na viongozi wa kisiasa ili kuleta taswira ya umoja wa kitaifa. Mawaziri na Naibu Mawaziri, wanafanya kazi kwa ushirikiano, lakini watendaji wakuu wa SUK bado wameshindwa kutekeleza majukumu yao na kuendeleza baadhi ya vitendo vinavyowanyima haki wananchi. Alisema haikuwa mwafaka muundo wa SUK kuhusisha mawaziri na naibu wao, bila ya kuangalia nafasi nyingine za watendaji wakuu wa Serikali wakati wa marekebisho ya 10 ya Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984. 
Alisema pamoja na rais kuzungumzia mwelekeo wa kuimarika na kukua kwa uchumi wa Zanzibar, bado hali ya vipato kwa wananchi wa kawaida ni duni kutokana na kuanguka kwa sekta ya viwanda na kuzorota kwa uzalishaji wa ndani.Hamad alisema sekta za uwekezaji, viwanda, mifugo na uvuvi lazima zipewe kipaumbele ili lengo la kuwapatia maisha bora wananchi, liweze kufikiwa.
Chanzo: Mwananchi

Saturday 17 August 2013

MWANASHERIA MKUU SMZ ” SERIKALI 2 NI KUVUNJA MUUNGANO

Na Salim Salim
Mwanaseria Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi wa Zanzibar leo amesema lengo la kuandikwa kwa Katiba Mpya si kuyafanyia Marekebisho katiba iliyokuwepo sasa bali ni kandika Katiba Mpya katiba ambayo itakuwa Muarubaini kwa kero za Muungano na Muungano wenyewe. Mwanaseheria Mkuu liyasema hayo leo asubuhi alipokwa akifunguwa Baraza la Katiba la Vyuo Vikuu liliondaliwa na ZAHILFE Shirikisho la Wanafunzi wa Vyuo Vikuu Zanzibar liliofanyika katika Ukumbi wa Salama Hal Bwawani.
Alilisifu Baraza hilo na kusema kuwa ni Baraza la Vijana wasome na kuwasifu Vijana kwa ile sifa yao kubwa ya kuleta mapinduzi katika jamii yeyote.Alimtaja kijana Sir King ndie waliosababisha Zanzibar iiteme Tanganyika mwaka 1895 Ogast na Tanganyika kuangukia katika mikono wa Wajerumani. Na kumtaja Gerald Pota alietumwa na Waingereza kuja kuunda Serikali na kumpangia Mfalme mshahara ambako alikuwa akilipwa paund 250 kwa mwaka. Msingi wa Muungano wa Tanzania ni kuungana kwa Nchi mbili huru Tanganyika na Zanzibar lengo la kuungana kwa nchi mbili hizi ni kufanya mambo yao pamoja na kupata faida zaidi na sio Nchi moja kuitawala Nchi nyengine alisema, hukua akiendela kusema:
Zanzibar si mkowa wala wilaya, Zanzibar ni Nchi, katika Muungano tulikubaliana baadhi ya mambo kufanya pamoja na sio Zanzibar kuwa Jimbo la Tnganyika. Alisema duniani kuna miungano mingi mizuri akiutolea mfano Muungano wa Uswis ambao una Serikali 24 na ule wa Muungano wa Maerkali wenye Serikali 52 na kusema kuwa ni uongo kuwa Serikali Tatu zitavunja Muungano na kusema Serikali Mbili ndizo zitakazovunja Muungano, na hata Muungano wa Serikali Tatu ukivunjika si kioja. Serikali Tatu hazitovunja Muungano Serikali Mbili ndizo zitakazo vunja Muungano. Alisema Uruhani wa Serikali ya Tanganyika ndio kero kubwa ya Muungano na Serikali tatu itairudisha Serikali ya Tanganyika ambako kero kubwa itakuwa ishatatuliwa.
Aliitaja Sheria ya Kuanzishwa na Bank Kuu ya Tanzania kuwa aliisaini Karume mwenyewe lakini Karume alipoona mapungufu ya Seria hiyo ndio maana akaanzisha PBZ. Aidha alisema kama Zanzibar inataka kuishtaki TFF itashinda na TFF haitokuwemo FIFA kwani TFF haiwakilishi Tanzania kama ilivyokuwa ZFA ilivyokuwa haiwakilishi Tanzania. Hivi hatuoni haya kubakia hivi hivi kuwa Manispaa wakati Zanzibar ilikuwa Empire alihoji Mwanasheria Mkuu na kuendelea kusema hivi tutamuamini vipi mtu ambae leo anasema Zanzibar si Nchi atakapokuwa Rais wa Tanzania ambao Zanzibar haitokuwa na Mamlaka atasema Zanzibar ni jimbo la Tanganyika na kumalizia kusema wengi wa Watanganyika wanachuki na Zanzibar. Aliwataka wanafunzi hao kuzungumzia mambo ya Muungano na kutaka kuwe na usawa “Bila ya kuwa na usawa katika Mungano huu huo si Muungano bali ni ukoloni” alisema, na kutaka kuwe na mfumo wa usawa katika Baraza la Mawaziri na Bunge na kuwe na makubaliano ya thuluthi mbili kila upande katika kupitisha sheria na kuengezwa au kupunguzwa mambo ya Muungano.
Alisema katika Muungano wa Serikali Tatu ni lazima Rasilimali zitumike kwa Usawa na sio kama hivi sasa Tanganyika inavyotumia Rasilimali za Muungano wao peke yao katika kusoma na kuinyima Zanzibar. Tume ya Pamoja ya Fedha haijaanza kazi mpaka leo, na katika Muungano kuna mapato ya Muungano na Matumizi ya Muungano na Mapato ya Muungano siku zote huwa mengi ambako Tnganyika hawataki tugawane. Alisema si kweli kama Muungano wa Serikali tatu una harama bali Muungano wa Serikali Mbili ndio wenye gharama na Zanzibar ndio inaharamika zaidi, aliwataka viongozi wawe wakweli na waache kuwapotosha wananchi. Aliwaonya Wazanzibar kuwacha kulumbana na badala yake kukaa pamoja kuidai nchi yao. Alisema Serikali ya Umoja wa Kitaifa iliundwa ili kuondowa tofauti kwa Wazanibar na kusema kuwa kuundwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa ni kuala gumu kuliko mabadiliko ya Muungano. Alisema Wanaotaka Seriakali Mbili hoja zao hazina msingi na hakuna haja ya kubakia kwenye Serikali mbili na wengi wanaotaka Serikali Mbili wanalinda maslahi yao ya kidunia.
Hoja yangu nawataka wanaotaka Serikali Mbili na Wanaotaka Mkataba wakae pamoja wajadiliano Mfumo wa Muungano wa Serikali Tatu mfumo ambao utakuwa na Mslahi na Zanzibar. Awali Mwenyekiti wa ZAHILFE alikanusha taasisi yake kuandaa kungamano la tarehe 6 mwezi wa 7 lililofanyika Taasisi ya Kiswahili na Lugha za Kingeni na badala yake kongamano hilo liliandaliwa na Mkowa wa Wanafunzi wa Vyuo Vikuu vywa CCM na kusema Taasisi yake haina mafungamano na chama chochote cha siasa. Kongamano hilo lilianza na Wimbo wa Taifa wa Zanzibar na lilihudhuriwa na baadhi ya Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi. Marais 10 wa Serikali za Wanafunzi waliochangia katika Kongamano hilo walitaka Zanzibar yenye Mamlaka Kamili na Usawa Katika Muungano.
Chanzo: habari leo

Friday 26 July 2013

Muungano wa Tanzania au Tanganyika na Zanzibar?

KWA mujibu wa Mkataba wa Muungano, uliotiwa sahihi Aprili 22, 1964, kati ya Mwalimu Julius Nyerere na Sheikh Abeid Amani Karume, na kwa mujibu pia wa Sheria ya Muungano, Namba 22 ya 1964, iliiyoridhia Mkataba huo na kuupa nguvu ya Kisheria na kutumika nchini, jina sahihi la Muungano limetajwa kama:
Jamhuri ya Tanganyika na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar, kuanzia siku ya Muungano na baada ya hapo, zitaungana kuwa Jamhuri moja kwa jina la Jamhuri ya Tanganyika na Zanzibar.
Kufikia hapo, wengi wanaweza kujiuliza; kama hapajawa na Muungano mwingine, jina hili la ‘Muungano wa Tanzania’ linatoka wapi? Na kama jina Tanzania limebuniwa baada ya Muungano, ina maana kwamba katika kipindi cha Muungano tangu ulipotiwa sahihi hadi kubuniwa kwa ‘Tanzania,’ hapakuwa na Muungano? Marekebisho yapi yalifanyika kufikia ‘Tanzania’ badala ya ‘Tanganyika na Zanzibar’? Na kwa nini?
Haya ni maswali mepesi, lakini yenye utata kwa Mtanzania yeyote yule. Yana utata kwa sababu historia ya Muungano, haijaandikwa itakiwavyo na kuwekwa wazi. 
Watanzania wamekuwa wakipewa tafsiri za kisiasa, nyepesi na za majukwaani. Na kwa kuwa ilikuwa ni dhambi kuu kuhoji juu ya Muungano wala kutoa maoni juu ya muundo na aina gani ya Muungano uliokusudiwa, Watanzania wameishi kwa kuuchukulia Muungano huo kama ‘fumbo la imani’ tu, huku kero za Muungano zikichipuka kama uyoga kwenye shamba lenye rutuba lililotelekezwa.
Jina la Muungano huu limetajwa kwenye Sheria ya Muungano Namba 22 ya mwaka 1964, kifungu cha 4, kuwa ni “Jamhuri ya Tanganyika na Zanzibar” (URTZ), kuanzia siku ya Muungano na baada ya hapo.
Wakati nchi mbili hizi zikiungana hapakuwa na Katiba iliyoandaliwa kusimamia Muungano. Kwa hiyo, ilikubaliwa kwamba katika kipindi cha mpito (wakati Muungano huo ukiandaliwa Katiba yake), Katiba ya Jamhuri ya Tanganyika itumike (na ilitumika) pia kama Katiba ya Muungano kwa kufanyiwa marekebisho kuingiza yale mambo 11 yaliyopitishwa kushughulikiwa na Serikali ya Muungano na kuwapo kwa Serikali ya Zanzibar (Sheria ya Muungano-Kifungu cha 5).
Mambo hayo ni Katiba na Serikali ya Jamhuri ya Muungano, Mambo ya Nje, Ulinzi, Polisi, Mamlaka juu ya hali ya hatari na Uraia. Mengine ni Uhamiaji, Biashara ya Nje na Mikopo, Utumishi wa Jamhuri ya Muungano, Kodi na Ushuru wa Forodha, na mwisho, Bandari, ndege za kiraia, Posta na simu za maandishi (telegraph).
Itakumbukwa kwamba Zanzibar haikuwa na Katiba yake wakati Muungano unafanyika, hadi mwaka 1984. Lakini Zanzibar ilikuwa na Sheria zake zitokanazo na maagizo ya Rais (Decrees).
Kwa hiyo, kwa kutambua kwamba Serikali za Tanganyika na Zanzibar hazikufa baada ya Muungano, iliwekwa bayana kuwa Sheria za Tanganyika na zile za Zanzibar, zitaendelea kutumika katika nchi hizo (Kifungu 8 cha Sheria ya Muungano na Ibara ya 5 ya Mkataba wa Muungano), bila kuingilia au kuingiliwa na shughuli za Serikali ya Muungano.
Ndiyo kusema kwamba Muungano wa Tanganyika na Zanzibar (URTZ), uliundwa kwa ajili ya, na ili kushughulikia mambo 11 tu ya kila nchi, wakati ule, ambapo Serikali za Tanganyika na Zanzibar zilibakia hai kuendelea kushughulikia mambo mengine yote yasiyo ya Muungano katika maeneo yake, huku Katiba ya Tanganyika ikiendelea kutumika kama Katiba ya Muungano pia.
Jamhuri ya Muungano ilitakiwa kuwa na Katiba yake katika muda wa miezi 12 iliyofuata kuanzia Aprili 26, 1964, yaani kufikia Machi 26, 1965, kwa mujibu wa Mkataba wa Muungano na Sheria ya Muungano; lakini haikuwa hivyo.
Ilipofika Machi 24, 1965, Bunge lilipitisha Sheria Namba 18 ya mwaka 1965 kuongeza muda wa kuitisha Bunge la Katiba “hadi hapo itakapoonekana vyema kufanya hivyo.”
Kuongezwa kwa muda wa kuitisha Bunge la Katiba, kulimaanisha kuchelewa kupatikana kwa Katiba halali ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar kama ilivyotakiwa chini ya Mkataba na Sheria ya Muungano ya 1964.
Ili kuokoa Muungano huo usiendelee kuchangia Katiba na Serikali ya Tanganyika, Julai 10, 1965, Bunge lilipitisha Katiba ya Muda (Sheria No. 43 ya 1965) ya Tanzania, iliyotambua kuwa “Tanzania ni Jamhuri ya Muungano” (Ibara ya 1) inayoundwa na Tanganyika na Zanzibar (Ibara ya 2), na kwamba kutakuwa na Chama kimoja cha siasa Tanzania (Ibara ya 3); lakini hadi hapo TANU na ASP vitakapoungana, Chama cha siasa kwa Tanganyika kitakuwa “The Tanganyika African National Union (TANU), na kwa Zanzibar, kitakuwa “Afro-Shirazi Party” (ASP).
Hapa, Katiba ilijikanganya. Kulikuwa na Chama kimoja vipi Tanzania wakati kulikuwa na TANU na ASP?
Hapo ndipo jina la “Tanzania” lilipoanza kuonekana katika ‘Katiba ya Muungano’ na kuleta mgongano kati yake na jina asilia la Muungano huo linalotambulika katika Mkataba wa Muungano, na katika Sheria ya Muungano ya 1964.
Ifahamike kwamba vyama vya siasa havikuwa na havijawa jambo la Muungano. Kwa hiyo, kwa kuingiza vyama vya siasa katika suala la Muungano, Katiba ya Muda ya 1965, ilikuwa imekiuka Mkataba/Sheria ya Muungano.
Utata huu unazua maswali pia juu ya uhalali wa Tume ya Vyama vya TANU na ASP, iliyoteuliwa kuandaa mapendekezo ya Katiba ya kudumu ya mwaka 1977. Ni kuingizwa kwa vyama vya siasa katika muundo wa Muungano kulikozua, na kunaendelea kuzua, mitafaruku na kero ndani ya Muungano hadi sasa.
Lakini kwanini haya yaliruhusiwa kuingia katika Katiba wakati kulikuwa na Wanasheria wenye elimu nzuri na uelewa wa juu katika kuutahadharisha Uongozi? Au ni kwa sababu ya wanasiasa wasioambilika?
Ni vyema nikumbushe pia kwamba Mkataba wa Muungano na Sheria ya Muungano, ndivyo msingi mkuu wa Katiba ya Muungano, vinginevyo hakuna Katiba ya Muungano wala ya Zanzibar, na hivyo, hakuna Muungano.
Wala Bunge la kawaida la Muungano halina mamlaka ya kurekebisha Mkataba/Sheria ya Muungano, au kuongeza ambacho hakikukusudiwa au kutajwa katika Mkataba wa Muungano. Hadi sasa, Mkataba wa Muungano na Sheria ya Muungano vinasomeka kama vilivyopitishwa mwaka 1964, lakini Katiba imeendelea kugeuzwa na kurekebishwa kwa matashi ya wanasiasa.
Hapa maswali yafuatayo yanajitokeza. Jina ‘Tanzania’ lilitoka wapi, na liliingiaje katika msamiati wa Katiba ya Muungano? Je; kutumika kwa jina hilo kunabatilisha jina asilia la ‘Jamhuri ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar?’ Kama halibatilishi, nini suluhisho la mgongano huu?
Ilikuwa hivi: Miezi mitatu baada ya Tanganyika na Zanzibar kuungana, lilitangazwa shindano la kubuni jina litakalowakilisha hadhi na kuwapo kwa Muungano wa nchi hizi mbili. Mshindi aliahidiwa zawadi ya pauni 10 za Uingereza, sawa na Shilingi 20/= za wakati ule za Tanzania.
Kamati ndogo ya Baraza la Mawaziri iliteuliwa kupokea na kuchambua maoni ya washindani 1,534 yaliyopokelewa na kuwasilisha machache (idadi haifahamiki) kwenye Baraza la Mawaziri kwa uamuzi wa mwisho. Maoni yalipokelewa kutoka ndani na nje ya nchi, zikiwamo Urusi, Uingereza, Sweden, Uchina, Ufaransa, Poland, Italia na Australia.
Katika mkutano na Waandishi wa Habari, Ikulu, Oktoba 29, mwaka 1964, Rais Julius Nyerere alitangaza kwamba Baraza la Mawaziri limechagua jina ‘Tanzania’ kuwakilisha Jamhuri ya Muungano, lakini hakutaja jina la mshindi ambaye hajajulikana hadi leo. 
Aliwafundisha pia namna ya kulitamka jina jipya, kwamba ni ‘Tan-Zan-ia,’ na si ‘Tanzania’ kama inavyotamkwa sasa. Tan-zan-ia ni kifupisho chenye kumaanisha Tan – Tanganyika na Zan – Zanzibar, ambapo herufi– ‘ia’ kukamilisha Tan-zan-ia, zimetoka Zanzibar (i) na Tanganyika (a). Kati ya majina manne yaliyochuana hadi mwisho na ‘Tan-Zan-ia,’ ni pamoja na ‘Tanzan,’  ‘Tangibar’ na ‘Zantan.’
Hapa ifahamike kwamba, jina hili ‘Tan-Zan-ia,’  mbali na kuzua mgongano na jina la Muungano (URTZ) kwa mujibu wa Mkataba na Sheria ya Muungano, lilikusudia kuwakilisha jina la ‘Muungano’ na mambo ya Muungano tu, lakini halikufuta, na hatudhani kwamba lilikusudia kufanya hivyo, muundo wa Muungano uliokusudiwa, wala kufuta Serikali ya Tanganyika na Zanzibar na mamlaka zake, kama tulivyoelezea hapo mwanzo.
Kuonyesha kwamba Tanganyika ilikuwa na hadi sasa ni hai, Katiba ya mwaka 1965 kwa mfano, Ibara ya 12, ilitambua Rais wa Jamhuri ya Muungano kuwa pia ndiye Rais wa Tanganyika, chini ya Katiba ya Muda.
Nayo Ibara ya 13 (1) ilitambua kuwa na Makamu wawili wa Rais, mmoja (wa pili) akiwa Msaidizi wa Rais kwa mambo ya Muungano nchini Tanganyika.
Ibara ya 20 ilimpa Rais mamlaka ya kuteua Mkuu wa Mkoa kwa kila Mkoa nchini Tanganyika, ambapo Ibara ya 25 ilizungumzia kuhusu Tanganyika kuwa na majimbo ya uchaguzi; na mifano mingine mingi.
Wataalamu wa mambo ya Sheria na Katiba bado wanahoji, kama Bunge la kawaida lililobadili jina la Muungano lilikuwa na mamlaka au uwezo wa kufanya hivyo kisheria.
Katiba ya Muda ya 1965 ilibainisha wazi kuwa Muungano wa ‘Tanzania’ unaundwa na Tanganyika na Zanzibar kwa maana ya kutambua kuwako kwa nchi hizi mbili.
Lakini Katiba ya 1977 inataja kuwa Muungano huo unaundwa na ‘Tanzania Bara’ na ‘Tanzania Zanzibar,’ kwa maana ya majina hayo kuchukua nafasi ya majina ya Tanganyika na Zanzibar.”
Kama lilivyo jina la ‘Tanzania,’ majina ya ‘Tanzania Bara’ na ‘Tanzania Zanzibar’ hayajulikani katika Mkataba wa Muungano na Sheria ya Muungano ambayo haijabadilika hadi leo.
Nini athari ya mgongano huu na uhalali wa mabadiliko haya kwa Mkataba/Sheria ya Muungano? Je; Bunge la Katiba lililopitisha Katiba hiyo, ndilo lile la aina ya lililotakiwa chini ya Mkataba na Sheria ya Muungano? Je; Serikali ya Muungano ina mamlaka na uwezo wa kubadili (majina) yaliyomo katika Mkataba uliyoiunda? Je; yai laweza kumbadili kuku?
Kupata majibu ya maswali haya, hatuna budi kufanya rejea kwa ufupi tu, mchakato mzima wa Katiba tatu za Muungano zilizopita ili kuona utata ulipo.
Hakuna ubishi kwamba Mkataba wa Muungano (Articles of Union) wa 1964, na Katiba ya muda (Interim Constitution) ya 1964 na ile ya 1965, zilitambua kuwapo kwa Serikali ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, Serikali ya Tanganyika na Serikali ya Zanzibar zikiwa na mamlaka kamili kuhusu mambo ya nchi yasiyo ya Muungano.
Ilikubaliwa pia kwamba iandaliwe Katiba ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar kwa utaratibu uliowekwa, na ipatikane ndani ya mwaka mmoja tangu siku ya Muungano; na kwamba wakati hilo likifanyika, Katiba ya Tanganyika itumike pia kama Katiba ya Tanganyika, na hapo hapo kama Katiba ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar kwa kufanyiwa marekebisho kutambua kuwapo kwa Serikali ya Zanzibar, kama ilivyokuwa kwa Serikali ya Tanganyika.
Tatizo lilianza na Katiba ya Muda ya mwaka 1965, ambayo, chini ya Ibara ya 12 (1), ilibainisha kwamba “Mamlaka ya Utendaji (the Executive) kuhusu mambo yote ya Muungano, katika, na kwa ajili ya Jamhuri ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, na (pia) kwa (Serikali ya) Tanganyika, yatakuwa kwa Rais wa Serikali ya Muungano.”
Kwa maana hii, Rais wa Kwanza wa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, Mwalimu Julius Nyerere alikuwa wakati huo huo Rais wa Tanganyika pia.  Ingekuwa vivyo hivyo, kama Rais Abeid Karume wa Zanzibar angeteuliwa kuwa Rais wa Kwanza wa Muungano, kwamba angesimamia Serikali ya Muungano na Serikali ya Tanganyika, kwanza kama Rais wa Muungano, na pia angesimamia Serikali ya Zanzibar kama Rais wa Zanzibar. 
Huu ulikuwa ni mpangilio wa muda kusubiri kuandikwa kwa Katiba ya Muungano ambapo madaraka na mamlaka hayo yangetenganishwa kwa kuzingatia Mkataba wa Muungano.
Utata huu ulizidishwa na Ibara ya 49 ya Katiba hiyo iliyoweka wazi kwamba mamlaka ya kutunga Sheria kuhusu mambo yote ya Muungano katika na kwa ajili ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, na kwa mambo yote katika na kwa ajili ya Serikali ya Tanganyika, ni ya Bunge la Muungano.
Hii ilimaanisha sasa kwamba Rais wa Muungano ndiye aliyekuwa Rais wa Tanganyika, na Bunge la Muungano ndilo lililokuwa Bunge la Tanganyika pia.
Kama tunaweza kuufananisha Muungano huu na taasisi mbili zilizokubaliana kuunda ubia (Jamhuri) kwa njia ya hisa zilizo sawa (tuseme hisa 11 kila moja, kama yalivyokuwa mambo ya Muungano), basi Tanganyika imetoa kila ilicho nacho juu na zaidi ya hisa ilizopaswa kuchangia katika Muungano, tofauti na matakwa ya Mkataba.
Na kwa kuwa mchango huo wa ziada hautambuliki katika hati zote za kuanzisha Ubia huo, basi, inakuwa imetoa kwa hiari na haiwezi kuongezewa gawio wala kuwa na sauti na kauli katika Ubia huo kwa hicho cha ziada.  Kufanya hivyo ni kuhodhi mamlaka ya Muungano ambako Wazanzibari wanaita ‘kumezwa kwa Zanzibar.’
Lakini kwa upande wa Zanzibar, mamlaka ya utendaji kwa Serikali ya Zanzibar, kwa mambo yasiyo ya Muungano, yalibakia kwa Rais wa Zanzibar.  Vivyo hivyo, mamlaka ya kutunga Sheria kwa mambo yasiyo ya Muungano, yalibaki kwa Baraza la Wawakilishi la Zanzibar.
Hapo ndipo Bunge na jina la Tanganyika lilianza kupotea kimiujiza, wakati jina la mdau wa pili, Zanzibar, likaendelea kudumu, na wakati huo huo Mkataba wa Muungano na Sheria ya Muungano, ziliendelea, na zinaendelea kuutambua Muungano kwa jina la Tanganyika na Zanzibar.
Nyundo ya chuma ilipigiliwa kichwani mwa Tanganyika, pale Sheria Na. 24 ya mwaka 1967 ilipotungwa kumpa Rais uwezo wa kuweka neno ‘Tanzania’ badala ya neno ‘Tanganyika’ katika maandishi na nyaraka zote za kisheria, lakini haikubadili majina hayo katika Hati ya Mkataba wa Muungano na Sheria ya Muungano.
Mabadiliko yote haya, kwa kuanzia na Katiba ya Muda ya mwaka 1965, ndiyo yaliyorithiwa bila utafiti makini na kuingizwa katika Katiba ya Kudumu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya 1977.
Ni kutokana na mabadiliko hayo, yanayofanya watu wafikirie na kuamini kwamba Tanzania ndiyo Tanganyika, na Tanganyika ndiyo Tanzania; wakati si kweli.   Na hii ndiyo dhana potofu ya Serikali mbili – Serikali ya Muungano na Serikali ya Zanzibar.
Chanzo: Raia Mwema

Thursday 25 July 2013

Wanasiasa Z’bar na propaganda dhaifu

Leo nalazimika kuandika makala haya kwa mshangao mkubwa wa baadhi ya wanasiasa hapa Zanzibar kutengeneza taswira ambayo haikubaliki wala kuendana na wakati tulionao.
Kuna baadhi ya wanasiasa wanatumia propaganda dhaifu kwamba wanaodai mabadiliko katika muundo wa Muungano wanataka kumrejesha Sultan!
Hii ni ajabu ya mwisho, pia ni aibu kusikia kauli kama hizo baada ya takriban miaka hamsini ya kujitawala.
Inafahamika vizuri kwamba Zanzibar ni nchi kamili na watu wake waliamua kujitawala wenyewe kupitia mapinduzi yaliyoung’oa utawala kisultan Januari 1964 na Aprili mwaka huu Jamhuri ya watu wa Zanzibar ikaungana  na Jamhuri ya Tanganyika kuunda Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
 Sultan wa mwisho kutawala Zanzibar ni Jamshid bin Abdullah Al Said ambaye kwa sasa anaishi Portsmouth, Uingereza akiwa na umri wa miaka 83.
Hakuna anayemtambua katika medani za kisiasa kwa Zanzibar ya leo zaidi ya kubaki katika vitabu vya kihistoria tu, lakini kizazi hiki kinachojali ni nchi yao iliyo huru ambayo ilikombolewa kutoka kwa wakoloni.
Umezuka mtindo kwa wasiokuwa na nguvu ya hoja kudai eti kuna watu vibaraka wa Sultan, ndiyo maana wanadai mabadiliko katika Muungano!
Huu ni uzushi na uongo usiokuwa na hata chembe ya ukweli, wananchi wa Zanzibari chini ya Afro Shiraz Party ndio waliompindua Sultan na kuirejesha nchi yao mikononi mwa wazalendo ambao ni wakwezi na wakulima; iweje leo miaka 49 tukijiandaa kuadhimisha jubilee ya miaka 50 ya Mapinduzi watamani kutawaliwa tena?
Kama leo itapigwa kura, kuulizwa nani kati ya Abeid Amani Karume na Sultan Jamshid anayefahamika, jawabu lisilokuwa na hata chembe ya shaka ni Karume. Sultan hana mlango wa kuingilia Zanzibar.
Kabla ya Mapinduzi, Zanzibar haikuwa Jamhuri, ilikuwa chini ya Sultan, lakini Mapinduzi ya umma ndio yaliyoifanya Zanzibar kuwa Jamhuri.
Umoja wa Mataifa uliyatambua Mapinduzi hayo kuwa ni halali na uliokuwa Umoja wa nchi huru za Afrika (OAU) uliyatambua pia.
Sheria na mikataba ya kimataifa haitoi nafasi kwa Sultan kujipenyeza Zanzibar na wala hicho kiti chake huko UN hakipo, kilibiruka mwaka 1964. Kwa hiyo msipoteze muda kwa propaganda mfu na zisizokuwa na mashiko.
Vuguvugu la mabadiliko lililoanzia na Mapinduzi ya kule Ufaransa yaliamsha ari na kuwatia shime wazalendo wa Zanzibar kufanya Mapinduzi yaliyosimamiwa na kuratibiwa na ASP.
Athari za Mapinduzi ya Ufaransa zilienea kote duniani na ilipofika Januari 12, 1964, Wazalendo wa Zanzibar chini ya Afro Shiraz Party walirejesha heshima na utu kwa wakulima na wakwezi.
Wazanzibari sasa wanataka mabadiliko, hawatafanya kama wale wa Ufaransa isipokuwa watatumia haki ya kutoa mawazo yao, iwe wanataka Serikali tatu au mbili ni haki yao.
Saa ya mabadiliko imefika, vijana wasiokuwa na ajira, uhakika wa chakula wala kulala wamefikia pahala wanataka kuona mabadiliko ya kweli yanatokea siyo tu katika siasa bali hata katika uchumi na ndiyo maana wengi wanaunga mkono pendekezo la tume ya Jaji Warioba la kuwa na shirikisho.
Ni lazima wanasiasa wetu wafahamu kuwa ulimwengu wa leo, vijana haukubali tena kuburuzwa na mara nyingi vijana wa kileo waliozaliwa katika Teknohama wanaunga mkono siasa yenye uchumi na wanazuoni wanaipima hoja hiyo katika  mizania miwili; mosi, msukumo binafsi wa kijana wa Zanzibar wa uhitaji wa mabadiliko na pili, ni mhemko wa majira.
Mhemko huu ni kama kilevi ambapo kama ukweli ulivyo idadi kubwa ya vijana ndio wanywaji ambao hawatapenda kunywa kilevi kama togwa kisichokuwa na ‘stim’ yoyote kwao.
Demokrasia ya kisasa inalazimisha kuheshimu mawazo ya wengine hata kama huyataki, ndiyo maana watu makini wanaamini kuwa uvumilivu mzuri ni ule unaojiepusha na chuki zisizo na msingi (prejudice).
Hata kama anayetoa maoni au kueleza ni yule msiyeafikiana, au kimaumbile si mzungumzaji mzuri jaribu kuuweka sawa ujumbe wake kwa misingi ya nguvu ya hoja huku ukizingatia alichokizungumza siyo namna alivyozungumza. Mara zote chuki isiyo na msingi huviza mabadiliko.
Ikiwa dhana ya ujana ndio nguvu ya mabadiliko katika jamii, wanaobeza msimamo wa wale wanaotaka Serikali tatu, tumeona namna watu wa Zanzibar na Tanganyika walivyotoa mawazo yao kutaka mabadiliko ya msingi katika muundo wa Muungano.
 Watu wasijadili suala la muundo wa Muungano kwa jazba wala chuki kama ilivyoanza kujitokeza hivi karibuni kwa upande wa Tanganyika ambao wanawachukulia Wazanzibari kama wakorofi.
Hawa wanaokejeli wenzao tunawafahamu ndio masalia ya wanasiasa waliochoka kimawazo, wengine wana joto lao la kushindwa maisha na kukosa vyeo walipokuwa Serikalini, ndio leo wanamalizia hasira zao kwa wale wanaotoa hoja za kudai Muungano wenye usawa baina ya nchi ya Zanzibar na Tanganyika .
Haitawezekana kwa hali yoyote ile wananchi wa Zanzibar walio huru waliokataa kutawaliwa eti baada ya miaka 49 ya Mapinduzi watamani kutawaliwa tena na ukoloni wa Sultan!
Hili ni jambo la kushangaza kuona kwamba katika Afrika hii kuna watu wanamuota Sultan, napenda kuwaeleza kwamba Sultan na watu wake hawana hata chembe ya nafasi katika Zanzibar mpya, wala ya zamani.
Itakumbukwa pia kuwa mara tu baada ya Mapinduzi mwaka 1964, Rais wa kwanza wa Zanzibar, Abeid Amani Karume kama ilivyo kwa Mwalimu Nyerere naye alichukia sana ubaguzi na ndio maana aliongoza kampeni ya ndoa za mchanganyiko wa rangi na makabila mbalimbali hapa Zanzibar.
Mzee Karume hakulazimisha watu kuoana bali aliwataka wazazi wawape watoto wao uhuru wa kuoa na kuolewa na wawapendao. Waarabu hawakutaka mabinti wao waolewe na Waafrika ilhali, na kinyume chake baadhi ya Waafrika walikataa watoto wao kuoa Waarabu.
Chanzo: Mwananchi

Thursday 30 May 2013

MAPENDEKEZO YA KAMATI YA MARIDHIANO ZANZIBAR KUHUSU UPI UWE MWELEKEO WA WAZANZIBARI

MAPENDEKEZO YA KAMATI YA MARIDHIANO ZANZIBAR KUHUSU UPI UWE MWELEKEO WA WAZANZIBARI KATIKA KUIJADILI RASIMU YA KATIBA YA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA ITAKAYOTOLEWA NA TUME YA MABADILIKO YA KATIBA
UTANGULIZI:
… Baada ya wananchi wa Zanzibar kutoa maoni yao juu ya vipi Muungano wa Zanzibar na Tanganyika unapaswa kuwa, hatimaye Tume ya Mabadiliko ya Katiba inatarajiwa kutoa rasimu ya awali ya Katiba Mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kati ya mwishoni mwa mwezi Mei na mwanzoni mwa mwezi Juni 2013.
Wakati tunaisubiri kwa hamu rasimu hiyo itolewe na kujua kilichomo, sisi wajumbe wa Kamati ya Maridhiano Zanzibar tumekaa na kutafakari juu ya upi unapaswa kuwa mwelekeo wa Wazanzibari katika kuijadili rasimu hiyo pale itakapotoka.
Baada ya mashauriano ya kina kati ya wajumbe wa Kamati ya Maridhiano na pia kwa kuwahusisha watu wengine mashuhuri hapa Zanzibar, tumekuja na mapendekezo yafuatayo ambayo leo hii tunayawasilisha kwa wananchi wa Zanzibar kupitia Kongamano hili. Haya si maagizo bali ni mashauri yenu na pindi mkiyakubali basi tutakuombeni tuyafanyie kazi kwa pamoja kwa kuyatumia katika kuipokea na kujadili rasimu pale itakapotolewa.
Mapendekezo yetu ni kama ifuatavyo:
1. Jina la Muungano:
Muungano huu umetokana na Jamhuri mbili kuungana kwa hiyari. Jamhuri hizo ni Jamhuri ya Watu wa Zanzibar na Jamhuri ya Tanganyika. Jina la awali lililotajwa katika Mkataba wa Muungano la muungano wa jamhuri hizi mbili lilikuwa ni Jamhuri ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar. Jina hili baadaye mwezi Oktoba 1964 lilibadilishwa na kuitwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Ukiangalia mifano ya nchi nyingine zilizoungana, jina la muungano huweka bayana kwamba zilizoungana ni zaidi ya nchi moja, zaidi ya falme moja au zaidi ya jamhuri moja. Kwa mfano, muungano wa nchi (states) za Marekani unaitwa kwa kiingereza United States of America (USA), ule uliokuwa muungano wa jamhuri za kisovieti ukiitwa Union of Soviet Socialist Republics (USSR) na ule muungano wa falme za kiarabu unaitwa United Arab Emirates (UAE).
Ili kuondosha dhana iliyojengeka kwamba muungano wa jamhuri zetu mbili umeunda nchi moja na kuzifuta nchi zetu, Katiba Mpya inapaswa kuweka jina linalotambua msingi huo na historia hiyo. Hivyo basi, jina jipya liwe ni Muungano wa Jamhuri za Tanzania na kwa kiingereza United Republics of Tanzania.
Jina hili litasaidia utambulisho wa nchi wanachama katika uwanja wa kimataifa pale litapoambatanishwa katika nyaraka zote rasmi pamoja na jina la nchi husika. Kwa maana hiyo katika uwanja wa kimataifa na katika pasi za kusafiria utaweka wazi na kuwa na “UNITED REPUBLICS OF TANZANIA – REPUBLIC OF ZANZIBAR” na “UNITED REPUBLICS OF TANZANIA – REPUBLIC OF TANGANYIKA”.
2. Mipaka ya Zanzibar na Tanganyika:
Wakati zinaungana, Zanzibar na Tanganyika zilikuwa tayari ni nchi zenye mamlaka kamili zikiwa ni wanachama wa Umoja wa Mataifa na hivyo kila moja ilikuwa na mipaka yake inayoeleweka. Katiba na sheria za nchi mbili hizi ziliweka bayana mipaka hiyo na mipaka hiyo ilitambuliwa chini ya sheria za kimataifa.
Rasimu ya Katiba Mpya ni lazima itamke kwa uwazi kabisa na kutambua na kuheshimu mipaka ya nchi mbili hizi kama ilivyokuwa kabla ya siku ya Muungano tarehe 26 Aprili, 1964.
Baada ya hapo, Katiba ya Zanzibar na Katiba ya Tanganyika (itakayotungwa baada ya kupata Katiba mpya ya Muungano) kila moja iweke wazi mipaka yake.
3. Uraia:
Uraia ndiyo msingi wa ujananchi. Kwa vyovyote vile Katiba Mpya isijumuishe suala la Uraia kuwa la pamoja kupitia Muungano. Kila nchi mwanachama katika muungano ibakie na uraia wake na iratibu masuala yote yanayohusu uraia wake na raia zake. Kwa kufuata mfano kama wa Muungano wa Ulaya (European Union), unaweza kuwa na haki inayotambulika kikatiba ya uhuru wa raia wa nchi moja mwanachama kwenda katika nchi nyengine mwanachama kupitia utaratibu maalum utakaowekwa (free movement of people). Hata hivyo, kila nchi mwanachama iwe na haki ya kuweka utaratibu wa vipi raia hao watafaidi haki na fursa za nchi mwanachama nyingine.
Hili ni la muhimu hasa kwa nchi ndogo kama Zanzibar ambayo ina rasilimali ndogo ya ardhi na hasa ikizingatiwa kuwa ardhi ilikuwa mojawapo ya sababu kuu za kufanyika Mapinduzi. Katika hali kama hiyo, Zanzibar ina sababu nzito za kuona inadhibiti na kusimamia wenyewe Uraia wake na utambulisho wa raia hao.
Hivyo basi, suala la Uraia lisiwemo katika mambo ya Muungano na badala yake kila nchi isimamie yenyewe masuala ya Uraia.
Hata hivyo, kunaweza kukawepo chombo cha pamoja kinachojumuisha nchi mbili hizi cha kuratibu masuala ya Uraia na haki na fursa ambazo raia wanaweza kuwa nazo kwa kila upande.
4. Uhamiaji:
Kutokana na sababu tulizozitaja hapo juu kuhusiana na suala la Uraia inapelekea wazi kuwa kila nchi mwanachama idhibiti na kusimamia wenyewe mambo ya Uhamiaji. Hivyo basi, rasimu ya Katiba Mpya isijumuishe suala la Uhamiaji kuwa ni suala la Muungano.
Kila nchi mwanachama kati ya Zanzibar na Tanganyika iwe na paspoti yake yenyewe yenye kubeba jina la nchi yake na nembo yake ya Taifa na yenye kudhamini usalama wa raia wake nje ya nchi kupitia uhakikisho unaotolewa na Serikali ya nchi husika.
Ili kuonesha sura ya kuwepo muungano wa kisiasa, paspoti za nchi mbili hizo zinaweza kuwa na jina la Muungano juu na kufuatiwa na jina la nchi mwanachama likiambatana na nembo ya Taifa ya nchi hiyo. Kwa mfano, “UNITED REPUBLICS OF TANZANIA – ZANZIBAR PASSPORT” na “UNITED REPUBLICS OF TANZANIA – TANGANYIKA PASSPORT”.
Kwa upande mwengine kunaweza kukawa na mamlaka ya kuratibu masuala ya uhamiaji wa nchi hizi mbili (Union immigration regulatory authority) kwa lengo la kuweka na kuratibu mfumo mzuri wa mawasiliano kati ya mamlaka za uhamiaji za nchi mbili hizi.
5. Mambo ya Nje:
Mamlaka juu ya mambo ya nje na uwezo wa nchi kuingia mikataba na nchi nyingine na mashirika ya kimataifa ndiyo roho ya nchi yoyote duniani kutambulika kimataifa na kuweza kusimamia mamlaka yake ya ndani yanapohitaji mashirikiano na nchi nyengine.
Ili nchi iweze kutambulika kimataifa inapaswa kuwa na mambo manne yafuatayo:
(a) eneo la ardhi lenye mipaka inayotambulika;
(b) watu wanaoishi kwenye eneo hilo wanaojitambulisha na eneo hilo;
(c) serikali inayotekeleza majukumu yake; na
(d) uwezo wa kuingia katika mahusiano ya kimataifa na nchi nyengine.
Kwa msingi huo, Wazanzibari wanahitaji kuona kuwa Mambo ya Nje haijumuishwi katika orodha ya mambo ya Muungano na badala yake kila nchi isimamie yenyewe mamlaka yake juu ya mambo ya nje.
Hata hivyo, uratibu wa sera ya mambo ya nje (foreign policy coordination) inaweza kuwa ni suala la muungano lakini utekelezaji wake kila nchi ikausimamia kupitia Wizara yake ya Mambo ya Nje. Uratibu wa sera ya mambo ya nje unaweza kufanywa kupitia chombo cha pamoja kitakachoundwa na Wizara za Mambo ya Nje za nchi mbili hizi kwa mfano kuwa na Council on Foreign Policy.
Kutokana na hoja hizo hapo juu inabaki kuwa kila nchi iwe na uanachama na kiti chake katika Umoja wa Mataifa na jumuiya nyengine za kimataifa. Hayo si ajabu katika miungano. Umoja wa Jamhuri za Kisoshalisti za Kisovieti (USSR) ulikuwa na uanachama na kiti chake Umoja wa Mataifa lakini miongoni mwa nchi wanachama, Jamhuri tatu za Ukraine, Belarus na Georgia ziliamua kuwa na uanachama na viti vyao katika Umoja wa Mataifa na hilo liliwezekana.
Kwa msingi huo huo, Zanzibar iwe na uanchama wake katika Umoja wa Mataifa, Umoja wa Afrika, Jumuiya ya Madola, Jumuiya ya Afrika Mashariki, Jumuiya ya SADC na jumuiya nyengine za kikanda na za kimataifa.
6. Sarafu, Benki Kuu, Mikopo na Biashara ya Nchi za Nje, Ushuru wa Forodha, Kodi ya Mapato na Kodi ya Mashirika:
Uchumi si suala la Muungano hata katika Katiba inayotumika sasa. Hata hivyo, nyenzo za kuendeshea na kusimamia uchumi wa nchi kwa maana ya sera za fedha na uchumi (fiscal and monetary policies) zimeendelea kudhibitiwa kupitia Serikali ya Muungano.
Vyombo vikuu vinavyosimamia sera hizo ambavyo ni Benki Kuu (BOT), Mamlaka ya Kodi Tanzania (TRA) na Wizara ya Fedha ya Serikali ya Muungano vimekuwa vikifanya maamuzi na kuyatekeleza bila ya kuzingatia kuwa kwa maumbile uchumi wa Zanzibar ambao ni uchumi unaotegemea utoaji wa huduma (service oriented economy) hauwezi kuwa sawa na uchumi wa Tanganyika ambao unategemea rasilimali (resource based economy). Sera za fedha na uchumi zikiwemo zile zinazohusu udhibiti wa sarafu na viwango vya kodi, ushuru na riba katika mabenki zimekuwa zikitungwa bila ya kuzingatia msingi huo wa chumi mbili zilizo tofauti na badala yake mara zote zimeegemezwa kwenye kulinda maslahi ya uchumi wa Tanganyika.
Sarafu ya pamoja imekuwa ikishuka thamani kwa kasi kila uchao kutokana na sababu nyingi lakini miongoni mwake zaidi zinatokana na uendeshaji mbaya wa uchumi wa Tanganyika. Serikali inapochapisha sarafu zaidi ili kudhibiti mfumko wa bei athari zake zinaikumba pia Zanzibar.
Zanzibar inahitaji kujikomboa kiuchumi ili iweze kutekeleza malengo ya Mapinduzi kwa wananchi wake na hivyo inahitaji kuwa na mamlaka yake kamili katika kusimamia masuala ya sera za fedha na uchumi yakiwemo masuala yote yanayohusu sarafu, viwango vya kodi na ushuru pamoja na riba katika mabenki, mikopo na biashara ya nchi za nje.
Kutokana na hali hiyo, masuala ya sarafu, benki kuu, mikopo na biashara ya nchi za nje, ushuru wa forodha, kodi ya mapato na kodi ya mashirika kila nchi inapaswa iyasimamie yenyewe.
7. Polisi:
Pamoja na kuwemo katika mambo ya awali ya Muungano lakini uendeshaji wa Polisi umekuwa na matatizo yake katika muungano. Miaka yote Polisi Zanzibar imekuwa ikilalamika kuwa inachukuliwa kama vile ni Mkoa tu na hata bajeti na mahitaji yake mengine yanachukuliwa hivyo hivyo na makao makuu ya Polisi yaliyopo Dar es Salaam.
Katika nchi nyingi duniani Polisi ambayo inashughulika na usalama wa raia na mali zao imekuwa ikiendeshwa chini ya Serikali za Manispaa na hata Majimbo seuze kwa nchi kama ilivyo Zanzibar.
Ukiondoa mishahara na bajeti ndogo ya uendeshaji inayotolewa na makao makuu ya Polisi, gharama nyengine za uendeshaji wa polisi kwa Zanzibar zimekuwa zikichangiwa na mamlaka za Zanzibar ikiwemo Bodi ya Mapato Zanzibar (ZRB).
Hivyo basi, wakati umefika kuona mamlaka kuhusu Polisi yanaondolewa katika orodha ya mambo ya Muungano na kila nchi ishughulikie yenyewe Polisi yake.
8. Mafuta na Gesi Asilia (pamoja na maliasili nyengine zote):
Baraza la Wawakilishi la Zanzibar kwa niaba ya Wazanzibari lilishafanya maamuzi mwezi Aprili 2009 kuyaondoa masuala ya mafuta na gesi asilia kutoka kwenye orodha ya mambo ya Muungano. Mbali na maazimio ya Baraza la Wawakilishi, masuala ya mafuta na gesi asilia yanahusu uchumi ambalo si suala la Muungano.
Katiba Mpya haipaswi kuyajumuisha masuala hayo mawili (pamoja na maliasili nyengine kwa ujumla) kuwa mambo ya Muungano.
Hivyo basi, rasimu yoyote itakayoyajumuisha masuala hayo ya Mafuta na Gesi Asilia (pamoja na maliasili nyengine zote kwa ujumla) kuwa masuala ya Muungano haitakubalika kwa Wazanzibari.
9. Vyama vya Siasa:
Muungano uliundwa na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar na Jamhuri ya Tanganyika kupitia serikali zao. Mazungumzo yaliyopelekea muungano huo na hata utekelezaji wa hatua za kuunganisha nchi mbili hizi katika muungano hayakuhusisha vyama vya siasa vya wakati huo, ASP kwa upande wa Zanzibar na TANU kwa upande wa Tanganyika. Ndiyo maana kwa miaka 13 ya Muungano (kuanzia 1964 hadi 1977) kila nchi kati ya nchi mbili hizi iliendelea kuongozwa na chama chake cha siasa.
Moja kati ya dhoruba kubwa dhidi ya makubaliano ya asili ya muungano huu ambayo ni Mkataba wa Muungano ilikuwa ni kuunganisha vyama vya siasa vya ASP na TANU na kuunda CCM ambacho kilijitangazia kushika hatamu na kuwa juu ya vyombo vyengine vyote vya nchi zikiwemo Serikali. Utaratibu huo uliingizwa ndani ya Katiba za nchi na hivyo kuuhalalisha kisheria. Tokea wakati huo, Zanzibar imekosa mamlaka ya kisiasa ya kufanya maamuzi yake kwa mambo yanayoihusu. Na pale ilipofanya hivyo ilifanya kwa kutegemea na kujiamini kwa uongozi uliopo Zanzibar ingawa majaribio ya kutumia nguvu ya vyama kuzuia maamuzi kama hayo yamekuwa yakifanyika na baadhi ya wakati kufuzu.
Maongozi ya nchi yoyote yanategemea historia, mila na utamaduni wa watu wa nchi husika.
Kwa msingi huo basi, na ili Zanzibar iweze kurejesha mamlaka yake ya kisiasa katika kufanya na kusimamia maamuzi kwa mambo yake, rasimu ya Katiba haipaswi kujumuisha suala la vyama vya siasa kuwa ni jambo la Muungano. Zanzibar na Tanganyika kila moja iweze kuandikisha vyama vyake vya siasa.
10. Utaratibu wa uendeshaji wa Mambo ya Muungano:
Kwa yale mambo yatakayokubaliwa kubaki katika Muungano kama vile:
- Katiba ya Muungano wa Jamhuri za Tanzania;
- Serikali ya Muungano wa Jamhuri za Tanzania;
- Uratibu wa Sera ya Mambo ya Nje;
- Ulinzi;
- Usalama;
- Mamlaka juu ya mambo yanayohusika na hali ya hatari;
- Utumishi katika Serikali ya Muungano wa Jamhuri za Tanzania; na
- Mahkama ya Rufani ya Muungano wa Jamhuri za Tanzania.
Utaratibu wa uendeshaji wake uwekwe wazi katika Katiba kwamba maamuzi yote yatafanywa kwa mashauriano na makubaliano kati ya nchi mbili zinazounda Muungano huu na yatakuwa halali tu iwapo yatafuata msingi huu.
HITIMISHO:
Haya kimsingi ndiyo mapendekezo yetu Kamati ya Maridhiano. Tunayaleta kwenu muyapokee, muyajadili na kuwaomba muyaridhie ili yawe ndiyo msingi wa mwelekeo wa wananchi wa Zanzibar ambao wengi wao waliojitokeza mbele ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba walitaka nchi yao iwe na mamlaka kamili.
Kwa mapendekezo haya, tunadhani Zanzibar na Tanganyika zitaendelea kuwa na mashirikiano ya kidugu kupitia mfumo mpya wa Muungano na wakati huo huo kila nchi mwanachama wa muungano ikibaki na mamlaka yake kamili katika yake maeneo ya msingi ambayo kila nchi hupenda kuwa nayo.
Imetolewa:
Zanzibar
25 Mei, 2013
Source: Jussa’s Wall on facebook

Thursday 14 March 2013

WATANZANIA WAASWA KUNYWA MAJI KWA WINGI

WAZIRI MKUU Mizengo Pinda amewahimiza Watanzania kuwa na tabia ya kunywa maji mengi kila siku ili kujikinga na matatizo ya figo ambayo yanazidi kuongezeka kila siku. Ametoa wito huo leo mchana (Alhamisi, Machi 14, 2013) wakati akizungumza na mamia ya wananchi wa mji wa Arusha waliohudhuria kilele cha maadhimisho ya Siku ya Afya ya Figo Duniani yaliyofanyika kwenye viwanja vya hospitali ya AICC jijini humo. Kaulimbiu ya Siku ya Afya ya Figo Duniani mwaka huu ni “Figo Salama kwa Maisha yako: Epusha Madhara Makubwa kwa Figo” au “Kidneys for Life: Stop Acute Kidney Injury”. Waziri Mkuu
alisema mtoto wa miaka 10 hadi mtu mzima wanatakiwa wanywe maji kiasi kisichopungua lita moja na nusu kwa siku wakati mtoto mwenye mwaka mmoja anatakiwa anywe maji yasiyopungua nusu kikombe (sawa na mililita 100) na kwamba kiasi hicho huongezeka kadri umri wa mtoto unavyoengezeka. “Hii itasaidia kuhakikisha hawaishiwi maji mwilini,” aliongeza.
Kwa mujibu wa takwimu zilizopo, imekadiriwa kuwa watu milioni mbili hupoteza maisha kila mwaka kutokana na maradhi ya ghafla ya figo wakati asilimia 20 ya vifo vya wagonjwa waliolazwa hospitalini husababishwa na maradhi hayo.
“Wataalam wanasema maambukizi ya magonjwa hayo husababisha madhara makubwa ya figo (Acute Kidney Injuries) ambayo huchangia kwa kiasi kikubwa kuharibika kwa utendaji kazi wa figo. Hali hiyo husababisha watu kupata ugonjwa wa ghafla wa figo (mshtuko wa figo) na pia kusababisha athari kubwa kwenye figo na kuzifanya zishindwe kufanya kazi ipasavyo,” alisema.
Alisema maradhi yanayoweza kujitokeza ghafla na kuharibu figo hayajatiliwa mkazo ipasavyo, hasa katika nyanja za utoaji mafunzo ya tiba, utafiti na elimu ya afya ya figo kwa umma. “Hali hii husababisha kutotumika kikamilifu kwa fursa za kubaini maradhi yanayojitokeza ghafla na kuharibu figo; pia inaathiri utoaji huduma za afya ya figo usiokidhi, na hivyo wagonjwa kulazwa kwa muda mrefu hospitalini,” alisititiza.
Chanzo: MjengwaBlog

Saturday 9 March 2013

Sympathy ya wakenya yamnyanyuwa Kenyatta

Rais Kenyatta akipiga kura
Inavyoonekana katika uchaguzi wa Kenya ni jinsi gani wananchi wa Africa wasivokuwa na imani na mahakama ya kimataifa, duru nyingi zilimpa nafasi Odinga kuwa angeshinda kirahisi hasa ukitizamia kuwa Kenyata anakabiliwa na mashitaka kwnye mahakama ya ICC. Lakini wananchi wa Kenya wamemchaguwa mtuhumiwa kama vile ni kuionesha mahakama hiyo kuwa huyu munaemshitaki kwetu sisi ni lulu. Na tunasubiri tuone jee nchi za kiafrica zitamuunga mkno Kenyata au Marekani na mataifa mengine ya ulaya ambayo yalionesha wazi kumuunga mkono Raila Odinga? Nawapongeza wakenya kwa uzalendo halisi wa kujali utu wao na kutokuburuzwa na mataifa yasiyowapendelea mema. Tungojee tuone.Mungu ibariki Africa