Tuesday 29 November 2011

Kikwete amwaga wino Muswada wa Katiba

Tume ya Katiba kuundwa wakati wowote
  Wengi wapongeza maafikiano na Chadema
Siku 11 bada ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuupitisha Muswada wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ya mwaka 2011, Rais Jakaya Kikwete, ameutia saini ili uwe sheria ya kuruhusu kuundwa kwa Tume ya kukusanya maoni ya wananchi kwa ajili ya kuandika Katiba Mpya.
Taarifa iliyotolewa jana na Ikulu, ilisema kuwa Rais Kikwete aliusaini muswada huo jana na kuongeza kuwa hatua hiyo ya Rais itafutiwa na kutungwa kwa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ya Mwaka 2011 baada ya Bunge kuupitisha baada ya kuwasilishwa na Serikali katika Mkutano wa Tano wa Bunge uliomalizika hivi karibuni.
"Kutiwa saini kwa Muswada huo ili uwe Sheria ni hatua muhimu ya kutungwa kwa Katiba mpya ya Tanzania kama ilivyoahidiwa na Rais Kikwete katika salamu zake za Mwaka Mpya kwa wananchi Desemba 31, mwaka jana," ilisema taarifa hiyo.
Taarifa hiyo iliongeza kuwa, pamoja na kutiwa saini hiyo, bado Serikali itaendelea kusikiliza maoni na mawazo ya wadau na wananchi mbalimbali kuhusu namna ya kuboresha sheria hiyo.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Rais Kikwete anatoa wito kwa mwananchi yeyote mwenye maoni ama mawazo ya namna ya kuboresha Sheria hiyo, ajisikie yuko huru kutoa maoni yake na Serikali itasilikiza na kuchukua hatua zipasazo.
WADAU WAMPONGEZA JK, CHADEMA
Katika hatua nyingine, wadau mbalimbali wamepongeza uamuzi uliofikiwa baina ya Rais Jakaya Kikwete na Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na kutaka kujua ni mambo gani yaliyokubaliwa kufanyiwa marekebisho kabla ya kusainiwa kwa muswada wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba wa mwaka 2011.
DK. BANA: JK AMEONYESHA BUSARA
Akizungumza na NIPASHE kwa njia ya simu jana, Mhadhiri Mwandamizi wa wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk. Benson Bana, alipongeza mwafaka huo akieleza kwamba Rais Kikwete ameonyesha busara na hekima ya hali ya juu kwa kusikiliza maoni ya Chadema kama kundi mojawapo katika jamii.
Alisema kwa kufanya hivyo Rais Kikwete ameonyesha uungwana na uvumilivu wa kuweza kuyasikiliza makundi mbalimbali katika jamii, ikiwemo Chadema.
Kadhalika, Dk. Bana alisema Chadema wametumia busara kufuata njia ya mazungumzo kuwasilisha mawazo yao badala ya kutumia ‘nguvu ya umma’ kama ambavyo walikuwa wameazimia.
“Tunaipongeza Chadema kwa kuona milango ya kutoa maoni hata baada ya Bunge kupitisha sheria ile, Chadema wanahoja kwa sababu Katiba ilikuwa ajenda yao kwenye kampeni za mwaka jana…nawapongeza kwa kutotumia nguvu ya umma kwa sababu ina mshindo mkubwa kwa taifa, ina madhara makubwa,” alisema.
Alisema hoja ya Katiba iliipandisha Chadema chati na kwamba kwa kuwa serikali imekubali kuitekeleza ni vyema ikaibeba hoja hiyo bila kuvunja Katiba iliyopo.
Alisema kimsingi, mwafaka uliofikiwa baina ya pande hizo mbili haupo kwenye sheria yoyote hivyo hayawezi kuathiri upande wowote ulioonyesha dhamira ya kushughulikia kilichokubaliwa.
Kwa upande wake, aliyekuwa Mhadhiri Mwandamizi wa UDSM, Dk. Donath Olomi, alisema maamuzi ambayo ameyafanya Rais Kikwete ni mazuri kwa sababu amesikiliza maoni ya jamii ambayo walikuwa wanasema mchakato haukuwa mzuri.
Alisema inaonekana kuwa muswada huo una mapungufu na ndio maana jamii ilikuwa inataka ufanyiwe marekebisho hivyo ilikuwa vizuri kukubaliana na kufanya marekebisho katika suala hilo.
Dk. Olomi ambaye pia ni Mwenyekiti na Mkuu wa Taasisi ya mafunzo ya uongozi na ujasiriamali, alisema maamuzi hayo ni mazuri kwani amekubali kusikiliza yale mapungufu na kukubali kuyafanyia marekebisho.
KAULI YA MUFTI SIMBA
Naye Mufti wa Tanzania, Sheikh Mkuu Issa bin Shaaban Simba, alihoji kuwa maboresho hayo yanasaidia masuala ya dini? na kama ni ndio basi anayapongeza
“Hayo maboresho ambayo unanieleza yanasaidia mambo ya dini nijibu kama ni ndio basi nayapongeza,” alisema Sheikh Simba.
MAONI YA TEC
Katibu Mtendaji wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Padri Anthony Makunde, alipongeza na kueleza kuwa suala la Katiba linawahusu Watanzania wote.
“Jambo lolote linaloelekea katika kujenga amani na mustakabali wa nchi linastahili kupongezwa...tushirikiane Watanzania wote tuweze kutengeneza Katiba inayofaa kwa vizazi vya leo na vizazi vijavyo,” alisema Padri Makunde.
JUKWA LA KATIBA
Mjumbe wa kamati ya uongozi ya Jukwa la Katiba, Hebron Mwakagenda, aliponda makubaliano hayo akieleza kwamba hayajakidhi kiu ya wananchi kwa kuwa haijaelezwa bayana kilichokubaliwa na utekelezaji wake utaanza lini.
Alisema suala la Katiba si la Chadema na Serikali bali ni la Watanzania wote hivyo kitendo cha pande hizo mbili kufikia makubaliano hakitakidhi matarajio ya wengi.
Alisema msimamo wa jukwaa hilo uko pale pale kwamba wanamtaka Rais asiusaini muswada huo hadi hapo maoni ya wananchi yatakaposikilizwa na kuingizwa kwenye maboresho hayo.
“Walichokubaliana ni kama kilichotokea Zanzibar kati ya Rais Amani Abeid Karume na Maalim Seif ambacho hadi leo haijulikani nini kiliafikiwa kwa hakika kabisa, kwa hiyo msimamo wetu ni kutokubali Rais asisaini ule muswada,” alisema Mwakagenda.
KAFULILA: HAKUNA JIPYA
Mbunge wa Kigoma Kusini (NCCR-Mageuzi), David Kafulila, alisema mwafaka huo hauna jambo lolote jipya kwa kuwa kilichoafikiwa sicho kilichokuwa kilio cha wananchi wengi.
“Tulitoka nje ya Bunge kwa kupinga muswada ule usisomwe mara ya pili tukitaka usomwe mara ya kwanza, kwa sababu kanuni zilikiukwa, matumaini yangu yalikuwa kwamba Rais angekubali kuurudisha bungeni ili ukajadiliwe upya,” alisema Kafulila.
Aliongeza: “Sioni mantiki yoyote ya makubaliano na sijui kwa nini Chadema wamekubali kusaini makubaliano hayo, kilichofanywa na CCM kupitisha muswada ule kinadhihirisha wazi kwamba serikali yake haina dhamira ya kutunga Katiba.”
Kafulila alisema makubaliano hayo hayatakuwa na manufaa makubwa kwa sababu hayaonyeshi kuwasilisha kilio cha wananchi waliokuwa wanataka muswada usomwe mara ya kwanza.
CHANZO: NIPASHE

Saturday 26 November 2011

Utozaji ushuru mara mbili Bara, Z`bar waondolewa

26th November 2011
 
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA)
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), imewataka wafanyabaisha kutoka pande mbili za Muungano kuchangamkia biashara mbalimbali kwa kuwa kikwazo cha kulipa ushuru mara mbili kimeondolewa.
Awali, wafanyabiashara walikuwa wakilalamikia hatua ya TRA kuwatoza ushuru wanaponunua bidhaa Zanzibar na pia zinapofika Tanzania Bara zinatozwa tena.
Hayo yalisemwa jana jijini Dar es Salaam, na Ofisa Mkuu wa Elimu kwa Walipa Kodi Kanda ya Mashariki, Hamisi Lupenja, alipozungumza na waandishi wa habari.
Lupenja alisema ushuru huo uliondolewa kufuatia mapendekezo ya kamati maalum iliyoundwa na Rais Jakaya Kikwete, kwa ajili ya kushughulikia kero za Muungano.
Alisema hivi sasa ushuru unalipwa kwa upande mmoja tu wa Muungano kwa bidhaa mbalimbali tofauti na ilivyokuwa siku za nyuma, ambapo mfanyabiashara alikuwa akilipa Zanzibar na akifika Tanzania Bara analipa tena.
Lupenja alisema mpango huo umekwisha kuanza ingawa hakusema ulianza lini, lakini alikiri kuwa kwa sasa kuna unafuu kwa wafanyabiashara wa pande mbili za Muungano.
Wakati huo huo, TRA imeanzisha mpango wa kutoa elimu kwa wafanyabiashara wenye ulemavu wa kuona (vipofu), kwa lengo la kuongeza wigo wa ulipaji kodi kwa hiari.
CHANZO: NIPASHE

Friday 25 November 2011

SMZ yaitupia Serikali ya Muungano gharama za Katiba Mpya

Waziri wa Katiba na Sheria wa Zanzibar, Abubakar Khamis Bakary, amesema Zanzibar haitachagia gharama za kufanikisha mchakato wa kupata Katiba Mpya ya Tanzania.
Abubakary alisema hayo wakati anafunga mjadala kuhusu katiba mpya katika kongamano lililofanyika katika ukumbi wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo mjini hapa jana.
Alisema gharama zote za kufanikisha upatikanaji wa katiba mpya zitabebwa na Serikali ya Muungano ikiwemo vifaa, malipo ya makamishina wa Tume, Wajumbe wa Bunge la Katiba na watendaji wa tume.
“Mfuko wa Fedha wa Muungano ndiyo utatumika kufanikisha kazi zote na sie Zanzibar ndio tumenufaika zaidi katika hilo,” alisema.
Hata hivyo, hakutaja kiasi cha fedha ambacho kinatarajiwa kutumika kama gharama za kufanikisha upatikanaji wa katiba mpya ambayo inatakiwa kuwa imekamilika kabla ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.
Waziri Abubakary alisema wabunge na wajumbe wa Baraza la Wawakilishi watakuwa sehemu ya Bunge la Katiba pamoja wajumbe 116 ambao watatoka katika asasi za kiraia Tanzania Bara na Zanzibar.
Kuhusu kero za Muungano, Waziri huyo alisema wananchi watumie fursa hiyo kutoa maoni yao juu ya mambo ya msingi ya kuzingatiwa katika mabadiliko ya Muungano.
Alisema zipo kero za Muungano na kutoa mfano kwamba wapo mabalozi wa Tanzania nje ya nchi 30, lakini Wazanzibari ni watatu tu.
Waziri huyo alisema katiba ni mali ya wananchi na itajengwa na wananchi wenyewe na ndiyo maana serikali imeamua kuwapa nafasi wananchi ya kutoa maoni kabla ya kuandikwa upya kwa katiba hiyo.
Kuhusu urasimu wa upatikanaji wa Vitambulisho vya Mzanzibari Mkaazi, alisema wapo watendaji wa SMZ wamekuwa wakifanya vitendo hivyo kwa makusudi kwa malengo ya kutaka kuchafua hali ya kisiasa ya Zanzibar
Hata hivyo alisema Serikali ya Umoja wa kitaifa ipo macho na haitokubali kuona Wazanzibari wananyimwa haki ya kupinga kura ya maoni kwa kukosa Vitambulisho hivyo.
Viongozi wengine waliyoshiriki katika mjadala huo ni Waziri wa Afya, Juma Duni Haji; Waziri Asiye na Wizara Maalum, Haji Faki Shaari; Naibu Waziri wa Afya, Dk. Sira Ubwa Mamboya; Mrajisi Mkuu wa Serikali, Abdallah Waziri na viongozi wa vyama vya siasa Zanzibar.
CHANZO: NIPASHE

Wednesday 23 November 2011

Waziri- Z'bar ijadili Katiba kwa maslahi ya taifa

WAZIRI wa Katiba na Sheria Zanzibar, Abubakar Khamis Bakar amewasihi Wazanzibari kujadili Muswada wa Sheria ya Katiba kwa lengo la kupata Katiba mpya yenye maslahi ya Wazanzibari na Watanzania kwa ujumla.

Waziri huyo aliyasema hayo jana katika Ukumbi wa Baraza la Wawakilishi la zamani Kikwajuni mjini Unguja, alipozungumza na wananchi, wanasiasa pamoja na waandishi wa habari juu ya muswada huo na utaratibu wa kupatikana kwa Katiba mpya.

Alisema upatikanaji wa Katiba mpya yenye maslahi kwa Wazanzibari inatokana na kuwepo kwa umoja na uzalendo ambao unatanguliza maslahi ya Zanzibar mbele na siyo kujali maslahi ya vyama.

Aliwataka pia wananchi wa Zanzibar kujikusanya na kuipitia Katiba iliyopo na kuyajadili mapungufu yaliyomo katika Katiba hiyo ili muda utakapofika wa kutoa maoni juu ya Katiba mpya, wafanye hivyo.

Aidha, alisema muswada huo uliopitishwa karibuni na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambao pia unasubiri kutiwa saini na Rais Jakaya Kikwete ni mzuri na wenye kujali maslahi ya Zanzibar.

Waziri huyo wa Katiba na Sheria Zanzibar aliwatahadharisha wananchi kuwa makini na watu ambao wanaweza kuwapotosha wananchi katika kipindi hiki cha kujadili mchakato wa kupata Katiba mpya.

Kwa upande wa wananchi waliochangia katika mkutano huo wamewaomba viongozi na wanasiasa kupita katika majimbo yao ili kuendelea kuwaelimisha wananchi juu ya upatikanaji wa Katiba mpya.

Aidha, wameviomba vyombo vya habari Zanzibar kuandaa vipindi mbalimbali na kushiriki kikamilifu katika makongamano na warsha mbalimbali juu ya upatikanaji wa Katiba hiyo.

Ubepari wa ulaji riba na ufisadi hautufai…

Ahmed Rajab
NINAYAANDIKA haya nikiwa London,Jiji ambalo siku mbili hizi naona limejiinamia.
Kwa kawaida siku kama hizi huwa ni siku za kushangilia majani yanapopukutika na kubadilika rangi kuwa ya dhahabu badala ya kijani. 
Badala yake Jiji hili limeshika tama, likiwaza yaliyowasibu Wagiriki na  Wataliana.
Mambo yamechacha barani Ulaya na ya huko si hasha yakatambaatambaa na kufika katika fukwe za Uingereza. Wagiriki na Wataliana wote wameziona serikali zao zikiporomoka baada ya nchi mbili hizo kuelemewa na milima ya madeni.
Waziri Mkuu wa Ugiriki, George Papandreou, ambaye ni mtoto wa waziri mkuu na pia mjukuu wa waziri mkuu (babu yake aliwahi kuwa waziri mkuu mara tatu) alilazimika kujiuzulu ili aipe nafasi serikali mpya ya umoja wa kitaifa ijaribu kuunusuru uchumi wa Ugiriki. 
Yumkini moja ya njia zitazoufanya uchumi wa nchi hiyo upate afueni kidogo ni kwa Ugiriki kujitoa kwenye kanda ya nchi zinazotumia sarafu ya yuro ya Ulaya.
Waziri Mkuu wa Italia naye, Silvio Berlusconi, aliyekuwa waziri mkuu mara nne kuanzia mwaka 1994 alilazimika pia kuuacha wadhifa huo. 
Berlusconi amepata sifa au ila ya kuwa kichekesho cha Ulaya kwa kashfa za uasherati zilizomvaa.  Hatosahaulika kwa hafla zake za usiku wa manane ambapo anasemekana haikuwa fedheha kwake kuwafanya wasichana wabichi wawe wanacheza dansa wakiwa uchi. 
Mwenyewe akiziita hizo hafla zake kuwa ni ‘bunga bunga’. Kwa vile sasa hana kinga ya uwaziri mkuu huenda akaishia korokoroni kwa ufisadi huo na wa rushwa.
Berlusconi ameondoka madarakani lakini Wataliana wanapata taabu kuwa na serikali ya umoja wa kitaifa iliyo imara.  Hivyo, Italia huenda ikarejelea mtindo wake wa miaka ya 1960, 1970 na ile ya 1980 uliokuwa ukizifanya serikali za akina Aldo Moro, Mariano Rumor, Giulio Andreotti au za akina Francesco Cossiga, Arnaldo Forlani, Giovanni Spadolini au Amintore Fanfani ziwe zinaporomoka kila baada ya miezi michache au kama zimekaa sana basi kila baada ya mwaka au miaka miwili.
Masoko ya sarafu katika nchi za Magharini yametanabahi kwamba kitisho kwa chumi za nchi hizo hakitoki Ireland, wala hakitoki Uhispani au hata Ugiriki. Zinatambua sasa kwamba kitisho kubwa kwa nchi zilizo kwenye ukanda wa yuro kinatoka Italia.
Kweli deni la Ugikiri si dogo — ni kama yuro bilioni 350.  Lakini deni la Italia ni kubwa mno, takriban yuro trilioni mbili (idadi ambayo hata mtu hajui aiandike vipi kwa tarakimu).
Endapo Italia itanyimwa mikopo zaidi hatua hiyo itazua kuyayuka kwa fedha katika eneo zima la Bara la Ulaya. 
Hayo yatakuwa maafa makubwa si kwa Ulaya tu bali pia kwetu Afrika ambako chumi zetu zimekuwa kama mikia ya chumi za Ulaya.
Kwa hali ya mambo ilivyo sasa, kuna wasiwasi mkubwa kwamba Ufaransa huenda ikazifuata nyayo za Ugiriki na Italia na ikateleza.
Hapa Uingereza juujuu, bila ya shaka, mambo yanaonekana kama ni shwari.  Lakini wenye kuhodhi nyenzo za uchumi si nchini Uingereza tu bali pia hata Marekani na bila ya shaka huko Ujerumani na Ufaransa wanatambua fika kwamba hawana lao jambo.
Imekuwa kama kuna maradhi, tena maradhi mabaya ya kuambukiza, katika chumi za nchi za Magharibi kwa ujumla.  Ubepari umeachwa uchi; rabakitana. Na unachusha.
Mfumo wa wenye nguvu duniani umebiringitia juu chini. Miaka 150 iliyopita hakuna asiyejuwa nani aliyekuwa na nguvu kati ya Bara la Ulaya na China.
Wakati wa Vita ya Kwanza ya Kasumba pale Uingereza ilipoishinda China, Uingereza iliilazimisha China iilipe fidia. 
Si hayo tu bali Uingereza ikanyosha kono lake na kuitwaa Hong Kong. Isitosheke; ikaanza kuwalazimisha Wachina waziweke wazi bandari zao kwa wafanyabiashara Wakiingereza. Hali kadhalika Waingereza wakaitaka China isitumie sheria zake kuwahukumu raia wa Uingereza.
Madola mengine ya Magharibi nayo yakaanza kuitapia China. Yakaanza kuishurutisha iwape uhondo na marupurupu kama hayo waliyopata Waingereza.
Wakati mmoja Wachina waliishika meli iliyokuwa ikipeperusha bendera ya Uingereza na China ikakataa kuomba radhi. Tukio hilo likawapa Waingereza kisingizio cha kuingia tena vitani.  Ndipo ilipoanza Vita ya Pili ya Kasumba. 
Wafaransa nao wakajitosa vitani kuwasaidia Waingereza. Pamoja na Waingereza wakauteka mji wa Beijing na wakazichoma moto kasri kadhaa ambazo mfalme wa China akizitumia kupumzikia katika majira ya kiangazi.
Wafaransa haohao sasa hawana haya na wanaitaka China ilidhamini kifedha Bara la Ulaya.  Kwa ufupi, wanataka China iliokoe Bara la Ulaya na hasa zile nchi zilizo kwenye ukanda wa sarafu ya yuro.
Wachina wanasema hawajui kwa nini wavuke misitu na nyika kwenda kuokoa chumi za Ulaya au kutoa dawa ya kuyaponyesha maradhi ya Ulaya. 
Wafaransa bila ya shaka ni wajanja na wanajua wanachokitaka: wanainyatia ile akiba ya sarafu za kigeni ya China zenye thamani ya dola za Marekani trilioni 2.3.
Na hapa ndipo tunapopaswa kumdhukuru Mzee Karl Marx.  Sikatai kwamba mwanafalsafa huyo alikosea katika baadhi ya utabiri wake.  Wala sikatai kwamba nadharia zake za kisiasa, hasa kuhusu mambo ya utawala zilikwenda kombo.
Hata hivyo, anapohitaji kupongezwa natumpongeze.  Ilikuwa ni yeye aliyesema mwanzo kwamba misingi ya ubepari si thabiti; haiko imara. Matokeo ya hali hiyo ndiyo tunayoyashuhudia hivi sasa barani Ulaya na pia Marekani ambako kima cha wasio na ajira kimepanda kuzidi asilimia 9. Hukohuko Marekani pia kila uchao umasikini unakithiri.
Ubaya wa mambo ni kwamba nchi kama yetu inaona fahari kuzikumbatia sera za kiuchumi zinazowanufaisha wachache sana katika jamii.  Si hayo tu lakini wakubwa wetu wanazikumbatia sera hizo pamoja na maovu yake mengine kama vile ufisadi na ule utamaduni wa jamii ya mtu kumla mtu, chambilecho Julius Nyerere.
Aghalabu hao wenye kuwala wenziwao ni wale walio kwenye madaraka wenye kuyatumia madaraka yao kujinyakulia utajiri ambao mara nyingi huwa ni mali ya umma.
Waliokuwa wakisema Umarx umepitwa na wakati sasa wanasemaje wakiuona utabiri wa Marx kila siku unathibitika kuwa ni wa kweli?  Wala wasihoji kwa kuitaja China na kusema kwamba China imepiga hatua kwa sababu imeukanya Umarx.
Marx hakutaka nchi ziwe masikini.  Lengo lake daima lilikuwa kutaka pawepo na ustawi wa jamii na utajiri wa kiutu. Tafauti ya nadharia yake ni kwamba akitaka wafanyakazi, wenye kuzalisha mali kwa jasho lao, ndio wawe wenye kuuhodhi utajiri. 
Marx hakutaka pawepo jamii ya mabepari wachache wenye kuwanyonya wafanyakazi walio wengi. Akitaka pawepo uadilifu katika mahusiano ya kiuchumi.
Kila siku zikienda tutazidi kushuhudia kuporomoka kwa mfumo wa kibepari wenye kutegemea ulaji wa riba, unyonyaji na ufisadi.  Na kila siku zikizidi tutafungua macho na kuwashuhudia waathirika wakichukua hatua za kuuhujumu mfumo huo.
Hili vuguvugu tuliloliamkia ghafla hivi karibuni takriban katika nchi nyingi za Magharibi za maandamano dhidi ya mabenki ni mojawapo tu ya ushahidi huo.  Halijafika bado kwa kasi Afrika lakini utabiri wangu ni kwamba haliko mbali.
Kama halitochukua umbo kama hilo la Ulaya na Marekani basi huenda likachukua umbo jingine.  Uwezekano huo upo hasa sasa ambapo Marekani, Ufaransa na nchi za Ulaya zikiwa zinajitutumua na kujivimbisha kijeshi barani Afrika toka katika eneo la Sahel hadi Pembe ya Afrika.
Jingine litaloweza kuchochea hali hiyo ni ule uporaji wa ardhi za kilimo barani Afrika unaofanywa na makampuni ya kigeni kwa kushirikiana na vibaraka wa mabepari wenye kutawala sehemu nyingi barani Afrika.
Huko kujifurisha kijeshi kwa Marekani na nchi nyingine za Magharibi barani Afrika pamoja na uporaji wa ardhi na maliasili za Bara hilo ni ishara nyingine kwamba ubepari wa Kimagharibi unatapatapa na unatafuta njia za kujiokoa. Ndiyo maana wengine tunaushikilia ukomredi wetu.
Source: Raia Mwema

Wednesday 16 November 2011

EU, Marekani wajitosa mgogoro wa Katiba

WAKUTANA NA OFISI YA SPIKA, UPINZANI BUNGENI DODOMA
MVUTANO baina ya wabunge wa Chadema na NCCR Mageuzi kwa upande mmoja dhidi ya Serikali na wabunge wa CCM kwa upande mwingine, umevuta nchi wahisani ambao wametuma maofisa wake mjini Dodoma kuchunguza kiini cha mvutano uliopo. Ujumbe wa maofisa watano ukiongozwa na Balozi wa Sweden nchini, Lennart Hjelmaker ulifika katika Ofisi ya Spika wa Bunge, Anne Makinda na baadaye kukutana na Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Katiba, Sheria na Utawala, Pindi Chana, Waziri Kivuli wa Katiba na Sheria, Tundu Lissu na Mbunge wa Kigoma Kusini (NCCR Mageuzi), David Kafulila.
Imeelezwa kwamba ujumbe huo wa nchi ambazo ni wafadhili wa Tanzania, umehoji masuala mbalimbali kuhusu mchakato unaoanza sasa wa kuiwezesha Tanzania kupata Katiba Mpya.

Taarifa hizo zinasema, maofisa hao wengi wakiwa ni wale wanaohusika na ushauri wa masuala ya siasa katika balozi hizo, wamekuwa wakihoji hatima ya msimamo wa upinzani ambao waliamua kususia Muswada wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba wa mwaka 2011.
Chana akizungumza na kwa simu jana alikiri kukutana na ujumbe huo ambao pia uliwajumuisha maofisa kutoka balozi zilizopo kwenye mabano, Logan Wheeler (Marekani), Veslemoy Lothe Salvessen (Norway), Mark Polatjko (Uingereza) na Dk Carol McQueen (Canada).
Maofisa hao wakiambatana na wengine kadhaa, jana asubuhi baada ya kipindi cha maswali na majibu Bungeni, walitambulishwa na mmoja wa wenyeviti wa Bunge, Janister Mhagama wakiwa kwenye Ukumbi wa Spika.

Chana jana alisema: “Ndiyo nilikutana nao na walichotaka kufahamu tu ni jinsi mchakato mzima wa sheria hii ulivyokwenda na hatua zote tulizopitia kama kamati hadi kufikishwa kwake bungeni.

Alipoulizwa iwapo walihoji suala la Wabunge wa Chadema na NCCR Mageuzi kususia mjadala wa muswada huo, Mwenyekiti huyo alijibu kwa kifupi tu: “Ndiyo, hata hilo walitaka kufahamu lilivyokuwa.”
Imeelezwa pia kwamba ujumbe huo ulifika Ofisini kwa Spika Makinda, lakini haikufahamika mara moja kama walipata nafasi ya kuzungumza na kiongozi huyo wa Bunge, kutokana na jana kutokuwepo ofisini.

Wabunge wa upinzani
Juzi usiku, ujumbe huo ukiongozwa na Balozi Hjelmaker ulikutana na Lissu pamoja na mambo mengine ukihoji sababu za kutoka nje ya ukumbi wa bunge.
Ujumbe huo pia ulihoji hatua ambazo wapinzani hao wanakusudia kuchukua ikiwa Bunge litatumia wingi wa wabunge wa chama tawala kupitisha muswada huo, kisha kupata baraka za Rais na kuwa sheria ya nchi.
Pia walihoji iwapo kuna dalili zozote za kufanya mazungumzo ya kuwezesha pande husika kufikia mwafaka wa pamoja, ili wote waweze kushiriki katika mchakato wa kuwezesha nchi kupata Katiba Mpya.

Akizungumzia kukutana ujumbe huo Lissu alisema: “Ndiyo, nimekutana nao na wamehoji mambo mengi kwelikweli lakini niseme kwamba inavyoonekana wana hofu kuhusu investiment (uwekezaji) ikiwa hakutakuwa na makubaliano.”
“Nimewaambia kwamba sisi msimamo wetu ni kwenda kwenye mahakama ya wananchi, kuwaambia kwamba tumekataa kuhalalisha mchakato haramu wa upatikanaji wa Sheria maana tangu mwanzo kanuni na sheria za nchi zilikiukwa.”
Kwa upande wake, Kafulila pia alikiri kukutana na ujumbe huo jana, bila kuwapo kwa Balozi wa Sweden ambaye aliondoka Dodoma kurejea Dar es Salaam, baada ya kipindi cha maswali na majibu.

“Kwangu ni kama walitaka kufahamu kuhusu mambo matatu, kwanza kwa nini tuliamua kutoka nje, nilivyotumia nafasi yangu ndani ya Kamati ya Katiba, Sheria na Utawala nilipoteuliwa na Spika kuingia kwenye kamati hiyo na nini kinafuata ikiwa muswada huo utapitishwa na baadaye kuwa Sheria,” alisema Kafulila na kuongeza:

“Kwa kifupi nimewaambia kwamba sababu za kuondoka ziko wazi na tumezisema mara nyingi, lakini kubwa nimewaambia kwamba mimi mawazo yangu ni kuwahamasisha wanaharakati na hata wabunge wenzangu wa Chadema kuona kama tunakuwa na mchakato wetu, sambamba na ule unaofanywa na Serikali.”
Kafulila alisema mchakato huo utawawezesha wanaopinga wa Serikali kuwa na mfano wa bora na kwamba matokeo ya kazi hiyo, yatatumika kuushawishi umma wa Watanzania kupiga kura ya hapana dhidi ya Katiba ‘haramu’, inayokusudiwa kutungwa kutokana na mfumo ‘haramu’.

Siku za mjadala zaongezwa
Mjadala kuhusu muswada huo uliendelea jana na umeongezewa siku hadi leo utakapohitimishwa majira ya mchana.Habari zilizopatikana zinasema kuongezwa kwa muda wa majadiliano kunaweza kuathiri ratiba ya Bunge na kwamba upo uwezekano wa kuongezwa kwa siku moja ili Bunge liahirishwe Jumamosi.
Mkutano wa Tano wa Bunge, bado unakabiliwa na kazi ya kujadili muswada mmoja wa sheria na kupokea taarifa mbili za kamati ambazo kimsingi zinaweza kuhitaji kujadiliwa.

Taarifa hizo ni ile ya Kamati Teule ya Bunge iliyokuwa akichunguza tuhuma za Wizara za Serikali kuchangisha fedha kutoka katika taasisi zilizoko chini yake kwa lengo la kupitisha bajeti bungeni na ile ya Kamati ya Nishati na Madini kuhusu sekta ya gesi nchini.

Mashambulizi kwa upinzani
Jana,  Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Uhusiano na Uratibu), Stephen Wassira aliungana na Mawaziri Profesa Anna Tibaijuka wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi na Naibu Waziri Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Ummy Mwalimu kuchangia muswada huo na kutuhumu kauli zilizotolewa na Waziri Kivuli wa Sheria na Katiba, Tundu Lissu akisema ni mpotoshaji.

Wassira alisema anakishangaa Chadema kwani wakati wanagombea Urais mwaka 2010, walisema “Wakichukua tu madaraka nchi hii watahakikisha wanatubadilishia katiba ndani ya siku 100 lakini sasa hivi wanabadilika tena wanasema haraka ya nini.”

Alisema hata wasomi na wanaharakati nao pia wanawapotosha wananchi kwa kusema mambo yasiyo ya kweli kuhusu mchakato huo. Alisema wasomi wanadai kwamba Bunge linatunga Katiba wakati wanajua halina mamlaka hayo, badala yake wanatakiwa kupelekewa wananchi waipitie na kutoa maoni yao.

Kwa upande wake, Mbunge wa Bariadi Magharibi (CCM), Andrew Chenge alisema kuna kundi la watu linapotosha wananchi kwa kujiona wao wanachokitaka lazima kiwe hivyo hivyo. Chenge ambaye aliwahi kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali alisema kundi hilo linashinikiza wananchi kufuata maoni yao kwa sababu limejiaminisha kwamba wao pekee ndiyo wanaoweza kutoa maoni yao yakasikilizwa na zaidi ya Watanzania 40.

Naye Agripina Buyogela Kasulu Vijijini (NCCR), alisema  mchakato wa huo ufuate haki kwa kufuata hekima za Mwalimu Julius Nyerere wakati wa mchakato wa kura za maoni kuhusu vyama vingi. Alisema asilimia 80 ilikataa vyama vingi lakini asilimia 20 ilikubali lakini kutokana na hekima za Mwalimu ilibidi akubali kura za watu wachache, ndiyo maana mpaka leo kuna vyama vingi.

Muswada huo umekuwa ikipingwa na wasomi kupelekwa bungeni kujadiliwa badala yake wakitaka urejeshwe kwa wananchi.
Mwenyekiti wa Kigoda cha Taaluma ya Mwalimu Nyerere, Profesa Issa Shivji alisema unatakiwa kusomwa kwa mara ya kwanza. Alipendekeza Tume ya Katiba kuwa na wataalamu wasiozidi 20 badala ya 30, kwani idadi hiyo ni kubwa mno akitaka pia majina ya wanaotakiwa kuiunda wapendekezwe na vyuo vikuu na vyama vya kitaaluma na Rais ateue majina kutokana na mapendekezo hayo.

Nahodha aonya
Waziri wa Mambo ya Ndani, Shamsi Vuai Nahodha amelitaka Jeshi la Polisi kuwakamata wote wanaotishia hali ya amani kwa kutangaza kuitisha maandamano bila kikomo.

Nahodha alisema jeshi hilo linatakiwa kuchukua hatua hiyo ya kuwakamata wanaotishia usalama wa raia kwa kutoa maneno ya uchochezi kwa wananchi ya kuandamana kuhusu katiba kwani ni kosa.

Wakati Nahodha akisema hayo, Baraza la Vijana la Taifa la Chadema (Bavicha), kupitia kwa Mwenyekiti wake, John Heche limetangaza kufanya maandamano katika majimbo ya wabunge wote watakaounga mkono muswada huo.Habari hii imeandaliwa na Neville Meena, Dodoma Keneth Goliama, Hussein Issa na Geofrey Nyang'oro, Dar

Chanzo: Mwananchi

Tuesday 15 November 2011

Wabunge: Chadema Wanachochea vurugu

SIKU moja baada ya wabunge wa Chadema, kutoka nje ya Bunge na kutoshiriki mjadala wa Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Katiba wa mwaka 2011, wabunge wa CCM na CUF wamepinga hatua hiyo na kusema wenzao hao wana kusudio la kuchochea vurugu na kuvunja Muungano.

Pia wengi wa wabunge hao waliochangia wamemnyooshea kidole Msemaji wa Kambi ya Upinzani, Tundu Lissu, kuwa amewapotosha Watanzania na ni mwanasheria na mwanaharakati anayepaswa kurudi shule kusoma na pia ni mchochezi wa kutotaka Muungano na Wazanzibari.

Sambamba na hilo, wabunge hao waliochangia Muswada huo juzi na jana, walitetea madaraka aliyonayo Rais wakisema si makubwa na anastahili kuwa nayo kama kiongozi wa nchi.

Tofauti na wabunge hao wa CCM na CUF, Mbunge wa NCCR-Mageuzi wa Kasulu Mjini, Moses Machali, alikuwa pekee aliyewatetea Chadema kwa uamuzi wao wa kususia majadiliano hayo akisema wametekeleza matakwa ya wananchi.

Miongoni mwa waliochangia mjadala huo ni Mbunge wa Wawi, Hamad Rashid Mohammed (CUF) aliyesema “ni dhambi isiyosameheka kudharau Wazanzibari waliopiga kura ya Serikali ya Umoja wa Kitaifa halafu unajifanya wewe (Chadema) ni mkombozi wa watu, Lissu anasema Bunge la kikatiba halitakuwa na haki kwa sababu wabunge wa Zanzibar watashiriki !

“Mna ajenda yenu (Chadema) ya siri, mnaleta ubaguzi ndani ya Bunge, sisi (CUF) ndio tuliandamana kudai Katiba na tulipeleka rasimu ya Katiba, Watanzania wenzangu tusishawishike, maoni ya mabadiliko ya Muswada yametokana na wananchi, taasisi na Kamati ya Bunge, tuaminiane na tupendane,” alisema na kupinga wananchi kuandamana nchi nzima kupinga Muswada huo.

Alihoji kauli ya maoni ya Kambi ya Upinzani kuwa Rais ni dikteta wakati Rais huyo ndiye aliyeleta Katiba hiyo na kufafanua kuwa tangu mwaka 1977 hakuwahi kuona Muswada ulioshirikisha wananchi kama huo.

Alisema madaraka ya Rais yameshapunguzwa vya kutosha kama rasimu ya Katiba kupelekwa kwa wananchi kujadiliwa kabla ya kupitishwa, pamoja na hadidu za rejea kutotungwa na Rais isipokuwa zimeshawekwa kwenye Muswada kitendo ambacho Rais amekikubali.

Kwa upande wa Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Ummy Mwalimu, alilalamikia wanasheria na wanaharakati bungeni kwamba ndio wanapotosha ukweli kwa makusudi na kuwataka kuacha kupinga madaraka ya Rais kwa kumwangalia kama Mwenyekiti wa CCM, bali kama taasisi yenye madaraka na Katiba ya sasa na kuacha kumwita Rais dikteta.

“Mimi nimekuwa mwanaharakati, najua siasa za uanaharakati, waseme huko nyuma kuna maslahi ya nani...wakasome tena wanasheria hawa, si kuleta uchochezi katika nchi yetu,” alisema. Alisema Rais amefanya uungwana kuwaheshimu na kuleta Muswada huo bungeni kwa ajili ya kuunda Tume hiyo, vinginevyo Katiba iliyopo inamruhusu kuunda Tume bila hata kushirikisha wabunge.

Mbunge wa Simanjiro, Christopher ole Sendeka (CCM) pamoja na kutaka mamlaka ya Rais yasiingiliwe, alimtaka Lissu anayejiita mwanasheria na mwanaharakati kurudi darasani kuelimika kutokana na kupotosha historia ya nchi kwamba Mwalimu Julius Nyerere alihusika kumomonyoa Muungano kwa kutofuata haki za binadamu, wakati kipengele hicho kiliingizwa kwenye Katiba wakati wa utawala wake na Zanzibar kushirikishwa.

Mbunge wa Gando, Khalifa Suleiman Khalifa (CUF), alisema Chadema wakipata Dola hawatautaka Muungano wala Wazanzibari. Mbunge wa Viti Maalumu, Angela Kairuki (CCM), alishauri wajumbe wa Tume itakayoundwa walipwe kwa mujibu wa kanuni na malipo ya Serikali na si Waziri wa Katiba apange.

Pia Mwenyekiti wa Tume awasilishe ripoti bungeni na si Waziri wa Katiba na misingi na gharama za Bunge la Katiba ziainishwe kwa uwazi kwenye sheria.

Mbunge wa Tabora, Ismail Aden Rage (CCM) alisema wasiokubaliana na Muswada huo wanatafuta mwanya wa kuleta vurugu na kuongeza: “Wanaotaka kuhoji madaraka ya Rais ni wahuni … nimekerwa na kauli ya wenzetu wa Chadema, taarifa ya Lissu inalenga kuvunja Muungano”.

Hata hivyo, Mbunge Machali tofauti na wenzake, aliwatetea akisema “watakaopitisha Muswada huu laana za Watanzania ziwe juu yenu kwa sababu hamkutaka usomwe mara ya pili”.

Alisema wabunge kujikita katika malumbano kunazidi kujenga chuki na aliwatetea Chadema kutoka ukumbi wa Bunge kutokana na kushindwa kuvumilia na walifanya hivyo kupinga mwenendo mzima wa kuwasilishwa Muswada huo.

Katika hatua nyingine, Mbunge wa Mbozi Mashariki, Godfrey Zambi (CCM), aliomba mwongozo wa Spika wa kitendo cha Chadema kutoka nje na kama vyama vingine vitatoka nje, mjadala wa Bunge utaendeleaje. Spika, Anne Makinda alijibu:

“Tumekubaliana mikutano yote ya vyama ifanyike saa 7 mchana na watakaotoka katikati ya mjadala waombe ruhusa, Katibu wa Chadema hajaniomba wakutane baada ya kipindi cha maswali, nami nilivyowaona nimewachukulia kama wengine wanavyokwenda kunywa chai”.

Chanzo: Habari leo

CCM- Serikali ya Umoja Z’bar imedumisha amani

15/11/2011
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimesema uamuzi wake wa kuafiki kuundwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar, ulikuwa sahihi ili kuipa nafasi demokrasia ichukue mkondo wake.

Katibu wa Kamati Maalumu ya Halmashauri Kuu ya CCM (NEC) Zanzibar, Itikadi na Uenezi, Issa Haji Ussi alisema hayo jana katika mkutano wake na wajumbe wa Kamati ya Siasa Jimbo la Muyuni katika Mkoa wa Kusini Unguja.

Ussi alisema hatua iliyofikiwa ya kuundwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa kimsingi ililenga kuendeleza misingi ya amani, utulivu na umoja miongoni mwa Wazanzibari wote.

“Tumechukua uamuzi thabiti usioweza kusahaulika kwa maslahi ya usalama wa visiwa vyetu lakini kuipa nafasi demokrasia kuchukua mkondo wake hatua ambayo leo hii sote tunashuhudia ustawi wa demokrasia pamoja na amani na utulivu,” alisisitiza.

Alisema CCM ni chama chenye uwezo wa kutathmini na kupambanua mambo na kwamba utulivu uliopo hivi sasa Zanzibar unatokana na umahiri wa viongozi na wanachama wake.

Katibu huyo alisema CCM imesoma alama za nyakati na kufanikiwa kukwepa wimbi la pupa la mabadiliko ya pepo za mageuzi ya kidemokrasia.

Alisema kimsingi CCM imetumia jasho jingi katika meza ya mazungumzo ili kukataa kumwaga damu nyingi wakati wa vita.

Ussi aliwaeleza wanachama hao wa CCM kuwa uamuzi wa kuelekea kuundwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa ulipitishwa na vikao vya NEC na kwamba chimbuko lake lilianza tangu mwaka 1995.

“Ni dhamira na nia ya CCM ya siku nyingi iliyofanya hadi kufikiwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa, kimsingi tumechonga mwiko ili kunusuru mikono isiunguzwe,” alisema.

Hata hivyo aliwahimiza wana CCM kujipanga na kutambua kuwa ujio wa Serikali hiyo unatokana na utashi wa chama hicho bila ya kuwa na lengo la kuifuta Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.

Alisema kuwa Serikali iliyopo ni ya Mapinduzi ya Zanzibar chini ya mfumo wa Umoja wa Kitaifa na kwamba Rais wa Zanzibar Dk. Ali Mohamed Shein amekula kiapo cha kuongoza Serikali hiyo.

“Thamani ya utu wetu imetokana na Mapinduzi ya Januari 12 1964, ni upuuzi wa mwisho kuyapuuza Mapinduzi kwakuwa ni sehemu ya maisha na uhai wa kila Mzanzibari,” alisema

Chanzo: Habari leo

Maoni ya kambi ya upinzani kuhusu sheria ya marekebisho ya katiba 2011

UTANGULIZI

Mheshimiwa Spika,
Tarehe 11 Machi 2011, Serikali ilichapisha Muswada wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ya mwaka 2011 katika Gazeti la Serikali la tarehe hiyo. Muswada huo ulipelekwa katika Mkutano wa Tatu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano kwa Hati ya Dharura. Hata hivyo, baada ya upinzani mkubwa dhidi ya Muswada huo kujitokeza karibu nchi nzima, Bunge lililazimika kuondoa Hati ya Dharura na hivyo kufanya Muswada kushughulikiwa kwa mujibu wa utaratibu wa kawaida wa kutunga sheria uliowekwa na kanuni za 80, 83 na 84 za Kanuni za Kudumu za Bunge la Jamhuri ya Muungano, 2007. Katika kufanya hivyo, Bunge – kwa kupitia Spika – liliiagiza Serikali kufanya mambo yafuatayo kwa mujibu wa Taarifa Rasmi ya Majadiliano Katika Bunge (Hansard) ya Kikao cha Nane cha Mkutano wa Tatu cha tarehe 15 Aprili 2011:
(a) “Muda zaidi utolewe kwa Kamati na wananchi kuufikiria Muswada huu. Katika kufanikisha hili, “… iandae Muswada huu kwa lugha ya Kiswahili ili wananchi wenyewe waweze kusoma yaliyomo kwenye Muswada huo badala ya kupewa tafsiri tu na watu wengine;
(b) “Muswada uchapishwe kwenye magazeti na kutangazwa kwenye vyombo mbali mbali vya habari ili kutoa fursa ya kutosha kwa wananchi wengi kuuelewa na kuutolea maoni;
(c) “Utangulizi wa Muswada huu uwekwe vizuri zaidi ili wananchi waelewe madhumuni ya Muswada huu, kwani imeonekana wazi wananchi wengi wanadhani tayari tumeanza kuandika Katiba, kumbe lengo la Muswada huu ni kutunga Sheria ya Kuunda Tume ya Kukusanya Maoni tu.” (uk. 31-32)
Mheshimiwa Spika,
Katika kutoa maagizo haya, Bunge lilisitiza kwamba “… Muswada huu uko ndani ya Bunge, hauko serikalini.” (uk. 33) Hii ni kwa sababu, kwa mujibu wa kanuni ya 84(1) ya Kanuni za Bunge, Muswada ulikwishasomwa kwa mara ya kwanza na kupelekwa kwenye Kamati inayohusika kwa ajili ya kuanza kujadiliwa. Aidha, kwa mujibu wa kanuni ya 84(2) Kamati ilikwishaanza kupokea maoni ya wadau “… kwa lengo la kuisaidia katika uchambuzi wa Muswada huo.” Kazi iliyokuwa imebaki kwa Kamati ilikuwa ni kutumia mamlaka yake chini ya kanuni ya 84(3) “… kufanya marekebisho katika Muswada wa Sheria kwa kumshauri Waziri … anayehusika na Muswada huo kufanya mabadiliko….” Ni baada tu ya kupata ushauri wa Kamati kuhusu mabadiliko ndio Serikali ingeweza kuleta Jedwali la Mabadiliko kwa lengo la kufanya mabadiliko katika hatua hii kabla Muswada haujaletwa Bungeni kwa ajili ya kusomwa mara ya pili na kwa mjadala wa Bunge zima.
Mheshimiwa Spika,
Hakuna hata moja ya maagizo haya ya Bunge ambalo limetekelezwa na Serikali. Tafsiri ya Kiswahili ambayo imeletwa Bungeni – pamoja na kuonyesha imesainiwa tarehe 8 Machi 2011 sawa na Muswada wa Zamani uliopigiwa kelele sana na wananchi – ililetwa kwenye Kamati wiki mbili zilizopita, ikiwa ni wiki moja baada ya Kamati kukataa kuujadili Muswada Mpya kwa vile ulifanyiwa mabadiliko na Serikali bila kupata ushauri wa Kamati kama inavyotakiwa na kanuni ya 83(4) ya Kanuni za Bunge. Badala ya kutekeleza maagizo ya Bunge, Serikali imeleta Muswada wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ya mwaka 2011 ambao ulichapishwa katika Gazeti la Serikali la tarehe 14 Oktoba 2011.
Muswada huu mpya una tofauti kubwa na za kimsingi na Muswada wa Zamani kama nitakavyoonyesha hapa. Kwa maoni ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, mabadiliko makubwa na ya kimsingi yaliyofanywa kwenye Muswada wa Zamani yalihitaji na bado yanahitaji mjadala wa kitaifa wa wananchi kama ambavyo wengi wamedai katika mijadala inayoendelea nchi nzima. Aidha, Bunge hili tukufu lilihitaji, na bado linahitaji, muda zaidi wa kuyatafakari mabadiliko haya makubwa nay a kimsingi katika Muswada wa Zamani. Katika mazingira haya, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaamini ni busara na ni sound policy kwa Muswada huu Mpya kusomwa mara ya Kwanza ili kuruhusu mjadala unaohitajika kufanyika.
TUME YA MABADILIKO YA KATIBA
Mheshimiwa Spika,
Kama ilivyokuwa kwa Muswada wa Zamani, Muswada huu unapendekeza kuundwa kwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba ambayo, kwa mujibu wa Utangulizi wa Muswada, itawajibika “… kuratibu na kukusanya maoni ya wananchi juu ya Katiba (na) kuainisha na kuchambua maoni ya wananchi….” Kwa mujibu wa ibara ya 5, Tume hii itaundwa na Rais “kwa kushauriana na kukubaliana na Rais wa Zanzibar, na kwa ushauri wa Mwanasheria Mkuu wa Serikali wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar….” Aidha, kwa mujibu wa ibara ya 6(1), Rais atateua wajumbe wa Tume “… kwa kushauriana na kukubaliana na Rais wa Zanzibar….”
Ibara ya 6(2) inapendekeza kwamba “… muundo wa Tume utazingatia msingi wa kuwepo kwa uwakilishi ulio sawa kwa kila upande wa Jamhuri ya Muungano.” Pendekezo hili linarudia, kwa njia iliyojificha zaidi, msimamo wa ibara ya 6(2) ya Muswada wa Zamani iliyokuwa imeweka wazi kwamba idadi ya wajumbe wa Tume itakuwa sawa kwa sawa kwa pande zote za Jamhuri ya Muungano! Kama ilivyokuwa kwa Muswada wa Zamani, ibara ya 7(2) ya Muswada inapendekeza kwamba “uteuzi wa Mwenyekiti na Makamu Mwenyekiti utafanyika kwa msingi kwamba iwapo Mwenyekiti atatoka upande mmoja wa Jamhuri ya Muungano, basi Makamu Mwenyekiti atakuwa mtu anayetoka upande mwingine wa Jamhuri ya Muungano.”
Muundo wa Tume unakamilishwa na Sekretarieti ya Tume itakayoongozwa na Katibu. (ibara ya 13(1) Kwa mujibu wa ibara ya 13(2), Katibu huyo atateuliwa na Rais “baada ya kukubaliana na Rais wa Zanzibar.” Watendaji wengine wa Sekretarieti watateuliwa na Waziri “kwa makubaliano na Waziri mwenye dhamana ya mambo ya Katiba wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.”
Muswada unapendekeza kumpa Rais – baada ya makubaliano na Rais wa Zanzibar – mamlaka ya kutoa hadidu za rejea za Tume na muda wa kukamilisha na kuwasilisha ripoti. (ibara ya 8(1) Na kama hali itahitaji kufanya hivyo, Rais – “kwa makubaliano na Rais wa Zanzibar” – anaweza kuongeza muda usiozidi miezi mitatu ili kuwezesha Tume kukamilisha na kuwasilisha ripoti. (ibara ya 8(2) Hadidu za rejea, kwa mujibu wa ibara ya 8(3), “… zitakuwa ni hati ya kisheria ambayo Tume itaizingatia katika utekelezaji wa majukumu na utumiaji wa mamlaka yake kwa mujibu wa Sheria hii.”
Mheshimiwa Spika,
Ibara ya 9(1) ya Muswada inaelezea kazi za Tume kuwa ni pamoja na:
(a) Kuratibu na kukusanya maoni ya wananchi;
(b) Kupitia na kutafiti usahihi na ulinganifu wa masharti ya kikatiba yanayohusu mamlaka ya watu, mifumo ya kisiasa, demokrasia, utawala wa sheria na utawala bora;
(c) Kutoa mapendekezo kwa kila hadidu ya rejea; na
(d) Kuandaa na kuwasilisha ripoti.
Ijapokuwa haijaanishwa hivyo, ni wazi – kwa mujibu wa wa ibara ya 17(1)(d) na (2) ya Muswada – kwamba moja ya kazi za Tume ni kuandaa Rasimu ya Muswada wa Katiba mpya. Mapendekezo ya Muswada kuhusu Tume ya Mabadiliko ya Katiba ni muhimu na yanazua maswali mengi yanayohitaji mjadala wa kitaifa na maamuzi ya wananchi. Maeneo haya muhimu ni pamoja na nafasi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano katika mchakato mzima wa kutengeneza Katiba Mpya.
MAMLAKA YA RAIS
Mheshimiwa Spika,
Kama ambavyo tumepata kusema ndani ya Bunge hili, kwa muda wote wa uhai wetu kama taifa huru, mfumo wetu wa kikatiba na wa kisiasa umejengwa juu ya nguzo kuu ya Urais wa Kifalme (Imperial Presidency). Hii inatokana na ukweli kwamba katika mfumo huu, Rais ana madaraka makubwa sana ya kiutendaji na ya kiutungaji sheria. Vile vile Rais ana kivuli kirefu cha kikatiba juu ya mahakama kwa kutumia mamlaka makubwa aliyonayo katika uteuzi wa viongozi wote wa ngazi za juu za Mahakama. Urais wa Kifalme ndio chanzo kikuu cha kukosekana kwa uwajibikaji katika ngazi zote za serikali na ndio kichocheo kikubwa cha rushwa na ufisadi wa kutisha ambao umefanywa kuwa ni sehemu ya kawaida ya maamuzi ya kiserikali. Sio vibaya, katika kuthibitisha jambo hili, kurudia maneno ya ibara ya 37(1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, 1977: “… Rais atakuwa huru na hatalazimika kufuata ushauri atakaopewa na mtu yeyote….” Na kama alivyowahi kusema Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere kwenye mahojiano ya mwaka 1978 na Shirika la Habari la Uingereza (BBC), kama Rais wa Tanzania alikuwa na mamlaka – kwa mujibu wa Katiba na sheria za nchi yetu – ya kuwa dikteta!
Muswada unaendeleza kivuli kirefu cha Urais wa Kifalme katika mchakato wa upatikanaji wa Katiba Mpya. Mtu mwenye mamlaka ya kidikteta, kama Rais alivyo kwa mujibu wa Katiba ya sasa, hawezi kusimamia upatikanaji wa katiba ya kidemokrasia. Kwa kutumia mamlaka makubwa ya uteuzi wa Tume yanayopendekezwa na Muswada huu, ni wazi Rais Kikwete, ambaye pia ni Mwenyekiti wa chama tawala cha CCM, atateua wajumbe anaowataka yeye na Rais Ali Mohamed Shein, Makamu wake na pia Rais wa Zanzibar! Ni wazi vile vile kwamba watu watakaoteuliwa na Marais hawa ni watu wasiokuwa tishio kwa status quo kwa maana ya kupendekeza mabadiliko makubwa katika mfumo wa kikatiba na kiutawala na hivyo kuhatarisha maslahi ya CCM!
Mheshimiwa Spika,
Hali ni hiyo hiyo kwa Sekretarieti ya Tume ambayo ndio chombo cha kiutendaji na moyo wa Tume yenyewe. Kama Katibu, ambaye ndiye mtendaji mkuu wa Tume ni mteuliwa wa Rais na ni mtumishi wa Serikali; kama watendaji wengine wa Tume ni watumishi wa serikali walioteuliwa wa Waziri ambaye naye ni mteuliwa wa Rais baada ya kukubaliana na Waziri mwenzake wa Zanzibar; na kama watumishi wengine wa Tume nao ni watumishi wa Serikali kama inavyopendekezwa na ibara ya 13 ya Muswada Mpya, ni wazi, kwa hiyo, kwamba mapendekezo haya yote ya uteuzi wa wajumbe, watendaji na watumishi wengine wa Tume yana lengo moja tu: kuhakikisha kwamba matokeo ya kazi ya Tume hiyo ni yale tu yanayotakiwa na Rais na Serikali yake na chama chake cha CCM.
Mheshimiwa Spika,
Badala ya mapendekezo haya ya Muswada Mpya, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inapendekeza utaratibu wa kidemokrasia zaidi katika uteuzi wa Tume. Kwanza, badala ya Tume hiyo kuwa ‘Tume ya Rais’ kama inavyopendekezwa katika Muswada, tunapendekeza iwe ‘Tume ya Vyama’ (multiparty Commission) kwa maana moja kubwa: wajumbe wa Tume wateuliwe kufuatana na mapendekezo na makubaliano ya vyama vya siasa vyenye uwakilishi Bungeni, vyama vingine vilivyosajiliwa pamoja na mashirika ya kijamii, taasisi za kitaaluma na za kidini. Hii haina maana kwamba wajumbe wa Tume hiyo hawatatakiwa kuwa na sifa zilizoainishwa katika ibara ya 6(3) ya Muswada Mpya. La hasha! Wajumbe wa Tume ya Vyama watatakiwa kuwa na sifa zozote za kitaaluma zinazotakiwa ili kuwawezesha kufanya kazi ya kitaalamu kama inavyopendekezwa na Muswada Mpya.
Pili, baada ya uteuzi wa wajumbe wa Tume ya Vyama, inapendekezwa kwamba wajumbe walioteuliwa kwa mashauriano na makubaliano kama tunavyopendekeza watatakiwa wathibitishwe na Bunge la Jamhuri ya Muungano. Pendekezo hili litahakikisha kwamba wajumbe wa Tume wanakuwa vetted na chombo kikuu cha uwakilishi wa wananchi. Hili litajenga kuaminiana baina ya Serikali, vyama vya siasa, mashirika ya kijamii, taasisi za kitaaluma na za kidini na litaipa Tume ya Mabadiliko ya Katiba uhalali mkubwa wa kisiasa, kitu ambacho ni muhimu katika mazingira ya sasa ya kisiasa.
Mheshimiwa Spika,
Tofauti pekee na muhimu kati ya pendekezo la Muswada Mpya na pendekezo letu kuhusu mamlaka ya uteuzi wa wajumbe wa Tume ni locus ya uwajibikaji wao. Wajumbe wanaoteuliwa na Rais wanakuwa na shinikizo la kutoa matokeo yatakayompendezesha Rais au chama chake. Wajumbe wanaotokana na mapendekezo na makubaliano ya wadau wengi na wanaothibitishwa na chombo cha uwakilishi cha wananchi kama tunavyopendekeza hawawezi kuwa na shinikizo la kutoa matokeo yatakayompendezesha mmojawapo wa wadau hao. Faida kubwa na ya wazi ya Tume ya Vyama ni kwamba matokeo ya kazi yake yana nafasi kubwa zaidi ya kukubaliwa, kuheshimiwa na kutekelezwa na wadau mbali mbali kuliko matokeo ya kazi ya Tume ya Rais. Kwa lugha nyingine, kazi ya Tume ya Vyama itakuwa na uhalali wa kisiasa (political legitimacy) mkubwa zaidi kuliko Tume ya Rais.
Pendekezo hili linawahusu Katibu, watendaji na watumishi wengine wa Tume vile vile. Kutokana na uzoefu uliotokana na historia yetu na mfumo wetu wa kiutawala na kikatiba, watumishi wa serikali wamekuwa hawana uhuru wa kufanya maamuzi kwa kuzingatia utashi wao na uadilifu wa kitaaluma bali hufanya maamuzi kwa kuzingatia matakwa ya mabosi wao wa kisiasa. Hii ni kwa sababu, kisheria na hata kivitendo, watendaji na watumishi karibu wote wa umma hujiona wanawajibika kwa mamlaka zao za uteuzi, yaani Rais na/au Waziri. Aidha, watendaji na watumishi hawa wanawajibika kinidhamu kwa mamlaka zinazoongozwa na watendaji wa Serikali ambao nao ni wateuliwa wa Rais na kwa hiyo wanakuwa na woga wa kufanya maamuzi yanayoweza kuhatarisha maslahi ya kisiasa ya Rais na chama tawala.
Kwa sababu hizo, ni muhimu kwa watendaji na watumishi wote wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba wawe huru dhidi ya mashinikizo yoyote ya kisiasa kutoka kwa Rais na Serikali yake na chama chake. Ili Tume iwe na mamlaka na uhuru unaohitajika kwa ajili ya utekelezaji wa majukumu yake na ili isiingiliwe kweli na mtu au mamlaka yoyote kama inavyosema ibara ya 10 ya Muswada, inabidi mamlaka ya uteuzi yaondolewe katika mikono ya Rais na/au Waziri ambaye ni mdau mmojawapo tu wa wadau wengi wa mchakato wa Katiba Mpya. Na namna ya pili ya kuhakikisha uhuru huu unakuwepo ni kuweka utaratibu wa kuwapata watendaji na watumishi hawa nje kabisa ya utumishi wa serikali kwa kuweka masharti ya kuwataka waombe kazi, kufanyiwa usaili na kuteuliwa na jopo la wataalamu walio huru.
Mheshimiwa Spika,
Namna ya tatu ya kuhakikisha uhuru wa Tume katika kutekeleza majukumu yake ni kuhakikisha wajumbe wake wanapatiwa ulinzi wa ajira zao (security of tenure) sawa na wanaopatiwa majaji wa Mahakama ya Tanzania ili kuzuia uwezekano wa wajumbe kuondolewa kwa sababu zisizotokana na utendaji wao wa kitaaluma au ukosefu wa maadili. Kwa maana hiyo, mapendekezo ya ibara ya 10 Muswada Mpya juu ya uhuru wa Tume hayatoshelezi hata kidogo. Hii ni kwa sababu ibara ya 12 ya Muswada Mpya, ambayo inazungumzia ukomo wa ujumbe wa Tume, haijaweka utaratibu wowote wa namna ya kushughulikia nidhamu ya wajumbe pale kunapokuwepo tuhuma za ukiukaji wa Kanuni za Maadili zinazopendekezwa katika ibara ya 12(2) na Jedwali la Pili la Muswada. Kutokuweka utaratibu huu kuna hatari kubwa kwani, kisheria, mamlaka ya uteuzi huwa ndio mamlaka ya nidhamu pale ambapo sheria haijaweka utaratibu tofauti wa nidhamu. Hii ina maana kwamba bila kuweka utaratibu wa kisheria wa nidhamu ya wajumbe wa Tume, Rais ndiye atakuwa na uwezo wa kuwaondoa madarakani kwa sababu yeye ndiye aliyewateua!
Mheshimiwa Spika,
Pendekezo letu la tatu linahusu hadidu za rejea. Hapa kuna hoja za aina mbili. Kwanza, sambamba na pendekezo la kutompa Rais madaraka ya uteuzi wa wajumbe wa Tume, Rais asipewe mamlaka ya kutoa hadidu za rejea kwa Tume. Pili, kwa vile – kama inavyopendekezwa katika Muswada Mpya – hadidu za rejea ni hati ya kisheria inayotakiwa kuzingatiwa na Tume katika utekelezaji wa majukumu yake, ni muhimu hati hii iwekwe wazi katika sheria yenyewe badala ya kubakia kuwa siri ya Rais. Watanzania lazima wajue Tume inapewa majukumu gani ya kisheria. Aidha, wajumbe wa Tume wenyewe lazima wafahamu wanapewa majukumu gani ya kisheria na wafahamu kwamba wanatakiwa kufuata matakwa ya sheria na sio maelekezo ya mtu mmoja hata kama ni Rais wa Kifalme. Hii itasaidia uwajibikaji wa Tume kwa wananchi kwani itakuwa rahisi kupima matokeo ya kazi ya Tume kwa hadidu za rejea zilizowekwa wazi katika sheria.
Ukweli ni kwamba badala ya kumsubiri Rais kutoa hadidu za rejea, tayari ibara za 9 na 16 za Muswada Mpya zimeshafanya hivyo kwa kuainisha kazi za Tume, mipaka ya Tume katika utekelezaji wa kazi hizo na utaratibu wa namna ya kuzifanya. Kwa ajili hiyo, zaidi ya kutaka kuonyesha kwamba Rais ana mamlaka makubwa katika mchakato mzima wa upatikanaji wa Katiba Mpya, mapendekezo ya ibara ya 8 hayana maana wala sababu yoyote na yanaweza kuondolewa bila kuathiri maudhui ya Muswada. Aidha, kwa kuzingatia mapendekezo ya ibara ya 9, haijulikani Rais atatoa maelekezo gani ya ziada yanayohusu kazi za Tume na namna ya kuzitekeleza. Kwa upande mwingine, mapendekezo ya ibara ya 8 yanaweza kuleta mkanganyiko na mgogoro wa kisiasa na kisheria usiokuwa wa lazima endapo Rais atatoa hadidu za rejea zinazotofautiana na matakwa ya kisheria kama yanavyopendekezwa na ibara 9 ya Muswada Mpya. Pendekezo letu, kwa hiyo, ni kwamba ibara ya 8 ifutwe yote na ibara za 9 na 16 zifafanuliwe vizuri ili kuweka wazi zaidi hadidu za rejea za Tume na namna ya kuzitekeleza.
Mheshimiwa Spika,
Kuna mapendekezo mengine yaliyoko kwenye Muswada yanayoonyesha hatari za Urais wa Kifalme. Kama tulivyoona, Tume inatakiwa kuwasilisha ripoti yake kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano na kwa Rais wa Zanzibar. Baada ya hapo, kwa mujibu wa ibara ya 18(2) ya Muswada, “baada ya mashauriano na makubaliano na Rais wa Zanzibar na baada ya kumalizika kwa taratibu za ndani zinazohusu utungaji wa sera, Rais atamwelekeza Waziri kuwasilisha Muswada wa Katiba katika Bunge la Katiba kwa ajili ya kupitishwa kwa vifungu vya Katiba.”
Pendekezo hili ni la hatari kubwa. Kwanza, ‘kumalizika kwa taratibu za ndani zinazohusu utungaji wa sera’ maana yake ni baada ya kukamilika kwa utaratibu wa kawaida wa kiserikali unaohusu utungaji sera na sheria. Chini ya utaratibu huu, rasimu ya muswada hupelekwa kwanza kwenye Kamati ya Watalaam ya Baraza la Mawaziri (Inter Ministerial Technical Committee of the Cabinet) kwa ajili ya kufanyiwa marekebisho na Makatibu Wakuu kabla ya kupelekwa kwenye Baraza la Mawaziri kwa maamuzi ya mwisho. Baada ya maamuzi ya mwisho ya Baraza la Mawaziri, rasimu ya muswada hurudishwa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa ajili ya kuandikwa upya ndipo upelekwe Bungeni la Katiba.
Katika hatua zote hizi, muswada wa sheria huweza kufanyiwa marekebisho makubwa. Kwa maana hiyo, pendekezo la kuuwasilisha Muswada wa Katiba Mpya katika Bunge la Katiba baada ya kuupitisha kwanza kwa Makatibu Wakuu ambao wote ni wateuliwa wa Rais, na kwenye Baraza la Mawaziri ambalo wajumbe wake wote (ukiacha Makamu wa Rais na Rais wa Zanzibar) ni wateuliwa wa Rais ni kutengeneza mazingira ya kisheria yatakayoruhusu uchakachuaji wa Muswada huo kwa lengo la kuhakikisha matokeo yake ya mwisho, yaani Katiba Mpya, yanakidhi maslahi ya Rais na chama chake cha CCM. Kwa vyovyote vile, pendekezo hili halikubaliki kwa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni.
SIFA ZA WAJUMBE
Mheshimiwa Spika,
Muswada Mpya unapendekeza sifa zifuatazo wanazotakiwa kuwa nazo wajumbe wa Tume:
(a) Uzoefu katika kufanya mapitio ya katiba na sifa za kitaaluma za wajumbe kwenye mambo ya katiba, sheria, utawala, uchumi, fedha na sayansi ya jamii;
(b) Jiografia na mtawanyiko wa watu katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania;
(c) Maslahi ya umma;
(d) Umri, jinsia na uwakilishi wa makundi mbali mbali ya kijamii; na
(e) Vigezo vingine ambavyo Rais ataona vinafaa. (ibara ya 6(3)
Zaidi ya sifa zilizotajwa, ibara ya 6(4) inakataza watu wenye sifa zifuatazo kuteuliwa kuwa wajumbe wa Tume:
(a) Wabunge, wajumbe wa Baraza la Wawakilishi la Zanzibar, madiwani na viongozi wa vyama vya siasa wa ngazi zote kuanzia Wilaya hadi Taifa;
(b) Watumishi wa vyombo vya usalama;
(c) Watu waliowahi kuhukumiwa kwa kutenda kosa au wanaotuhumiwa mahakamani kwa mashtaka ya kukosa uaminifu au uadilifu;
(d) Watu wasiokuwa raia wa Tanzania.
Mapendekezo haya yana athari kubwa kwa mchakato mzima wa upatikanaji wa Katiba Mpya. Kwanza, kwa kukataza viongozi wa ngazi za juu na za kati wa vyama vya siasa kuteuliwa wajumbe wa Tume kunaondoa kwenye mchakato wa Katiba Mpya kundi kubwa la watu wenye utaalamu na uzoefu katika masuala mbali mbali ya kisiasa, kikatiba, kisheria, kiuchumi, kiutawala, kifedha na kisayansi jamii. Vile vile, viongozi wa vyama vya siasa wanawakilisha makundi makubwa ya kijamii yenye mtawanyiko wa watu na wa kijiografia katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, na wanawakilisha watu wa umri na jinsia zote kama inavyopendekezwa katika Muswada Mpya.
Aidha, kwa kuwa maneno ‘maslahi ya umma’ hayajafafanuliwa katika Muswada, hakuna anayeweza kudai kwamba viongozi wa ngazi za juu na za kati wa vyama vya siasa vilivyosajiliwa kisheria baada ya kutimiza masharti yote husika ya kisheria, na ambao wanaungwa mkono na mamilioni ya wananchi wa Tanzania kwa kupewa nafasi za uwakilishi katika taasisi za uwakilishi za umma kama Bunge, Baraza la Wawakilishi na Halmashauri za Serikali za Mitaa hawajui wala hawazingatii maslahi ya umma na kwa hiyo hawafai kuwakilishwa katika Tume ya Mabadiliko ya Katiba! Kama ingekuwa hivyo, Rais – ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM na kwa hiyo kiongozi wa chama cha siasa – naye pia atakuwa hana sifa za kuteua Tume! Na wakati haja ya kutoshirikisha watumishi wa taasisi za ulinzi na usalama katika mchakato wenye ubishani wa kisiasa kama utungaji wa Katiba Mpya inaeleweka, ni matusi kwa watu waliochaguliwa na wananchi kuwa Wabunge, Wawakilishi au Madiwani au viongozi wa vyama vya siasa vilivyowapendekeza watu hao, kuwekwa pamoja na wahalifu na kutamkwa kuwa hawana sifa za kuteuliwa kuwa wajumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba!
Inaelekea lengo kuu la pendekezo hili ni kuhakikisha kwamba vyama vya upinzani, hasa hasa CHADEMA, vyenye ushawishi mkubwa ndani na nje ya Bunge havipati fursa ya kuamua muundo na maudhui ya Katiba Mpya hasa katika hatua muhimu za uundaji wake. Pili, lengo kuu vile vile ni kuhakikisha kuwa Rais, na kwa hiyo chama chake cha CCM, wanadhibiti mchakato wa Katiba Mpya katika hatua muhimu ya uundaji wake. Endapo watafanikiwa katika hili, Rais na chama chake cha CCM watakuwa na nafasi kubwa ya kuamua aina ya Katiba Mpya itakayotokana na mchakato walioudhibiti kama inavyopendekezwa na Muswada Mpya. Hii ni kwa sababu, kwa kutumia uzoefu wa Tume nyingine zilizopata kuteuliwa miaka ya nyuma, wajumbe wengi huwa ni watumishi au waliopata kuwa watumishi wa Serikali na/au taasisi zake. Wajumbe wa aina hii wamekuwa hawana uthubutu wa kupendekeza mabadiliko makubwa yanayohitajika katika mfumo wa utawala wa nchi yetu.
Mheshimiwa Spika,
Badala ya kukataza viongozi wa vyama vya siasa kama inavyopendekezwa na Muswada Mpya, na kwa kuzingatia nafasi ya vyama vya siasa katika historia yetu na mfumo wetu wa utawala, na kwa lengo la kuhakikisha Tume inakuwa na utaalamu, uzoefu na uhalali wa kisiasa unaohitajika, watu wanaostahili kuteuliwa kuwa wajumbe wa Tume wawe ni wale wenye sifa zinazopendekezwa na ibara ya 6(3)(a), (b), (c) na (d) ya Muswada. Kwa sababu hiyo, hakutakiwi kuwa na vigezo vingine visivyojulikana wazi kwa wananchi. Kwa maneno mengine, pendekezo la kuwa na ‘vigezo vingine ambavyo Rais ataona inafaa’ halikubaliki kwani linampa Rais mwanya wa kuteua marafiki zake au watu ambao hawana sifa zinazojulikana. Kwa maoni yetu vile vile, badala ya kuwa sababu ya disqualification, uongozi wa kuchaguliwa na wananchi katika taasisi za uwakilishi au katika vyama vya siasa unatakiwa kuwa an added advantage pale ambapo kiongozi husika ana sifa za kitaaluma zinazotakiwa!
MISINGI MIKUU YA KITAIFA
Mheshimiwa Spika,
Muswada unapendekeza kuwepo kwa ‘misingi mikuu ya kitaifa’ ambayo Tume inatakiwa kuizingatia kwa lengo la kuihifadhi na kuidumisha. Misingi mikuu inayopendekezwa ni:
(a) Kuwepo kwa Jamhuri ya Muungano;
(b) Uwepo wa Serikali, Bunge na Mahakama;
(c) Mfumo wa kiutawala wa kijamhuri;
(d) Umoja wa kitaifa, amani na utulivu;
(e) Uchaguzi wa kidemokrasia wa mara kwa mara katika vipindi maalum kwa kuzingatia haki ya watu wote kupiga kura;
(f) Ukuzaji na na uhifadhi wa haki za binadamu;
(g) Utu, usawa mbele ya Sheria na mwenendo wa sheria; na
(h) Uhuru wa kuabudu na uvumilivu wa dini nyingine. (ibara ya 9(2)
Kifungu hiki kimefanyiwa mabadiliko kwa kufuta maneno ‘Tume itahakikisha … kutokugusika na utakatifu (inviolability and sanctity) wa mambo yafuatayo’ yaliyokuwa katika Muswada wa Zamani, na badala yake yamewekwa maneno mapya ‘… kuhifadhi na kudumisha mambo yafuatayo….’ Mabadiliko haya yamefanywa ili kujaribu kuondoa hofu iliyojitokeza wakati wa mikutano ya kukusanya maoni ya wadau kwamba lengo la pendekezo hilo lilikuwa kuzuia mjadala juu ya masuala ya kikatiba yenye utata mkubwa kama vile suala la Muungano. Hata hivyo, hatari ya kuzuiliwa kwa mjadala juu ya misingi mikuu ya kitaifa bado haijaondolewa kwani, kwa mujibu wa ibara mpya ya 9(3), “… Tume itatoa fursa kwa watu kutoa maoni yao kwa uhuru kwa lengo la kuendeleza na kuboresha masuala hayo.” Tafsiri halisi ya maneno haya ni kwamba mjadala pekee utakaoruhusiwa juu ya ‘misingi mikuu ya kitaifa’ ni ule ambao lengo lake ni ‘kuendeleza na kuboresha masuala hayo.’
Kwa maoni yetu, lengo kuu la pendekezo linalohusu kuendeleza na kuboresha ‘misingi mikuu ya kitaifa’ ni kuzuia mjadala wenye kuhoji ‘kuwepo kwa Jamhuri ya Muungano’ ili kuendeleza mfumo wa sasa wa Muungano wenye Serikali mbili. Hii ni kwa sababu katika mambo yote yanayopendekezwa kuwa misingi mikuu ya kitaifa, ni ‘kuwepo kwa Jamhuri ya Muungano’ yenye Serikali mbili ndio ambayo imekuwa na mgogoro mkubwa kwa muda wote wa maisha ya Jamhuri ya Muungano. Ukiacha ‘ukuzaji na uhifadhi wa haki za binadamu’ ambalo lilikataliwa na Serikali ya Mwalimu Nyerere kwa miaka yote ya utawala wake, mambo mengine yote yanayotajwa kuwa ‘misingi mikuu ya kitaifa’ hayajawahi kubishaniwa kwa miaka yote ya uhai wa Jamhuri ya Muungano.
Mheshimiwa Spika,
Pendekezo la ‘misingi mikuu ya kitaifa’ linastaajabisha sana kwani, kwa mujibu wa ibara ya 98(1)(b) ya Katiba ya sasa, ‘kuwapo kwa Jamhuri ya Muungano, Ofisi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano, madaraka ya Serikali ya Kamhuri ya Muungano, kuwapo kwa Bunge la Jamhuri ya Muungano, madaraka ya Serikali ya Zanzibar, Orodha ya Mambo ya Muungano na idadi ya Wabunge kutoka Zanzibar’ ni mambo yanayoweza kubadilishwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano ili mradi tu mabadiliko hayo yaungwe mkono na theluthi mbili ya Wabunge wote wa kutoka Tanzania Bara na wa Tanzania Zanzibar. Kwa sababu hiyo, pendekezo la ibara ya 9(3) ya Muswada kwamba ‘misingi mikuu ya kitaifa’ izungumzwe kwa lengo la kuiendeleza na kuidumisha tu halikubaliki kwa sababu linazuia uhuru wa kuhoji na/au kupinga mambo ambayo kwa Katiba ya sasa ni ruhusa kuyahoji, kuyapinga na/au hata kuyabadilisha! Tunapendekeza ibara ya 9(2) na (3) za Muswada zifutwe kabisa ili kuwepo na uhuru kamili wa kujadili, kwa kupinga au kuunga mkono, kila jambo linalohusika na Katiba Mpya.
NAFASI YA ZANZIBAR
Mheshimiwa Spika,
Pengine mabadiliko makubwa yaliyofanywa katika Muswada ni mapendekezo yanayohusu nafasi ya Zanzibar katika mchakato wa Katiba Mpya. Itakumbukwa kwamba moja ya masuala yaliyozua tafrani kubwa katika mchakato wa kukusanya maoni juu ya Muswada wa Zamani hasa katika kituo cha Zanzibar ni kuwepo hisia kwamba nafasi ya Zanzibar ilikuwa imepuuzwa katika Muswada huo. Muswada sio tu kwamba umetekeleza matakwa yote ya ushirikishwaji wa Zanzibar, bali umekwenda mbali zaidi kwa kuifanya Zanzibar mwamuzi wa mustakbala wote wa kikatiba wa Tanzania. Hii imefanyika kwa njia mbili: kwanza, kwa kumfanya Rais wa Zanzibar kuwa mshirika sawa wa kikatiba wa Rais wa Jamhuri ya Muungano; na pili, kwa kuipa Zanzibar nafasi kubwa ya uwakilishi katika mchakato mzima wa Katiba Mpya.
NAFASI YA RAIS WA ZANZIBAR
Mheshimiwa Spika,
Muswada unapendekeza kwamba utekelezaji wa mamlaka yote ya Rais, Waziri na Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano lazima ufanyike kwa ‘mashauriano na makubaliano’ na Rais, Waziri au Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar. Kwa mfano, ibara ya 5 inayohusu kuundwa kwa Tume inamtaka Rais ‘kushauriana na kukubaliana’ na Rais wa Zanzibar na kupata ushauri wa Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano na Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar. Vile vile, ibara ya 6(1) inayohusu uteuzi wa wajumbe wa Tume; ibara ya 8(1) na (2) inayohusu hadidu za rejea na kuongeza muda wa Tume; na ibara ya 13(2) inayohusu uteuzi wa Katibu wa Tume, zote zinataka kuwepo na makubaliano na Rais wa Zanzibar. Aidha, ibara ya 13(5) inayohusu uteuzi wa watendaji wengine wa Tume inalazimu makubaliano kati ya Waziri na Waziri mwenzake wa Zanzibar ambao nao ni wateuliwa wa Rais wa Jamhuri ya Muungano na Rais wa Zanzibar.
Mamlaka ya Rais wa Zanzibar hayaishii tu kwenye uteuzi wa wajumbe na watendaji wa Tume, bali pia yanaingia hata katika uwasilishaji wa ripoti ya Tume. Kwa mujibu wa ibara 18(1) ya Muswada, mara baada ya kumaliza kazi yake, Tume itawasilisha ripoti yake kwa Rais na kwa Rais wa Zanzibar. Aidha, kwa mujibu wa ibara ya 18(2), mara baada ya kupokea ripoti hiyo, Rais, ‘baada ya kushauriana na kukubaliana’ na Rais wa Zanzibar, “… atamuagiza Waziri kuwasilisha Muswada wa Katiba katika Bunge la Katiba.” Kwa mapendekezo haya pia, Rais wa Zanzibar sio tu kwamba ana mamlaka karibu sawa na Rais wa Jamhuri ya Muungano bali pia ana kura ya turufu katika mchakato wa Katiba Mpya. Maana yake ni kwamba Rais wa Zanzibar asipopatiwa nakala ya ripoti ya Tume au asipokubaliana na Rais wa Muungano, basi Muswada wa Katiba hautawasilishwa kwenye Bunge la Katiba!
Mheshimiwa Spika,
Mapendekezo haya yanaashiria kuwepo kwa mtazamo ambao chanzo chake ni Makubaliano ya Muungano kati ya Jamhuri ya Watu wa Zanzibar na Jamhuri ya Tanganyika ya tarehe 25 Aprili 1964. Kwa mtazamo huo, Zanzibar ni nchi huru kama ilivyokuwa mwaka 1964 na kwa hiyo ni lazima sio tu ishirikishwe kwa usawa, bali pia lazima ikubaliane na mabadiliko yoyote ya kikatiba yanayopendekezwa na Muswada. Kama Profesa Palamagamba Kabudi wa Kitivo cha Sheria cha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam alivyosema kwenye Semina ya Wabunge Juu ya Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Katiba iliyofanyika tarehe 12 Novemba 2011: ‘Katika kuandika katiba mpya, wabia wa Muungano wanarudi kwa usawa.’
Hata hivyo, Mheshimiwa Spika, mtazamo huu sio sahihi. Kwanza kabisa, Zanzibar sio nchi huru tena kama ilivyokuwa mwaka 1964, kama ambavyo hakuna tena nchi inayoitwa Tanganyika wala serikali yake. Hii ni kwa sababu tangu kusainiwa kwa Hati za Muungano mwaka 1964, na kwa mujibu wa ibara ya 4(3) ya Katiba ya sasa, masuala yote yanayohusu Muungano kama vile Katiba ya Tanzania yamekasimiwa kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano, ambayo pia imekasimiwa mamlaka juu ya masuala ya iliyokuwa Tanganyika. Masuala haya ya Muungano hayawezi kujadiliwa upya na kwa usawa kati ya nchi hizi mbili kwa vile moja kati ya nchi hizo haipo tena na iliyobaki imepoteza sehemu ya uhuru wake kutokana na Muungano huo! Hii ndio kusema hakuwezi tena kuwa na wabia wa Muungano bila kwanza kuirudisha Tanganyika kama nchi na bila kuirudisha Jamhuri ya Watu wa Zanzibar yenye uhuru na mamlaka kama iliyokuwa nayo kabla ya Muungano!
Pili, kuna dhana kwamba Rais wa Zanzibar hakushirikishwa katika mchakato wa maandalizi ya Muswada wa Zamani. Dhana hii vile vile ni potofu. Kwanza, Rais Ali Mohamed Shein mwenyewe ametamka wazi kwa waandishi wa habari kwamba alishiriki katika hatua zote za maamuzi kwenye Baraza la Mapinduzi. Pili, mujibu wa ibara ya 54(1) ya Katiba ya sasa, Rais wa Zanzibar ni mmoja wa wajumbe wa Baraza la Mawaziri la Serikali ya Jamhuri ya Muungano na kwa hiyo ni mshiriki wa maamuzi yote ya Serikali hiyo. Kwa maana hiyo, maslahi ya Zanzibar yanawakilishwa ndani ya ‘chombo kikuu cha kumshauri Rais’ katika Jamhuri ya Muungano. (ibara ya 54(3) Hii ni licha ya ukweli kwamba, kwa mlolongo wa madaraka uliopo katika ibara ya 54(2), Rais wa Zanzibar sio mmoja wa wajumbe wanaoweza kuongoza mikutano ya Baraza hilo.
Aidha, ndani ya Baraza la Mawaziri, Zanzibar inawakilishwa pia na Makamu wa Rais ambaye – kwa mujibu wa ibara ya 47(1) ya Katiba ya sasa – “… ndiye Msaidizi Mkuu wa Rais kuhusu mambo yote ya Jamhuri ya Muungano….” Kwa maana hiyo, mapendekezo ya Muswada yanayomfanya Rais wa Zanzibar kuwa sio tu mshiriki sawa lakini pia mwamuzi wa mustakbala wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano yanaenda kinyume sio tu na Katiba ya sasa bali pia na Hati za Muungano wenyewe. Kwa mapendekezo haya, endapo Rais wa Zanzibar hatakubaliana na uteuzi wowote wa wajumbe wa Tume au Katibu wake au watendaji wake wengine, anaweza kusimamisha mchakato mzima wa kikatiba hata kama unahusu masuala ya Tanzania Bara yasiyo ya Muungano!
UWAKILISHI WA ZANZIBAR
Mheshimiwa Spika,
Ushawishi mkubwa wa Zanzibar hauishii katika kura ya turufu aliyo nayo Rais wa Zanzibar pekee yake. Zanzibar ina ushawishi mkubwa vile vile kutokana na nafasi kubwa iliyo nayo katika vyombo vya maamuzi vinavyopendekezwa na Muswada. Kwa mfano, kwa mujibu wa ibara ya 6(2), “… muundo wa Tume utazingatia msingi wa kuwepo kwa uwakilishi ulio sawa kwa kila upande wa Jamhuri ya Muungano.” Hii ina maana kwamba wajumbe wa Tume na Sekretarieti yake wanatakiwa wawe sawa kwa sawa kati ya Tanzania Bara na Zanzibar. Ikumbukwe kwamba Tume hii inatengeneza Katiba inayohusu masuala ya Muungano, ambayo ni haki kwa Zanzibar kushirikishwa kwa usawa kabisa, na vile vile masuala yasiyokuwa ya Muungano ya Tanzania Bara ambayo Zanzibar haina haki ya kushiriki.
BUNGE LA KATIBA
Mheshimiwa Spika,
Eneo la pili ambalo Zanzibar ina ushawishi mkubwa kutokana na uwakilishi wake ni katika Bunge la Katiba linalopendekezwa katika Sehemu ya Tano ya Muswada. Kwa mujibu wa ibara ya 20(2), wajumbe wa Bunge la Katiba watakuwa ni wabunge wote wa Bunge la Jamhuri ya Muungano; wajumbe wote wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar; mawaziri wa katiba na sheria wa Jamhuri ya Muungano na wa Zanzibar; Wanasheria Wakuu wa Jamhuri ya Muungano na wa Zanzibar; na wajumbe mia moja kumi na sita wakaoteuliwa kutoka asasi zisizokuwa za kiserikali, asasi za kidini, vyama vya siasa vyenye usajili wa kudumu, taasisi za elimu ya juu na makundi yenye mahitaji maalum katika jamii. Inaelekea kwamba, kwa mujibu wa ibara ya 20(4), wajumbe wasiokuwa wabunge ama wawakilishi nao pia watateuliwa na Rais licha ya kutoka nje ya mfumo wa kiserikali!
Mheshimiwa Spika,
Kwa mujibu wa ibara ya 66(1)(a) ya Katiba ya sasa ya Muungano, wajumbe wa Bunge la Jamhuri ya Muungano ni pamoja na wabunge wa majimbo ya uchaguzi. Kwa composition ya sasa ya Bunge, kuna jumla ya majimbo ya uchaguzi 239 ambayo kati yao majimbo ya Zanzibar ni hamsini. Vile vile, kwa mujibu wa ibara ya 66(1)(c) ya Katiba, Baraza la Wawakilishi Zanzibar linawakilishwa na wabunge watano katika Bunge la Jamhuri ya Muungano. Aidha, kama inavyotakiwa na ibara ya 66(1)(b), kuna wabunge wanawake mia moja na mbili wanaojulikana kama ‘wabunge wa viti maalum.’ Kwa mgawanyo wa sasa wa wabunge hawa, idadi ya wanaotoka Zanzibar ni ishirini na tano kwa vyama vyote vyenye uwakilishi bungeni. Na mwisho, kuna wabunge wasiozidi 10 wanaoteuliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano kwa mujibu wa ibara ya 66(1)(e). Hadi sasa, Rais ameshateua wabunge watatu ambao wote ni wa kutoka Zanzibar. Kwa hiyo, katika Bunge la sasa lenye wabunge 353, wabunge wanaowakilisha Zanzibar ni themanini na tatu au karibu 23.5% ya wabunge wote wa Bunge la Jamhuri ya Muungano.
Kwa mujibu wa Sehemu ya Kwanza ya Sura ya Tano ya Katiba ya Zanzibar, wajumbe wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar ni pamoja na wawakilishi wa majimbo hamsini ya uchaguzi, wawakilishi kumi wa kuteuliwa na Rais wa Zanzibar na wawakilishi ishirini wa viti maalum na Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar. Kwa hiyo, jumla ya wajumbe wa Baraza la Wawakilishi kwa sasa ni themanini na moja. Kwa maana nyingine ni kwamba endapo mapendekezo ya ibara ya 20(1)(b), (c) na (d) ya Muswada yatakubaliwa, idadi ya wajumbe wa Bunge la Katiba wanaotoka Zanzibar itaongezeka hadi kufikia mia moja sitini na nne kati ya wajumbe 545 wa Baraza hilo kwa mujibu wa ibara ya 20(2). Idadi hii ni sawa na 30% ya wajumbe wote wa Bunge la Katiba.
Idadi hiyo ya uwakilishi wa Zanzibar bado haitakidhi matakwa ya Muswada kwani ibara ya 20(3) inapendekeza kwamba “… idadi ya wajumbe wa Baraza la Katiba kutoka Tanzania Zanzibar … haitapungua theluthi moja ya wajumbe wote wa Bunge la Katiba”! Theluthi moja ya wajumbe wa Bunge la Katiba ni wajumbe 182. Kwa hiyo ili kukidhi matakwa ya Muswada kuhusu uwakilishi wa Zanzibar, itabidi wajumbe 18 kati ya 116 waliotajwa na ibara ya 20(2)(e) watoke Zanzibar ili kufikisha idadi ya wajumbe 182 ambayo ndio theluthi moja ya wajumbe wote wa Bunge la Katiba.
Mheshimiwa Spika,
Kuna maeneo mengine ya Muswada ambayo pia yanazua maswali mengi juu ya nafasi ya Zanzibar katika mchakato wa Katiba Mpya. Kwa mfano, wakati ibara ya 21(1) inapendekeza kwamba Spika na Naibu Spika wa Bunge la Katiba wachaguliwe kutoka miongoni mwa wajumbe wa Bunge hilo, ibara ya 21(2) inapendekeza kwamba endapo Spika atatoka upande mmoja wa Jamhuri ya Muungano basi Naibu wake lazima atoke upande mwingine. Sambamba na pendekezo hili, ibara ya 22(1) inapendekeza Makatibu wa sasa wa Bunge la Jamhuri ya Muungano na wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar watakuwa ndio Katibu na Naibu Katibu wa Bunge la Katiba. Aidha, sawa na ibara ya 21(2), ibara ya 22(2) inapendekeza kwamba endapo Spika atatoka upande mmoja wa Jamhuri ya Muungano, basi Katibu wa Bunge la Katiba lazima atoke upande mwingine.
Mapendekezo haya yanaonyesha sio tu nafasi na ushawishi mkubwa wa Zanzibar katika mchakato wa Katiba Mpya, bali pia ni mwendelezo wa dhana potofu kwamba Zanzibar ni mshirika sawa wa Jamhuri ya Muungano. Hii inathibitishwa pia na pendekezo la ibara ya 24(3) ya Muswada inayotaka Katiba Mpya ikubaliwe na theluthi mbili ya wajumbe wa Bunge la Katiba wanaotoka Tanzania Bara na vile vile theluthi mbili ya wajumbe wanaotoka Zanzibar. Ni wazi, kwa hiyo, kwamba iwe ni kwa masuala ya Muungano yanayoihusu Zanzibar pia, au kwa masuala yasiyokuwa ya Muungano ya Tanzania Bara ambayo hayaihusu, Zanzibar itakuwa na kura ya turufu kwa mujibu wa mapendekezo ya Muswada huu.
Mheshimiwa Spika, Uwakilishi mkubwa wa Zanzibar katika Bunge la Jamhuri ya Muungano umetumika kihistoria kwa lengo la kuwatuliza Wazanzibari wakati Serikali ya Mwalimu Nyerere ilipokuwa inamomonyoa uhuru wa Zanzibar kwa kuongeza orodha ya Mambo ya Muungano kwenye Katiba ya Muungano. Katika kitabu chake Pan Africanism or Pragmatism? Lessons of Tanganyika – Zanzibar Union, Profesa Issa Shivji, mwanazuoni mashuhuri wa kikatiba na mwanafunzi wa historia ya Muungano huu amemnukuu aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar wakati wa utawala wa hayati Sheikh Abedi Amani Karume, Bw. Wolfgang Dourado akimnukuu Sheikh Karume juu ya nafasi ya Zanzibar katika Bunge la Jamhuri ya Muungano: “‘Msiwe na wasi wasi, sisi tuna haki ya kuwakilishwa katika Bunge lao lakini wao hawana haki ya kuwakilishwa katika Baraza letu la Mapinduzi’”!
Mheshimiwa Spika,
Sababu nyingine inatokana na kuongezeka kwa ushawishi na nafasi ya Zanzibar katika siasa za ndani ya CCM, hasa hasa katika zama hizi za vyama vingi na vita za makundi mbali mbali ndani ya chama hicho. Katika mazingira haya, mtu yeyote anayetaka kupitishwa kuwa mgombea urais kwa kupitia CCM anakuwa anahitaji kura za CCM Zanzibar ili kushinda katika kinyang’anyiro hicho. Kwa kauli ya Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere mwenyewe katika kitabu chake Uongozi Wetu na Hatima ya Tanzania, “sababu moja kubwa iliyofanya viongozi wetu wasitake kuwaudhi ‘Wazanzibari’ … ni umuhimu wa kura za Zanzibar katika kumteua mwanachama wa CCM kuwa Mgombea wa Urais wa Jamhuri ya Muungano. Kwa kiongozi yeyote anayeliona jambo hilo kuwa ni muhimu kupita mengine yote, kuwaudhi ‘Wazanzibari’ ni dhambi ambayo haina budi iepukwe kwa kila njia.” Kwa maoni ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, hofu hii ya kuwaudhi ‘Wazanzibari’ ndio imepelekea kimya kikuu – ndani ya CCM na ndani ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano – juu ya ukiukwaji mkubwa wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano uliofanywa na Sheria ya Mabadiliko ya Kumi ya Katiba ya Zanzibar, 2010.
Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaamini kwamba upendeleo wa Zanzibar unaopendekezwa katika Muswada huu kuhusiana na uwakilishi katika Bunge la Katiba na katika vyombo vingine vya maamuzi juu ya mchakato wa Katiba Mpya sio wa haki na haukubaliki tena. Kwanza, ibara ya 64(2) ya Katiba ya sasa inaweka wazi kwamba Baraza la Wawakilishi Zanzibar lina mamlaka ya kutunga sheria katika Zanzibar ‘… juu ya mambo yote yasiyo mambo ya Muungano….’ Hii pia ndio lugha ya ibara ya 78(1) ya Katiba ya Zanzibar kama ilivyofanyiwa marekebisho mwaka jana. ‘Katiba ya Tanzania’ ni jambo la kwanza katika orodha ya Mambo ya Muungano iliyoko kwenye Nyongeza ya Kwanza ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano. Kwa Muswada Mpya kupendekeza kwamba Baraza la Wawakilishi Zanzibar liwe sehemu ya Bunge la Katiba ni kukiuka wazi wazi matakwa ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano na ya Katiba ya Zanzibar. Ni ajabu iliyoje kwamba wale wanaojifanya ni machampioni wa Muungano wanaweza kunyamazia ukiukaji huu wa Katiba!
Mheshimiwa Spika,
Thomas Paine, mwandishi maarufu wa Marekani ya wakati wa Mapinduzi ya mwaka 1776, aliwahi kuandika kijitabu alichokiita Common Sense juu ya uhalali wa Uingereza kutawala Bara la Amerika ya Kaskazini ambako alisema: ‘… [T]here is something very absurd in supposing a continent to be perpetually governed by an island [for] in no instance hath nature made the satellite larger than its primary planet…’! Yaani, ni ujinga kudhani kwamba bara linaweza kutawaliwa milele na kisiwa kwa sababu utaratibu wa asili haujawahi kufanya kitegemezi kuwa kikubwa kuliko sayari yake ya msingi. Hata kama ni kweli kwamba Tanganyika sio bara kama ilivyokuwa Marekani ya Kaskazini, bado tunakubaliana na Tom Paine kwamba ni ujinga kudhani kwamba Visiwa vya Zanzibar vitaendelea kuwa na maamuzi na ushawishi mkubwa katika masuala yasiyokuwa ya Muungano ya Tanganyika kwa sababu utaratibu wa asili haujawahi kufanya maslahi ya Visiwa hivyo kuwa bora zaidi ya maslahi ya Tanganyika!
Kwa maoni yetu, wakati umefika kwa Muungano kuwekwa kwenye msingi wa usawa na imara zaidi. Msingi huo unahitaji kurudishwa tena kwa Serikali ya Tanganyika ambayo ndio ilikuwa – pamoja na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar – mbia mkuu wa Muungano wa mwaka 1964. Kurudishwa huko kwa Tanganyika kutaiwezesha Zanzibar kujadiliana nayo kwa usawa juu ya masuala yote yanayohusu Muungano. Haya yote yanawezekana tu endapo Muungano huu utawekwa mbele ya wananchi ili waamue – kwa kura ya maoni – kama wanataka kuendelea nao au la; na kama wanataka kuendelea nao ni muundo gani wa Muungano wanaoutaka.
Mheshimiwa Spika, Mapendekezo ya kurudishwa kwa Tanganyika na Serikali yake sio mapya. Miaka ishirini iliyopita, Tume ya Rais ya Mfumo wa Chama Kimoja au Vyama Vingi vya Siasa (Tume ya Nyalali) ilipendekeza hivyo hivyo. Miaka saba baadae, Tume ya Kukusanya Maoni Juu ya Katiba, White Paper Na. 1 ya 1998 (Tume ya Kisanga) nayo ilipendekeza hivyo hivyo. Kuendelea kupuuza mapendekezo haya wakati Zanzibar inavunja Katiba ya sasa ya Muungano; kuendelea kukaa kimya kwa hofu ya kuwaudhi ‘Wazanzibari’ wakati wao wanajitwalia uhuru wa kujiamulia mambo yao wenyewe huku wakiendelea kushiriki katika maamuzi ya mambo ya Tanganyika yasiyokuwa ya Muungano; kuendeleza kile alichokiita Mwalimu Nyerere falsafa ya ‘changu ni changu, chako ni chetu’ katika mahusiano ya Zanzibar na Tanzania Bara, ni kutulazimisha tuipinge dhana nzima ya Muungano kati ya nchi zetu mbili kitu kinachoweza kupelekea kuvunjika kwa Muungano wenyewe. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni isingependa tufike huko lakini ndoa hii ya kulazimishana haiwezi ikadumu muda mrefu kwa taratibu za aina hii.
UDHOOFISHAJI WA UPINZANI
Mheshimiwa Spika,
Mapendekezo ya Muswada juu ya uwakilishi katika Bunge la Katiba yana athari nyingine kubwa katika majadiliano na maamuzi ndani ya Bunge la Katiba. Kwa mujibu wa uchambuzi uliofanywa na Profesa Issa G. Shivji kwa Kamati ya Katiba, Sheria na Utawala, endapo mapendekezo ya ibara ya 20(2) ya Muswada yatapitishwa, CCM itakuwa na kati ya wajumbe 350 hadi 400 katika Bunge la Katiba ambalo lina wajumbe 545. Kwa upande mwingine Chama cha Wananchi (CUF) ambacho kina Wawakilishi 29 katika Baraza la Wawakilishi Zanzibar kitakuwa na wajumbe 65 katika Bunge la Katiba. Kwa maana ya uwakilishi katika Bunge la Katiba, CUF itakuwa ndio chama cha pili kwa nguvu za kisiasa ndani ya Bunge hilo, licha ya kuwa na wabunge wawili tu wa kuchaguliwa kwa upande wa Tanzania Bara na licha ya kupata kura chache sana katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana.
Na kama inavyojulikana, tangu Muafaka wa Kisiasa Zanzibar kati ya CCM na CUF wa mwaka 2010 na kuzaliwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa, upinzani wa kisiasa Zanzibar umekufa na kwa upande wa Tanzania Bara, na hasa Bungeni na kwenye chaguzi ndogo kama ule wa Igunga, CUF imekuwa ikishirikiana na CCM kuipinga CHADEMA. Kwa mapendekezo haya, kambi ya CCM na CUF katika Bunge la Katiba inaweza kufika hata zaidi ya wajumbe 465 katika ya wajumbe 545 wa Bunge hilo! CHADEMA ambayo kwa sasa ndio chama kinachoongoza Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kutokana na matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa 2010, itabakia na Wabunge wake 48 na vyama vya kibunge vilivyobaki, yaani NCCR-Mageuzi, TLP na UDP vitabaki na jumla ya Wabunge sita. Kwa hiyo, CHADEMA itakuwa chama cha tatu kwa nguvu za kisiasa ndani ya Bunge la Katiba licha ya kuwa ni chama kikuu cha upinzani chenye nguvu na ushawishi mkubwa wa kisiasa nchini!
Kwa maana nyingine, iwe ni kwa makusudi au bila ya kujua au kwa kunuia, athari mojawapo kubwa ya mapendekezo ya Muswada kuhusu uwakilishi katika Bunge la Katiba itakuwa ni kuiongezea nguvu zaidi kambi ya CCM/CUF na kupunguza nguvu na ushawishi wa CHADEMA ambayo ndio chama pekee kinachobeba matarajio na matamanio ya Watanzania wengi wanaotaka mabadiliko ya kimsingi ya kisiasa, kiuchumi na kijamii katika nchi yetu. Haihitaji kuwa na shahada ya uzamivu kujua kwamba Bunge la Katiba lenye uwakilishi wa aina hii litapitisha Katiba Mpya ambayo pengine itatofautiana na Katiba ya sasa kwa jina tu! Na wala haihitaji kisomo kikubwa kujua kwamba Bunge la Katiba la aina hii halitagusa ‘msingi mkuu’ uliobaki wa Jamhuri ya Muungano, yaani Serikali mbili. Hapa pia ni wazi kuwa lengo halisi la mapendekezo haya ni kuhakikisha kwamba mchakato wa Katiba Mpya utazaa matunda yasiyokuwa tofauti sana na ya Katiba ya sasa!
‘UWAKILISHI’ WA BUNGE LA KATIBA
Mheshimiwa Spika,
Sio Bunge hili tukufu la Jamhuri ya Muungano wala Baraza la Wawakilishi Zanzibar lenye mamlaka kikatiba na kisiasa ya kutunga Katiba Mpya ya Tanzania. Hii ni kwa sababu sisi wote tulioko humu ndani tulichaguliwa kwa mujibu wa Katiba ya sasa na mamlaka yetu yote yako ndani ya kona nne za Katiba hiyo. Kama ni kweli, kama anavyodai Profesa Kabudi, kwamba kitendo cha kutunga Katiba Mpya vile vile ni kitendo cha kuua Katiba ya Zamani, basi sisi Wabunge na Wawakilishi wa Zanzibar hatuna mamlaka ya kuiua Katiba ya sasa kwa sababu sisi wote tulikula kiapo cha kuilinda, kuihifandhi na kuitetea.
Pili, sisi sote ni Wabunge na Wawakilishi wa vyama vya siasa kwa sababu, kwa mujibu wa Katiba ya sasa sheria zote husika, tumechaguliwa kwa sifa kuu ya kuwa wanachama wa, na tuliopendekezwa na, vyama vya siasa. Kuligeuza Bunge la Jamhuri ya Muungano na Baraza la Wawakilishi Zanzibar kuwa Bunge la Katiba ni sawa na kusema kwamba wasiokuwa wanachama wa vyama vya siasa hawana haki ya kushiriki katika kutunga Katiba Mpya kwa sababu ya kuwa na kilema cha kisheria kinachowakataza kuchaguliwa kuwa Wabunge na Wawakilishi! Ibara ya 20(4) ya Katiba ya sasa inatamka wazi kwamba “… ni marufuku kwa mtu yeyote kulazimishwa kujiunga na chama chochote….” Sio kosa, kwa hiyo, kwa mamilioni ya Watanzania ambao wameamua kwa hiari zao kutokuwa wanachama wa vyama vya siasa. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni haikubaliani, na haiwezi kukubali, ubaguzi wa aina hii dhidi ya Watanzania walioamua kutumia haki zao za kikatiba ya kutokujiunga na chama chochote cha siasa. Aidha, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni haitakubali Watanzania hao waadhibiwe kwa kunyimwa kushiriki katika Bunge la Katiba kwa sababu tu ya kutokuwa wanachama wa vyama vya siasa.
Tatu, wajumbe 116 wanaopendekezwa kuteuliwa kwenye Bunge la Katiba kwa mujibu wa ibara ya 20(2)(e) na (4) ya Muswada Mpya sio, na hawawezi kuwa, wawakilishi wa wananchi. Kwanza, hawajachaguliwa na mtu yeyote na wala taasisi zao kuwawakilisha katika Bunge la Katiba kwa sababu Muswada Mpya unapendekeza wateuliwe na Rais. Pili, Bunge la Katiba ni chombo cha uwakilishi wa moja kwa moja wa wananchi na kwa mila na desturi zinazokubalika na kutumika kimataifa, wajumbe wa Bunge la Katiba huchaguliwa moja kwa moja na wananchi bila ya kujali vyama vya siasa na huwa na kazi moja tu: kutunga Katiba Mpya. Kwa sababu zote hizi, Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inapendekeza wajumbe wa Bunge la Katiba wachaguliwe moja kwa moja na wananchi na kusiwe na masharti yoyote kuhusu uanachama wa vyama vya siasa.
UHALALISHAJI WA KATIBA MPYA
Mheshimiwa Spika,
Muswada una mapendekezo ambayo yanaashiria kuachana na utaratibu wa kihistoria wa utungaji wa Katiba ambao umewaweka wananchi kando katika michakato wa kikatiba tangu miaka ya mwanzo ya uhuru. Kwa mujibu wa ibara ya 27(1), kutakuwa na kura ya maoni kwa lengo la kuihalalisha Katiba Mpya. Kwa mujibu wa ibara ya 30, watu wote walioandikishwa kuwa wapiga kura kwa mujibu wa Sheria ya Uchaguzi ya Taifa na Sheria ya Uchaguzi ya Zanzibar, watakuwa na haki ya kupiga kura katika kura hiyo ya maoni. Aidha, kufuatana na ibara ya 32(2), matokeo ya kura ya maoni yataamuliwa kwa msingi wa kuungwa mkono kwa zaidi ya 50% ya kura zote zilizopigwa Tanzania Bara na kiasi hicho hicho kwa Zanzibar.
Mapendekezo ya ushirikishwaji wa wananchi katika kuipa Katiba uhai wa kisheria ni jambo la maana sana na linaonyesha kuwa tumeanza kuachana na urithi wa kikatiba wa kikoloni ulioanza na Katiba ya Uhuru ya mwaka 1961. Hata hivyo, mapendekezo haya yamejaa mitego na vichaka vingi vya hatari. Kwanza, ibara ya 27 inapendekeza kwamba kura ya maoni itaratibiwa na kusimamiwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi kwa kushirikiana na Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar. Tume hizi mbili – kwa mashauriano na Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano na Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar – ndizo zitakazotengeneza swali litakaloulizwa kwenye kura ya maoni. (ibara ya 28(1) na (2) Aidha, kwa mujibu wa ibara ya 31, utaratibu utakaotumika katika kura ya maoni ni ule unaotumika katika chaguzi za kawaida katika nchi yetu, yaani Sheria ya Uchaguzi wa Taifa, Sheria ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, Sura ya 292 na Sheria ya Uchaguzi ya Zanzibar.
Mheshimiwa Spika,
Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inarudia kauli yake ndani ya Bunge hili wakati wa kujadili Makadirio na Matumizi ya Wizara ya Katiba na Sheria tarehe 24 Agosti, 2011: “Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni haina imani, sio tu na Tume ya Taifa ya Uchaguzi, bali pia na mfumo mzima wa kisheria na kitaasisi unaoendesha chaguzi za nchi yetu. Mfumo huu na watendaji wake wameonyesha wazi kutokuwa huru na kutumiwa na Chama cha Mapinduzi kuchakachua matokeo ya chaguzi mbali mbali hapa nchini. Kwa maana hiyo, Tume ya Uchaguzi ya Taifa, na ile ya Zanzibar, haiwezi kuachiwa jukumu kubwa la kuendesha kura ya maoni kwa ajili ya kupata Katiba Mpya. Kambi Rasmi ya Upinzani inapendekeza kwamba Serikali ilete bungeni muswada wa mapendekezo ya mabadiliko ya Katiba na ya sheria husika za uchaguzi kwa lengo la kuiunda upya Tume ya Taifa ya Uchaguzi kwa lengo la kuhakikisha inasimamia zoezi la kura ya maoni kwa uhuru na bila upendeleo kwa chama tawala.”
Kuna maeneo mengine ambayo nayo yanaonyesha kwamba lengo halisi la Muswada huu ni kupata Katiba ambayo haitabadilisha mambo ya msingi ila itakuwa mpya kwa jina tu. Kwanza, ibara ya 26(2) inapendekeza kumpa Rais mamlaka ya “kuliitisha tena Bunge la Katiba lenye wajumbe wale wale siku zijazo kwa ajili ya kutunga masharti ya katiba kabla ya kuizindua Katiba inayopendekezwa kwa lengo la kurekebisha masharti yaliyomo kwenye Katiba iliyopendekezwa.” Maana halisi ya maneno haya ni kwamba Rais atakuwa na mamlaka ya kuita tena Bunge la Katiba ili lifanye marekebisho ya mambo ambayo yeye au serikali yake au chama chake hawayapendi katika Katiba Mpya kabla haijapigiwa kura ya maoni na wananchi! Kama chombo huru cha wananchi, Rais hawezi kujipa madaraka ya kupingana na kauli ya wananchi kupitia Bunge la Katiba.
Pili, wakati ibara ya 32(3) inapendekeza kurudiwa kwa kura ya maoni endapo kura za ‘NDIYO’ na ‘HAPANA’ zitalingana, ibara ya 32(4) inaelekeza kwamba “endapo wingi wa kura ya maoni utakuwa ni ‘HAPANA’, Katiba ya Jamhuri ya Muungano ya mwaka 1977, itaendelea kutumika.” Endapo pendekezo hili litapitishwa na kuwa sheria, hii itakuwa ni kualika maasi kwa vile, kwa vyovyote vile, wananchi wa Tanzania – baada ya kupitia mchakato mrefu wa kutengeneza Katiba Mpya – hawatakubali tena kuvishwa minyororo ya Katiba ya sasa. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inapendekeza kwamba badala ya kurudi kwenye status quo ante kama inavyopendekezwa, mchakato wa Katiba Mpya uanze tena hadi hapo utakapopatikana muafaka wa kitaifa wa katiba.
HITIMISHO
Mheshimiwa Spika,
Muswada wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, 2011 ni Muswada muhimu kuliko pengine miswada yote ambayo Bunge la Kumi litapata fursa ya kuijadili na kuipitisha. Ni muswada wa kihistoria kwa vile, tangu uhuru wa Tanganyika miaka hamsini iliyopita, na tangu Muungano miaka karibu arobaini na nane iliyopita, Watanzania hatujawahi kupata fursa ya kujadili na kuamua mustakbala wa taifa letu kikatiba kwa utaratibu kama unaopendekezwa katika Muswada huu. Hata hivyo, kwa jinsi ambavyo Muswada huu ulivyoandaliwa na kwa maudhui yake na kwa jinsi ulivyoletwa Bungeni kwa kukiuka makusudi Kanuni za Bunge, ni wazi – kama utapitishwa jinsi ulivyo – Watanzania tutakuwa tumekosa fursa ya kuamua mustakbala wa taifa letu kwa njia ya amani na maridhiano. Bunge hili tukufu lina wajibu mbele ya historia na kwa vizazi vya sasa na vijavyo, kuhakikisha kwamba tunapata muafaka wa kitaifa juu ya Tanzania tunayoitaka. Hukumu ya historia, endapo Bunge hili tukufu litaendekeza ushabiki wa kisiasa na kufanya maamuzi ya mambo makubwa kama haya kwa kupiga kelele au kwa kuzomea au kwa kugonga meza kwa nguvu, itakuwa ni kali sana. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni haiwezi kuwa sehemu ya maamuzi makubwa kama yanayopendekezwa na Muswada huu bila kwanza wananchi wa Tanzania na Wabunge wenyewe kupata muda wa kutosha wa kuyatafakari masuala haya yote kwa uzito unaoyastahili na kuyafanyia maamuzi ya busara.
Kwa sababu hizi zote, Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja chini ya kanuni ya 86(3)(b) ya Kanuni za Kudumu za Bunge hili tukufu kwamba Bunge hili likatae Muswada huu Kusomwa Mara ya Pili kwa sababu Serikali imeleta Muswada Mpya na wenye mabadiliko makubwa na ya msingi bila kufuata masharti ya kanuni ya 84(3) ya Kanuni za Kudumu za Bunge; na pia kwa sababu Serikali haijatekeleza maagizo ya Bunge hili tukufu kuhusu kutoa muda zaidi kwa Kamati na wananchi kuufikiria, kuuelewa na kuutolea maoni Muswada huu kinyume na matakwa ya ibara ya 18(a) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano juu ya uhuru wa wananchi kutoa maoni yao; ibara ya 21(1) na (2) juu ya haki ya kushiriki katika shughuli za utawala wan chi, na haki na uhuru wa kushiriki kwa ukamilifu katika kufikia uamuzi juu ya mambo yanayowahusu wananchi, maisha yao au yanayolihusu Taifa.
Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha.
—————————————————————
Tundu Antiphas Mughwai Lissu (MB)
MSEMAJI, KAMBI RASMI YA UPINZANI BUNGENI
&
WAZIRI KIVULI, KATIBA NA SHERIA

Mwakilishi ahoji Rais wa Zanzibar kuapa Baraza la Mawaziri

15th November 2011

Makamu Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake Tanzania, (UWT) Asha Bakari Makame, amesema hajafurahishwa na Rais wa Zanzibar kula kiapo kuwa Waziri asiyekuwa na Wizara maalum katika Baraza la Mawaziri la Muungano.
Aliyasema hayo wakati akichangia muswada wa mabadiliko ya Katiba ya Muungano uliowasilishwa katika semina ya wajumbe wa Baraza la Wawakilishi na Waziri wa Katiba na Sheria Zanzibar Abubakari Khamis Bakari
“Mheshimiwa Mwenyekiti sijafurahishwa Rais wetu kuapishwa kuwa Waziri asiyekuwa na wizara maalum na lazima hilo liangaliwe upya katika Katiba mpya,” alisema Asha ambaye ni mwanasiasa mkongwe Zanzibar.
Alisema wajumbe wa Baraza la Wawakilishi wana dhamana kubwa ya kutetea maslahi ya nchi na kuwataka wajiamini hasa katika kutetea maslahi ya Zanzibar katika kuelekea mchakato wa kupata Katiba mpya ya muungano
Hata hivyo Waziri wa Kilimo na Maliasili Zanzibar, Mansoor Yussuf Himid, alisema kuwa, Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohammed Shein, hastahili kulaumiwa kwa sababu ametekeleza matakwa ya Katiba na jambo hilo limeanza kabla ya uongozi wake.
“Rais tusimlaumu kwa jambo alilolikuta, kama hatutaki tuliondoshe na wakati wake ndio huu” alisema Mansoor.
Hata hivyo, alisema kwamba muswada wa kuweka utaratibu wa mabadiliko ya Katiba baada ya kupitishwa na bunge, lazima pia upitishwe na Baraza la Wawakilishi kabla ya kuanza kutekelezwa kwa sheria hiyo.
“Tusije kukubali muswada kupitishwa bungeni iwe mwisho, lazima uletwe Baraza la Wawakilishi kabla ya kuanza utekelezaji wake” alisema Mansoor ambaye pia mweka Hazina CCM Zanzibar.
Nafasi ya Rais wa Zanzibar kuwa Makamu wa Rais wa Muungano ilifutwa baada ya mabadilko ya 11 ya Katiba Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kufuatia kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vingi mwaka 1992 na kuanzishwa nafasi ya mgombea mweza kuwa makamu wa rais wa mungano
Kwa mujibu wa Ibara ya 54 (1) ya Katiba ya muungano, Rais wa Zanzibar anakuwa mjumbe wa Baraza la Mawaziri katika serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
CHANZO: NIPASHE