Wednesday 25 April 2012

Yasemwayo kuhusu Muungano yasikilizwe

KESHO tarehe 26 Aprili Jamhuri ya Muungano ya Tanzania, yaani Muungano kati ya Tanganyika na Zanzibar utatimiza miaka 48, ukikaribia nusu karne. Huo si umri mdogo.
Bara siku hiyo itasherehekewa rasmi. Zanzibar itapita tu huku wengi wa wananchi wake wakiwa wanaguna na kujiuliza kwa muda gani Muungano huo utaendelea kuwako kama hivi ulivyo katika muundo wake wa sasa.
Kwa namna tunavyoiona hali ya mambo ilivyo hivi sasa Visiwani wananchi wa moto na hakuna suala kubwa la kisiasa linalowashughulisha zaidi ya hili la Muungano. Haya yanaonekana bayana unaposikiliza maoni ya wananchi katika majukwaa ya kuhamasisha watu katika mchakato wa katiba mpya ya Jamhuri hiyo na pia katika majukwaa ya mawasiliano ya kijamii.
Serikali inaweza kuyapuuza maoni hayo na inaweza pia ikatumia mkono wa chuma katika jaribio la kuyazima maoni hayo. Ikifanya hivyo itafanya kosa kubwa sana. Si tu kwamba itakuwa inakwenda kinyume na maadili ya utawala bora na kwamba itakuwa inawanyima wananchi haki na uhuru wao wa kutoa mawazo wayatakayo lakini pia itahatarisha amani. Mrindimo na mngurumo uliopo sasa Visiwani kuhusu Muungano hauwezi kuzuiwa kwa matumizi ya nguvu.
Lakini wenye maoni ya kuupinga muundo wa Muungano kama ulivyo hivi sasa nao pia wana jukumu la kuendesha kampeni zao kwa njia ambazo hazitotishia amani. Wakifanya vitendo vyenye kukiuka sheria au hata wakianza kutumia matusi katika hoja zao huenda wakahatarisha mengi zaidi ya amani na hali ya utulivu.
Mwenye macho haambiwi tazama na mwenye masikio hawezi kuepuka kuyasikia maoni ya Wazanzibari dhidi ya muundo wa sasa wa Muungano na mengine dhidi ya kuwako kwa Muungano wenyewe. Maoni haya yanasikika kutoka kwa wanachama wa vyama vyote vya kisiasa nchini humo na pia hata kutoka kwa wale wasio wanachama wa vyama vya kisiasa au hata wasiopendelea kwa kawaida kuzijadili siasa.
Wapo bila ya shaka Wazanzibari wanaopendelea Muungano uliopo uendelee vivi hivi ulivyo na wasioona kuwa kuna dosari kubwa yoyote katika mahusiano baina ya Tanganyika na Zanzibar isipokuwa ‘kero’ za hapa na pale zinazoweza kuondoshwa kwa mashauriano kati ya pande mbili za Muungano. Watu wenye fikra kama hizi wapo lakini ni wachache Visiwani.
Ukiwadadisi Wazanzibari utang’amua haraka kwamba wengi wao wanahisi ya kuwa kuwapo kwa Muungano kumezidi kuyaathiri vibaya maisha ya Wazanzibari wa kawaida. Ukiwauliza kwa nini watakupa hoja aina kwa aina — pamoja na zile ambazo pengine haziingii akilini. Wanavyofikiri wao ni kwamba matatizo yao ya kisiasa, kiuchumi na ya kijamii yamezidi kuwa mawi kwa nchi yao kuungana na Tanganyika. Kwa upande wa pili, kuna Watanganyika wasemao kwamba nao wamechoka ‘kuibeba’ Zanzibar na ikiwa Wazanzibari wanataka kujitoa kwenye Muungano basi nawatoke watokomee mbali.
Kwa ufupi, hoja kubwa inayotumiwa na Wazanzibari ni kwamba wanahisi ya kuwa nchi yake imemezwa na Tanganyika. Na ilipomezwa ikapokonywa madaraka yake kamili ya kuendesha shughuli zake za kiuchumi, kijamii na za kisiasa. Zanzibar haiwezi kuchukua hatua yoyote ya maana kuhusu mustakbali wake bila ya kupata idhini ya Bara. Hivyo ndivyo wanavyohisi.
Pili, wanatambua kwamba yale yaitwayo ‘Mambo ya Muungano’ ndiyo yanayotumiwa na serikali ya Tanzania (kwa maana ya Bara au Tanganyika) kuikalia kichwani Zanzibar. Kinachozidi kuwaudhi ni kuona kwamba hayo ‘Mambo ya Muungano’ yameongezwa kutoka 11 na kufikia idadi ya 22.
Sasa Wazanzibari wamemaizi kwamba kwa vile wana umoja wa kisiasa na kuna utulivu nchini mwao wana kila haki ya kudai warejeshewe mamlaka yaliyoporwa na serikali ya Muungano. Wanachotaka ni kurejeshwa tena Jamhuri ya Watu wa Zanzibar iliyotoweka mwezi Aprili mwaka 1964 baada ya Muungano kuundwa na Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Sheikh Abeid Amani Karume. Hiyo hatua iliyochukuliwa tarehe 26 Aprili mwaka 1964 na marais hao wa Tanganyika na Zanzibar hii leo inakosolewa sana Zanzibar kwani inaonekana kuwa ni hatua iliyokwenda kinyume na maslahi ya kitaifa ya Zanzibar.
Hizi si hisia za leo na jana. Ni hisia zilizokuwepo tangu siku ya mwanzo ya kuundwa kwa Muungano. Hata akina sisi twenye kupigania nchi za Kiafrika ziungane na ziwe na umoja, tukitetea itikadi ya ujumuiya wa Afrika (pan-Africanism), pia tulikuwa na shaka kubwa. Tukiamini kwamba Muungano uliundwa kwa papara na si kwa muundo ambao ungezishajiisha nchi nyingine barani Afrika ziwe na hamu ya kujiunga nao.
Ingawa juujuu uliweza kutumiwa kuwa ni mfano wa nchi zilizoungana kwa nia ya kuleta umoja wa Afrika, kwa hakika undani wake ulidhihirisha mapema kwamba utakuwa kikwazo cha kuleta umoja uliokuwa ukitetewa na watu kama kina Kwame Nkrumah wa Ghana.
Kwa jumla, wengi wa Wazanzibari wamekuwa wakiupinga Muungano kwa sababu wanahisi ya kuwa haujawaletea manufaa yoyote ya maana kwa upande wa kisiasa, kiuchumi au kijamii. Kadhalika, hata wale wachache wenye kuutetea Muungano wanasema kwamba wanaupinga muundo wake wa sasa.
Hiyo ndiyo halisi ilivyo leo Visiwani. Hali hiyo itazidi kujidhihirisha wakati wananchi watapowasilisha maoni yao kwa Tume ya Katiba katika mchakato wa kutafuta katiba mpya ya Jamhuri ya Muungano. Ndiyo maana hivi sasa Wazanzibari wanaliona zoezi la kuiandika upya Katiba ya Muungano kuwa ni lenye kuwapa fursa ya kuzidai haki zao za kurejeshewa madaraka yao.
Wanavyotaraji ni kwamba patatokea mageuzi makubwa ya kimsingi kuhusu hadhi ya Zanzibar na nafasi yake katika Muungano au nje ya Muungano. Kikubwa wanachodai ni kwamba kama Muungano uwepo basi uwe ni Muungano wa Mkataba na si wa Katiba.
Ingawa ni vigumu kwa sasa kuweza kutabiri jinsi mchakato huo utavyoendelea na nini matokeo yake yatavyokuwa, lakini tukiyakumbuka yaliyojiri kwenye mikutano mbalimbali, kongamano na mihadhara iliyohudhuriwa na umati wa watu tunaona kwamba Wazanzibari wote hao wamekuwa na kauli moja wakiifuata ajenda moja.
Wanachosema ni kwamba wanataka muundo wa sasa wa Muungano ubadilishwe na kwamba Zanzibar na Tanganyika ziungane kwa kutumia mkataba baada ya Zanzibar kuyatwaa tena mamlaka yake ya kuiwezesha kujiamulia mambo yake.
Ni muhali kuweza kuendelea na mchakato wa sasa wa kuijadili na kuichambua Katiba ya Muungano bila ya kuwa na majadiliano ya maana na ya kijituuzima kuhusu muundo wa Muungano. Majadiliano hayo hayaepukiki hasa miongoni mwa Wazanzibari. Hayaepukiki kwa sababu Wazanzibari wamekwishaanza kuuliza swali la kimsingi: mchakato huu utakuwa na maana gani iwapo wananchi watazuiliwa kuujadili Muungano?
Kwanza, tayari suala hilo limo midomoni mwa wananchi kufika hadi ya kuwapandisha jazba. Pili, vijana wa leo, wakike na kiume, wengi wao waliozaliwa baada ya kuundwa Muungano wanasema wanataka kuona mageuzi makubwa yanatokea nchini mwao yatayowawezesha Wazanzibari wajiamulie mambo yao yenyewe.
Wapo pia Wazanzibari wenye msimamo mkali wenye kushikilia kwamba kabla ya mchakato huu wa katiba kuendelea kwanza pangepigwa kura ya maoni Visiwani Zanzibari kuhusu Muungano wenyewe. Wanachotaka ni kwamba Wazanzibari wangeulizwa iwapo wanautaka au hawautaki Muungano na kama wanautaka ni Muungano wa aina gani wautakao.
Kwa maoni ya wengi endapo kura ya maamuzi ya aina hiyo itatayarishwa leo Visiwani na Wazanzibari watakuwa na uhuru kamili wa kuamua basi wengi wao wataukataa Muungano kama ulivyo sasa.
Huu ni mtihani mkubwa kwa serikali zote mbili za Tanzania — ile ya umoja wa kitaifa huko Zanzibar na ya Muungano jijini Dar es Salaam. Panahitajika hekima na si mabavu kuyatathmini maoni ya walio wengi na kutafuta njia za kuwaridhisha.
Chanzo: Raia Mwema

Friday 20 April 2012

Waandamana kutaka kura ya kuamua Muungano

Salma Said, Zanzibar
JESHI la Polisi Zanzibar limewatia mbaroni zaidi ya watu 10 wakiwemo viongozi wa kundi la wanaotaka kuitishwe kura ya maoni kuhusu Muungano, baada ya kukataa kutii amri ya jeshi hilo iliyowataka kuondoka katika viwanja vya Baraza la Wawakilishi jana.

Kundi la watu zaidi ya 40 lilifika katika viwanja hivyo vya Baraza la Wawakilishi huko Chukwani wakitaka kuonana na Spika wa Baraza hilo, Pandu Ameir Kificho.

Spika alimuagiza Katibu wake, Yahya Khamis Hamad kuongea na wananchi hao.
Wakizungumza nje ya viwanja hivyo, wananchi hao walisema lengo lao ni kuonana na Spika Kificho ili kuwasilisha ombi lao la kutaka kupelekwa hoja binafsi ya kuitishwa kura ya maoni ya kutaka au kukataa Muungano.

Katibu wa Baraza hilo alisema sio vibaya wananchi hao kuwasilisha mapendekezo hayo kwa Spika, lakini aliwataka wananchi hao kufuata utaratibu unaokubalika wa majadiliano na siyo kujikusanya katika viwanja hivyo jambo ambalo linatishia usalama.

“Waheshimiwa pengine mmekuja hapa kwa nia njema kabisa lakini kwa utaratibu huu nimelazimika kuja hapa nje na kukuombeni muondoke ili muache shughuli za baraza ziendelee kwa sababu sipendi kuona mkipambana na polisi katika viwanja hivi,” alisema Katibu huyo.

Aliongeza, “Hata Spika alisema kwa utaratibu kama huu hataweza kuwaruhusu kuonana naye lakini kama mtafuata utaratibu mzuri ambao umewekwa na tumeuainisha ndani ya barua zenu basi mnaweza kukutana na kuongea naye."

“Lakini kwa hali kama hii haitawezekana kwa sababu shughuli za Baraza zinaendelea lakini pia wananchi wanashindwa kupita hapa na kufanya shughuli zao kwa kuwa mmefunga njia, waheshimiwa wanataka kuja hapa lakini wanashindwa kutokana na hali hii,” alisema Katibu Hamad.

Mapema, wananchi hao wakiongozwa na Rashid Salum Adiy walifika katika viwanja hivyo kwa wingi wakiwa na mabango yao yenye ujumbe wa kutaka kuitishwa kwa kura ya maoni kuamua mustakabali wa Zanzibar ambapo walitaka kuingia ndani na kuonana na uongozi wa baraza hilo.

Hata hivyo jeshi la polisi lilitoa tahadhari na kuwataka waondoke katika viwanja hivyo na kuelekea nyumbani ili kupisha viongozi wa wajumbe wa Baraza la Wawakilishi kuwasili katika baraza hilo ili waendelee na shughuli za Baraza hilo ambalo jana limeakhirishwa.

Rashid Sulum Adiy ni kiongozi wa kundi hilo la wazanzibari wenye kudai kuitishwa kura ya maoni juu ya mustakabali wa Zanzibar ndani ya Muungano na anataka Baraza la Wawakilishi liitishe kura ya maoni ya kuwauliza wazanzibari iwapo wanautaka Muungano au hawautaki.

Katika barua yao walioiwasilisha kwa Spika Kificho ya Aprili 18 mwaka huu inasema “Sisi ni wananchi 1825 miongoni mwa watu 300,000 sote wazanzibari na ni watu wazima wenye akili timamu kutoka majimbo 50 ya Unguja na Pemba tunakutaka utuwasilishie mbele ya Baraza la Wawakilishi ombi la hoja yetu binafsi ya kuwepo kwa kura ya maoni juu ya suala la Muungano wa Tanzania,” ilisema barua hiyo.

Wakitilia mkazo hoja hiyo katika barua yao walisema baada ya kipindi cha miaka 48 ya Muungano hoja yao hiyo ya kuitisha kura ya maoni ni muhimu sana kwa wazanzibari na vizazi vya baadae.

“Hatukubali kama tutapigwa mabomu, marungu au kukamatwa kwa sababu ya hatari inayotukabili mbele yetu. Kwa hivyo kwa heshima na tunaliomba baraza nalo lishirikiane na sisi kwa kutumiza wajibu wake na kulikubali ombi letu la kuwa na kura ya maoni juu ya Muungano,” ilisema barua hiyo ambayo Mwananchi inayo nakala yake.

Barua hiyo imesema Muungano huo umekosa misingi ya kisheria ya kitaifa na kimataifa na ndio sababu ya kuongezeka kero na kasoro kadhaa, lawama na matatizo mbali mbali yanayoshindikana kutatuliwa kwa pande mbili hizo.

Walisema kwa kuwa Muungano huo unahusu nchi mbili tofauti, za Zanzibar na Tanganyika ni vizuri wananchi wakapewa nafasi ya kuhojiwa iwapo wanautaka uendelee au uvunjike kwani maamuzi ya wananchi ndio yanayotegemea kuendeleza usalama na utulivu uliopo.

Hivi karibuni Rais Kikwete aliteua tume ya kukusanya maoni juu ya Katiba mpya na tayari wajumbe wa tume hiyo wameshaapishwa na wataanza kazi rasmi mwanzoni mwa mwezi ujao lakini malalamiko juu ya suala hilo yamekuwa yakijichomoza kila siku hapa Zanzibar.

Makundi mbali mbali yamekuwa yakifanya mikutano ya wazi kuelezea suala hilo huku idadi kuwa ya wazanzibari wakiunga mkono hoja ya kuwepo kura ya maoni kwanza kabla ya tume kuanza kufanya kazi zake.Kamishna wa polisi Ali alisema watu hao watafikishwa mahakamani Jumatatu kwa kosa la kusababisha uvunjifu wa amani.

Alisema ingawa sheria inawapa watu haki ya kudai wanachotaka, bado watu wana wajibu wa kufuata taratibu ili kulinda haki za wengine na badala ya kujichukulia sheria mkononi.
Chanzo: Mwananchi

Thursday 19 April 2012

Wawakilishi Zanzibar wailipua familia ya Karume

Salma Said, Zanzibar
KAMATI Teule ya Baraza la Wawakilishi imegundua ufisadi wa kutisha katika maeneo tofauti ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), huku familia ya Rais mstaafu wa visiwa hivyo, Aman Abeid Karume ikitajwa kukiuka sheria kwenye umiliki wa ardhi.

Wakati familia hiyo ya Rais mstaafu Karume ikituhumiwa kukiuka sheria za ardhi, mfanyabiashara maarufu nchini Said Salim Bakharessa ambaye naye ametajwa kujipatia kiwanja cha Serikali kwa bei ndogo, alijitetea mbele ya kamati na kumlipua waziri aliyekuwa na dhamana ya ardhi akisema, "Mimi nilipigiwa simu na waziri akiniambia kuna kiwanja kinauzwa."
Akisoma ripoti hiyo Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Omar Ali Shehe, alitaja maeneo ambayo yalibainika kuwa na ukiukaji mkubwa wa sheria ambayo mbali na sekta ya ardhi ni ajira katika utumishi Serikali, mikataba katika maeneo nyeti na ukiukaji wa sheria za ununuzi.
Akizungumzia uhalali wa mikataba ya nyumba ya Serikali iliyopo Kiponda inayodaiwa kwamba alipewa mwananchi na baadae kuiuza kwa mtu mwingine, Shehe alisema Kamati imebaini kwamba, mikataba yote ya mauziano iliyofungwa baina ya Serikali na Juma Ali Kidawa na baina yake na Amina Aman Abeid Karume, ni batili na ya udanganyifu.
Shehe alisema kumekuwapo uvamizi wa fukwe na uharibifu wa mazingira kwenye hoteli inayopakana na Chuo cha Maendeleo ya Utalii Zanzibar, Maruhubi, kwenye Hoteli ya Zanzibar Ocean View, Kilimani-Zanzibar na Hoteli ya Misali iliyopo Wesha, Chake Chake-Pemba.
Aliongeza kwamba Kamati imejiridhisha kwamba Ramadhan Abdallah Songa na Mama Fatma Karume walishiriki katika udanganyifu wa mkataba wa mauziano uliofungwa baina ya Serikali na Kidawa.
"Aidha, hati ya matumizi ya ardhi aliyopewa Karume na Mansour Yussuf Himid, (Akiwa Waziri wa Ujenzi, Nishati na Ardhi), imekiuka taratibu za kisheria na kiutawala), " alisema mwenyekiti huyo.

Shehe alisema Kamati inapendekeza nyumba hiyo ambayo sasa imeshajengwa Hoteli ya Amina Aman Karume, hati zote za umiliki wake, zifutwe na apatiwe tena hati ya umiliki wa ardhi husika na baadae atakiwe kumsaidia Kidawa kwa kiwango cha fedha kisichopungua Sh20 milioni, kujinasua na maisha.

"Hatua za kisheria zichukuliwe dhidi ya wananchi wote waliohusika katika udanganyifu uliojitokeza katika upatikanaji wa mikataba ya mauziano kutoka katika mamlaka ya Serikali na kumuuzia Kidawa na mauziano baina ya Kidawa na Amina Aman Abeid Karume,"alisema Shehe.

Shehe alisema pia kwamba imegundulika Machano Othman Said akiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Miundombinu na Mawasiliano) katika Serikali ya awamu hiyo ya sita, anamiliki asilimia 10 ya hisa katika mradi wa Hoteli ya Misali Sunset Beach, iliyopo Wesha Pemba.

Alisema kwa nafasi yake wakati huo akiwa waziri, Machano (ambaye kwa sasa ni Waziri asiye na Wizara Maalumu), alitumia nafasi yake kuisaidia kuendeshwa hoteli hiyo bila kibali cha mazingira wala leseni ya utalii kutoka Pemba, ambako ndiko kwenye mradi huo hivyo awajibishwe.

Katika ripoti hiyo, Shehe alibainisha kuwa uchunguzi uliofanyika kuhusu uhaulishwaji wa kiwanja cha Wizara ya Miundombinu na Mawasililiano ambacho kipo kwenye eneo ilipokuwepo Karakana na wizara hiyo, eneo la Mtoni, Mjini, Zanzibar, umeonyesha kuna ukiukwaji mkubwa sheria na taratibu za uuzaji wa mali za Serikali.

Shehe, alisema wamejiridhisha kwamba wizara hiyo ya Miundombinu na Mawasiliano haikufuata taratibu za uuzaji wa kiwanja hicho ilichokuwa inakimiliki na kuamua kukiuza kwa kampuni binafsi bila ya kufuata taratibu za kiutawala na taratibu za kisheria.

"Hali hiyo imepelekea wasi wasi mkubwa wa kuwepo kwa harufu ya ubinafsi na harufu ya rushwa, zaidi ukizingatia thamani ya kiwanja hicho kuwa ni sawa na Sh200 milioni bei ambayo ni ndogo kwa mujibu wa bei ya soko na kwa kuzingatia ukubwa wa kiwanja chenyewe na eneo kilipo,"alisema Shehe.

Alisema kulikuwa na matumizi mabaya ya madaraka ya Ofisi ya Rais kwani walipokuwa wakiangalia namna gani ulitolewa uamuzi mzito wa kuuza kiwanja hicho cha Serikali, ilibainika iliruhusiwa na Ofisi ya Rais.

"Katika utafiti wetu, tuligundua kuwa, maombi ya ruhusa ya kuuzwa kwa kiwanja hicho, yametoka kwa Katibu wa Rais, Haroub S. Mussa, ambaye aliandika barua, tuliyoifanya kielelezo Namba. 9 cha Ripoti yetu," alifafanua.

Shehe alisema Haroub hana mamlaka ya kuruhusu uuzwaji wa kiwanja, wala kusimama katika nafasi ya kupeleka uamuzi wa Rais kwa mtu mwengine yeyote kwani kazi hiyo kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar, kifungu cha 49(1), inafanywa na Katibu Mkuu Kiongozi.

Kutokana na hali hiyo, kamati imependekeza aliyekuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mawasiliano na Uchukuzi (2008-2010, Machano) na watendaji wote waliohusika katika kuingia mikataba na Kampuni ya Coastal Fast Ferries Ltd, wawajibishwe kwa misingi ya sheria.

Kuhusu kuchunguza suala zima la Uwanja wa Ndege wa Zanzibar, alisema ulipaji wa fidia kwa watu ambao mali zao zimeathirika kutokana na ujenzi wa uzio wa uwanja huo umegubikwa na utata.

"Matatizo ya ununuzi wa jenereta, mikataba ya ukodishwaji wa sehemu za biashara kwenye eneo la uwanja na utaratibu wa ajira na utoaji wa huduma mbali mbali kwenye maeneo ya uwanja na Wizara ya Miundombinu na Mawasiliano kwa ujumla, haukuzingatia sheria," alisema Shehe.

Alisema kamati imegundua na kujiridhisha kwamba, kumefanyika uzembe wa makusudi na Wizara zote mbili zimehusika katika uzembe huo yaani Ofisi ya Rais, Fedha, Uchumi na Mipango ya Maendeleo na Wizara ya Miundombinu na Mawasiliano na matokeo yake zaidi ya Sh300 milioni, zinaelekea kupotea huku jenereta lililonunuliwa kwa fedha zote hizo, limeshindwa kujaribiwa kwa kipindi chote cha muda wake wa majaribio (warrant period).

"Aidha, kitendo cha jenereta kukaa bila ya matumizi ya muda mrefu pia ni sehemu ya uharibifu wake. Kwa mantiki hiyo, Kamati inafahamu kwamba, jenereta hilo limetelekezwa," alisema.

Alisema kamati inapendekeza hatua za kinidhamu zichukuliwe kwa watendaji wote waliohusika na uzembe wa ununuzi wa jenereta hilo, huku msisitizo ukiwekwa kwa makatibu wakuu wa Ofisi ya Rais, Fedha, Uchumi na Mipango ya Maendeleo na Wizara ya Miundombinu na Mawasiliano; Mkurugenzi na Meneja wa Mamlaka ya Uwanja wa Ndege.

"Kuhusu mikataba, kamati inapendekeza mikataba yote inayohusiana na ukodishwaji wa biashara mbali mbali katika eneo la uwanja wa ndege ipitiwe upya ili iendane na mabadiliko ya biashara na msisitizo ukiwekwa katika gharama za kodi husika,"alisema.

Katika utoaji ajira kwa upendeleo, Shehe alieleza kuwa Waziri wa Wizara Miundombinu na Mawasiliano, Katibu Mkuu na Naibu Katibu Mkuu, wamekuwa wakiwaajiri watoto, ndugu ama jamaa zao, huku wakiwapa fursa nyingi za upendeleo kinyume na utaratibu.

"Spika, naomba kwa makusudi wajumbe wako wapate taarifa hizi katika mfanyakazi, Aisha Msanif Haji, mtoto wa Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Miundombinu na Mawasiliano, ambaye ameajiriwa na bado akiwa katika kipindi cha majaribio, tayari amepewa ruhusa ya kusoma, huku akiwa anaendelea kupokea mshahara kama kawaida."

Alisema imethibitika kwamba, kuna mfanyakazi analipwa mshahara wa ngazi ya mtaalamu (msomi wa shahada) wakati bado hajafikia elimu hiyo.
"Huyu si mwengine isipokuwa mtoto wa Katibu Mkuu wa Wizara ya Miundombinu na Mawasiliano,"alisema.
Shehe alisema kutokana na hali hiyo, Kamati imependekeza viongozi na watendaji wakuu wa wizara zote mbili (Wizara ya Miundombinu na Mawasiliano na Ofisi ya Rais, Utumishi wa Umma na Utawala Bora) waliohusika na kadhia hiyo wawajibishwe kisheria.
Pia uajiri wa wafanyakazi wote ambao kamati imeona hawana sifa za kuajiriwa, ufanyike upya kwa kufuata muongozo wa sheria zilizopo.
Chanzo: Mwananchi

Shein: Zanzibar GNU sets precedent for other nations



Zanzibar President Dr Ali Mohamed Shein has said the government of national unit (GNU) has succeeded in sustaining peace and tranquility since its formation in November 2010.
Addressing a public rally after laying the foundation stone at the Bopwe East branch, in Pemba Islana where he pledged to contribute 5m/- out of the 8.7m/- needed to complete the branch, said the GNU has set a precedent for other nations to follow.
He said the cabinet has been working in unity putting national interests at fore. "My ministers and I work together; this is in spite the fact that it is formed by members from CCM and CUF, what matters to us is national interests in serving the people," said Dr Shein.
He said under the GNU, he will continue leading the country respecting the constitution of the United Republic of Tanzania and that of Zanzibar. "We shouldn’t mix party politics with government affairs,” stressed Dr Shein.
He said that the GNU has provided to be a role model for other nations to follow, as many ambassadors; including representatives of UN organisations have been flocking to Zanzibar to learn how it worked.
"The GNU is here to serve the people, the goal being to see that their lives improve. I serve for no other purpose than the wellbeing of the people," stressed Dr Shein.
The GNU was formed by CCM, which won many seats in the presidential elections in 2010 and CUF, which by far scooped more seats compared to other opposition parties.
Source: The Guadian

Wednesday 18 April 2012

Wanunuzi wa ndege ya Rais mbaroni

Viongozi wawili mashuhuri nchini Cameroon wamekamatwa kwa kuhusika na ununuzi wa ndege mbovu ya rais.
Wawili hao ni pamoja na Waziri Mkuu wa zamani Ephraim Inoni na aliyekua Waziri wa mambo ya ndani Marafa Hamidou Yaya.
Wanasiasa hao waliongoza ujumbe Marekani kununua ndege ya rais kwa jina Albatross, kwa gharama ya dola milioni 31. Rais Paul Biya, Mkewe Chantal na wanawe walikuwa kwenye ndege hiyo wakati ilipopata hitilafu ya mitambo, na kumlazimu rubani kutua ghafla.
Wakati huo Bw Yaya alikuwa katibu wa afisi ya Rais huku Inoni akiwa naibu wake. Baadaye Inoni aliteuliwa Waziri Mkuu na Yaya akapalekwa Wizara yenye ushawishi ya mambo ya ndani. Wadadisi wamesema Yaya alionekana kuwa mrithi wa kiti cha urais kabla ya kuachishwa kazi mwaka 2011.
Punde baada ya habari kutokea kukamatwa kwa viongozi hao, raia wengi walijitokeza kushuhudia wawili hao wakisafirishwa katika jela kuu la nchi.
Wengine ambao wanashikiliwa kufuatia sakata hiyo ni pamoja na Aliyekuwa Waziri,Jean-Marie Atangana Mebara, Balozi wa Zamani nchini Marekani,Jerome Mendouga na aliyekuwa mkuu wa shirika la ndege nchini Cameroon Yves Michel Fotso.
Chanzo: BBC

Sunday 15 April 2012

Slaa amgomea JK

KATIBU Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk. Willibrod Slaa, ameeleza kushtushwa na kauli ya Rais Jakaya Kikwete inayolenga kuzuia wananchi kujadili kuhusu Muungano wakati wa mchakato wa marekebisho ya Katiba.

Dk. Slaa aliye katika ziara ya kichama kukagua uhai wa chama hicho ikiwa ni pamoja na kukijenga, alitoa dukuduku lake hilo jana wakati akihutubia mkutano mkubwa wa hadhara uliofanyika katika viwanja vya Shycom, mjini Shinyanga.

Katibu mkuu huyo wa CHADEMA alitoa kauli hiyo ikiwa ni siku moja tu tangu Rais Kikwete alipowaapisha wajumbe 30 wa Tume ya kukusanya maoni ya Katiba mpya inayoongozwa na mwanasheria na mwanasiasa anayeheshimika, Jaji Joseph Warioba.

Wakati akizindua tume hiyo juzi, pamoja na mambo mengine, Rais Kikwete alisema tume hiyo katika kazi yake haitahusika katika kuhoji kuhusu kuwapo ama kutokuwapo kwa muungano.

Kwa upande wake Dk. Slaa aliwataka Watanzania kuachana na maneno ya watawala na kutobweteka baada ya kuundwa kwa tume hiyo ya Jaji Warioba.

“Jamani Watanzania wenzangu wa Shinyanga, naomba tuzungumze kidogo hili la Katiba mpya, kwanza nawaomba msibweteke eti kwa sababu tume imeundwa, kuundwa tume hakuleti katiba mpya na bora. Pia tunataka Kikwete ajue kuwa Watanzania hawatengenezi katiba ya Kikwete wala ya CCM. Wanataka Katiba mpya na bora ya kwao.

“Nami namuomba ni bora akajitahidi kujiepusha na matamko ya ajabu, maana anaendelea kutupatia ajenda. Anasema suala la muungano lisijadiliwe wakati wa mchakato wa utoaji maoni. Hapa anataka kutuma ujumbe gani…” alisema Dk. Slaa na kushangiliwa.

Akiuchambua muungano, Dk. Slaa alisema ni haki ya Watanzania kwa maana ya wale wa Zanzibar na wa Bara kujadili muungano wanaoutaka kwani kufanya hivyo hakuna nia ya kuuvunja.

“Sisi CHADEMA tunasimamia nini? Tunataka Watanzania wajadili wanataka muungano wa aina gani, tunataka Zanzibar ipate haki zake kama ilivyokuwa mwaka 1964.

“Hapa hoja si muungano uwepo ama usiwepo, hoja ni aina gani ya muungano wa kisiasa Watanzania wanautaka. Tunaamini kuwa hakuna mwanasiasa mwenye akili timamu anaweza kuhubiri kuvunja muungano.

“Mwanasiasa anayezungumzia kuvunja muungano huyo ni mwendawazimu, maana muungano wa kweli wa Watanzania uko kwenye damu zao. Lakini katika suala la kiutawala wananchi waachwe waamue wanataka aina gani, hii ndiyo hoja hapa,” alisema Dk. Slaa.

Akifafanua, Dk. Slaa alisema wanazo taarifa kwamba tayari CCM kupitia katika Halmashauri Kuu yao ya Taifa wameshafikia hatua ya kuwatumia makada wao, wakiwamo viongozi wa kiserikali kama wakuu wa mikoa na wilaya katika kuhakikisha yale ambayo chama hicho tawala kinayataka, yanaingizwa katika Katiba mpya.

“Napenda kumwambia haya huku akijua kuwa, mkononi kwangu au ofisini kwetu tayari tunao uamuzi wa Halmashauri Kuu ya chama chao, ambayo imewaagiza viongozi ambao ni makada wao, kuhakikisha masuala ambayo chama hicho kinataka yanaingia katika Katiba mpya, hii ni hatari,” alisema Dk. Slaa.

Akifafanua, alisema chama hicho kitaendelea kuwa mstari wa mbele kuwaongoza Watanzania waandike Katiba mpya inayozingatia haki za msingi kama vile masuala ya ardhi, huku pia akisisitiza kuwa suala la mamlaka ya rais linapaswa kuangaliwa upya na kurekebisha.

Aliongeza kuwa, moja ya mwarobaini wa kuachana na wateule wengi wa rais ni kuwa na serikali za majimbo ambako viongozi wake sharti wachaguliwe na watu badala ya sasa wananchi kutawaliwa na mkuu wa mkoa au wilaya wasiyemjua

Friday 13 April 2012

Wazanzibari wa Tume watashikana ama wataangushana?

Barazani kwa Ahmed Rajab
 
WATANZANIA sasa wanatambua kwamba mchakato wa Katiba umeanza kwa dhati. Pia sasa wanajua nani yumo na nani hayumo kwenye Tume ya Kukusanya na Kuratibu Maoni ya Mabadiliko ya Katiba.
Tume hiyo, ambayo kwa mkato inaitwa Tume ya Katiba, ni chombo chenye umuhimu mkubwa katika mchakato mzima wa kutunga Katiba mpya na kinahitaji kuwa na uadilifu wa hali ya juu wa kuweza kuwakilisha maoni halisi ya wananchi kuhusu Katiba waitakayo na hivyo kuhusu aina ya Muungano wautakao.
Majina 30 ya wajumbe wa Tume hiyo yalitangazwa Ijumaa iliyopita na Rais Jakaya Kikwete pamoja na ya mwenyekiti wa tume na makamu wake.
Wajumbe hao (15 kutoka Bara na 15 kutoka Visiwani) wataapishwa baadaye mwezi huu kama inavyotakiwa na Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ya Mwaka 2011 ambayo ndiyo iliyosababisha kuundwa kwa Tume hiyo ya Katiba. Mwenyekiti wao, Jaji Joseph Warioba ametoka Bara na Makamu wake Jaji Mkuu mstaafu Augostino Ramadhani ni Mzanzibari.
Kuteuliwa kwa Tume hiyo ni hatua ya mwanzo katika mchakato uliopangwa uendelee kwa muda wa miaka miwili na kufikia kikomo Aprili mwaka 2014.
Inatarajiwa kwamba kufikia hapo, Jamhuri ya Muungano ya Tanzania itakuwa imepata Katiba mpya itayotungwa na Bunge la Katiba na kupigiwa kura ya maoni na wananchi.
Yote hayo yatatendeka kwa mujibu wa Sheria Kuhusu Mchakato wa Mabadiliko ya Katiba iliyopitishwa na Bunge hivi karibuni. Sheria hiyo ndiyo iliyomwezesha Rais kuunda hiyo Tume ya Kukusanya na Kuratibu Maoni Kuhusu Katiba Mpya.
Sheria hiyo ina vifungu vingi vilivyo muhimu sana kama kile chenye kutaka pawepo na idadi sawa ya wajumbe kutoka Zanzibar na kutoka Bara katika Tume ya Katiba. Hilo limetekelezwa.
Labda kifungu kilicho muhimu zaidi ni kile chenye kusisitiza kwamba mchakato huo uwe unaongozwa na kuamuliwa na wananchi. Ndiyo maana pakawa na haja ya kupigwa kura mbili tofauti za maoni — moja kwa upande wa Bara na nyingine kwa upande wa Zanzibar.
Zoezi hilo la kura ya maoni lina umuhimu wa aina yake — pingine kama wa kufa na kupona — kwa Zanzibar. Lakini hata kabla ya Wazanzibari kupiga kura hiyo ya maoni juu ya iwapo wanaikubali au wanaikataa Katiba itayopendekezwa Tume ya Katiba itakuwa na jukumu la kukusanya maoni ya Wazanzibari katika kila shehia ya Unguja na Pemba. Hapo Tume itakuwa na kazi ya kweli.
Kwa mara ya mwanzo Wazanzibari watapata fursa ya kutoa maoni yao bila ya woga wowote na bila ya vikwazo vyovyote kuhusu mustakbali wa nchi yao na namna wanavyotaka kujipatia malengo yao ya kitaifa.
Kwa vile mchakato huo umeanza, ni muhimu kukumbushana kwamba hili si jaribio la kwanza la kutunga Katiba mpya ya Tanzania. Kabla ya mchakato huu wa sasa kulikuwa na Tume za Nyalali na Kisanga zilizotoa mapendekezo ya kimsingi kuhusu Katiba mpya ya Tanzania. Mapendekezo hayo lakini yalipingwa na kutupiliwa mbali na Serikali ya Muungano.
Miongoni mwa mapendekezo ya Tume ya Nyalali lile la kuwa na mfumo mpya wa vyama vingi vya kisiasa lilikubaliwa lakini mapendekezo yake kuhusu mageuzi ya kimsingi ya kisheria na kikatiba yalikataliwa ingawa yalikuwa muhimu ili mfumo wa kidemokrasia uweze kumea vizuri katika Jamhuri ya Muungano ya Tanzania.
Ni taabu kutabiri matokeo ya huu mchakato wa sasa yatakuwaje. Ninasema hivi kwa sababu kwa upande wa Zanzibar kumetokea mageuzi makubwa ya kifikra miongoni mwa wananchi kuhusu Muungano wa Visiwa hivyo na Tanganyika. Na wanapoyajadili masuala yanayohusika na Muungano utawakuta kuwa hawana tena woga wa kudhaniwa kuwa ni mahaini.
Natuombe salama kwa sababu jinsi Wazanzibari wanavyotoa hoja za kuunga mkono maoni yao sitostaajabu endapo mchakato huu utasimamishwa kabla ya wakati wake pale wajumbe wa Kamati ya Tume watapoyasikia rasmi maoni hayo.
Jambo jingine lililotokea huko Visiwani hivi karibuni ni Wazanzibari wengi vya vyama na itikadi tofauti za kisiasa kuwa na sauti moja kuhusu ile wanayoiita Ajenda ya Zanzibar. Tunachosubiri kuona ni iwapo wajumbe 15 wenye kuiwakilisha Zanzibar katika Tume ya Katiba nao wataibuka kuwa na sauti moja na msimamo mmoja wenye kuyawakilisha matakwa halisi ya Wazanzibari wenzao au la.
Ikiwa watakuwa na msimamo huo patakuwa salama. Lakini ikiwa wataonekana kuwa kama nyumba iliyogawika kama hali ya mambo ilivyokuwa katika tume zilizopita, ikiwa watakuwa wanazozana wenyewe kwa wenyewe na kupingana kwa misingi ya kichama na kupuuza matakwa ya Wazanzibari basi wenzao wa Visiwani hawatowasamehe wala hawatokuwa na imani nao.
Hivi sasa takriban kila wiki kunafanywa mikutano na mihadhara mbalimbali katika sehemu tofauti za Zanzibar ambapo Wazanzibari wanakusanyika bila ya kujali mielekeo yao ya kisiasa kuutafakari mustakbali wa Zanzibar ndani na nje ya Muungano wake na Tanganyika.
Kilichojitokeza ni kwamba mikutano hiyo inaandaliwa na kudhaminiwa na jumuiya zisizo za kisiasa. Kwa hakika, vyama vikuu vya kisiasa huko Zanzibar vimekaa kimya, havisemi lolote kuhusu suala hili. Sababu zilizovifanya vyama hivyo visithubutu kufungua midomo yao zinaeleweka. Hiyo ni kheri pia kwani wananchi wa Visiwani wamepata uwanja wa kuyasema yaliyo kwenye nyoyo zao bila ya kufungika kwa maagizo au misimamo rasmi ya vyama hivyo.
Ninafikiri labda sababu iliyovifanya vyama vya CCM na CUF vikae kimya ni kwamba mapendekezo yao rasmi kama yalivyo kwenye ilani zao yamepitwa na wakati na hayakubaliwi na idadi kubwa ya Wazanzibari wenye kuamini kwamba hayatoweza kulitatua tatizo lao la kimsingi.
Pendekezo rasmi la CCM/Zanzibar ni la kuendelea na mfumo uliopo wa serikali mbili (ya Zanzibar na ya Muungano) na kutia virakapale palipochanika au kufumka. Lile la CUF ni la kutaka pawepo serikali tatu (ya Zanzibar, ya Tanganyika na ya Muungano).
Ukizungumza na Wazanzibari na ukisoma wanayoyaandika katika mitandao yao utaona kwamba wengi wao, bila ya kujali ni wafuasi wa chama gani, wanataka nchi yao iwe na mamlaka kamili ya kidola. Wanataka iwe na mamlaka yatayoiwezesha nchi hiyo iendeshe shughuli zake za ndani na za nje. Muhimu kushinda yote wanataka iwe na serikali yenye uwezo kamili wa kusimamia mambo yake ya kiuchumi, ya kijamii na ya kisiasa. Tukitaka tusitake hii ndio hali halisi ilivyo Zanzibar hii leo.
Ikiwa vile vyama viwili vikuu vya kisiasa huko Zanzibar pamoja na tabaka zima la wanasiasa wa huko hawatoona umuhimu wa kuiangalia upya misimamo yao kuhusu Muungano basi nao pia watakuwa wamepitwa na wakati na hawatokuwa na maana yoyote kwa nchi yao.
Lazima watambue kwamba kuna mambo mawili makuu yenye kuwafanya Wazanzibari wawe kila mara wanakuna vichwa vyao. Nayo ni namna ya kujipatia tonge na suala la Muungano. Ndiyo maana tunaona kwamba wananchi wa kawaida wa Zanzibar wamewapiku viongozi wao wa kisiasa, kutoka vyama vyote. Wananchi wako katika safu za mbele kabisa katika kudai haki zao na ndiyo maana pia tunaona kwamba ni asasi zisizo za kiserikali pamoja na vikundi vingine ndivyo vilivyo mbele katika kuuongoza mjadala na kuelimishana kuhusu Katiba mpya.
Wazanzibari wanajua walitakalo. Siku hizi hawakubali tena kubabaishwa au kutishwa na yeyote yule waridhie wasilolitaka.
Kadhalika, ni dhahiri kwamba leo Wazanzibari wana umoja wasiokuwa nao kwa muda mrefu sana. Wameazimia kwamba vizazi vyao vijavyo viwe na maisha bora kuliko waliyokuwa nayo wao. Kwa hilo tu pana haja kubwa ya viongozi wa Zanzibar — wa CCM na wa CUF — wawe wanashirikiana na kufanya kazi pamoja ili wawe na msimamo ambao utayawakilisha kikweli matakwa halisi ya wananchi wenzao. Wakifanya hivyo watakuwa wanalipigania lengo la kitaifa la Wazanzibari.
Vivyo hivyo wale wajumbe 15 Wakizanzibari katika Tume ya Katiba wanawajibika kushirikiana na kuwa kitu kimoja katika kuyatetea maslahi ya Zanzibar. Lazima waiweke mbele Ajenda ya Zanzibar na wasiyumbishwe na ajenda za vyama au zao wao wenyewe binafsi au tamaa ya kunufaika wao.
Wajumbe hao wametwikwa jukumu kubwa. Wasipoitumia vyema fursa waliyoipata ya kuiwakilisha vilivyo nchi yao basi watajikuta wanalaaniwa si na wananchi wenzao tu bali historia nayo daima itakuwa ikiwalaani.

Friday 6 April 2012

Rais Kikwete ateuwa tume ya katiba


UONGOZI WA JUU




1.


Mhe. Jaji Joseph Sinde WARIOBA


- Mwenyekiti







2.

Mhe. Jaji Mkuu Mstaafu, Augustino
RAMADHANI

- Makamu Mwenyekiti







WAJUMBE KUTOKA TANGANYIKA




1.


Prof. Mwesiga L. BAREGU









2.

Nd. Riziki Shahari MNGWALI









3.

Dr. Edmund Adrian Sengodo MVUNGI









4.

Nd. Richard Shadrack LYIMO









5.

Nd. John J. NKOLO









6.

Alhaj Said EL- MAAMRY









7.

Nd. Jesca Sydney MKUCHU









8.

Prof. Palamagamba J. KABUDI









9.

Nd. Humphrey POLEPOLE









10.

Nd. Yahya MSULWA









11.

Nd. Esther P. MKWIZU









12.

Nd. Maria Malingumu KASHONDA









13.

Mhe. Al-Shaymaa J. KWEGYIR (Mb)









14.

Nd. Mwantumu Jasmine MALALE









15.

Nd. Joseph BUTIKU









WAJUMBE KUTOKA ZANZIBAR



1.

Dkt. Salim Ahmed SALIM









2.

Nd. Fatma Said ALI









3.

Nd. Omar Sheha MUSSA









4.

Mhe. Raya Suleiman HAMAD









5.

Nd. Awadh Ali SAID









6.

Nd. Ussi Khamis HAJI









7.

Nd. Salma MAOULIDI









8.

Nd. Nassor Khamis MOHAMMED









9.

Nd. Simai Mohamed SAID









10.

Nd. Muhammed Yussuf MSHAMBA









11.

Nd. Kibibi Mwinyi HASSAN









12.

Nd. Suleiman Omar ALI









13.

Nd. Salama Kombo AHMED









14.

Nd. Abubakar Mohammed ALI









15.

Nd. Ally Abdullah Ally SALEH









UONGOZI WA SEKRETARIETI



1.

Nd. Assaa Ahmad RASHID

- Katibu







2.

Nd. Casmir Sumba KYUKI

- Naibu Katibu