Saturday 27 October 2012

Safu mbili zinazoihujumu serikali ya ubia Zanzibar

NOVEMBA 5 Wazanzibari wataadhimisha kutimu miaka miwili tangu iundwe Serikali ya Umoja wa Kitaifa. Kabla ya hapo Wazanzibari walikuwa wamegawanyika vibaya sana. Hakuna asiyetambua hatari iliyokuwepo siku hizo. Walikuwa haweshi kuzozana kisiasa. Athari ya mzozano wao ni madhara makubwa yaliyotokea katika historia ya karibuni ya nchi yao.
Kwa hakika, mzozano huo si wa jana wala juzi. Ulianza kuchomoza mwaka 1957 pale siasa zilipokuwa zinachacha na watawala wa kikoloni wa Kingereza walipoanzisha mfumo wa siasa za vyama vingi.
Mikwaruzano na mifarakano ya kisiasa iliendelea na kusababisha Mapinduzi ya mwaka 1964. Baada ya Mapinduzi hayo haikuchukua muda Zanzibar ikapoteza mamlaka yake kamili ilipoungana na Tanganyika mwezi wa Aprili mwaka huo wa 1964.
Wakati huo Mapinduzi yalikuwa ya moto lakini yalikuwa bado machanga na hayakutimia hata umri wa Siku Mia Moja. Ndiyo maana kuna wenye kuhoji kwamba Mapinduzi hayo yalinyimwa fursa ya kujiimarisha na kujizatiti ili yaweze kuyatanzua matatizo ya muda mrefu ya kisiasa, kiuchumi na kijamii yaliyokuwa yakiwakabili Wazanzibari.
Moja ya mambo yenye kusikitisha katika historia ya karibuni ya Zanzibar ni kwamba Mapinduzi ya nchi hiyo, ambayo katika siku zake za awali yalitangaza kanuni za kupigiwa mfano za kutaka kuleta usawa na maendeleo kwa Wazanzibari wote, yaliachiwa yapoteze dira na yapotoke.
Serikali ya Muungano, kwa upande wake, iliyakodolea macho tu Mapinduzi na vitimbi vya upotovu vya viongozi wake. Wakati wote huo Serikali ya Muungano haikuchukua hatua yoyote na wala haikuonyesha dalili ya kutaka kufanya chochote kile kuizuia hali ya uonevu na ya utawala mbovu isizidi kuwa mbaya.
Matokeo yake ni kwamba Mapinduzi yalikwenda kombo na yakapotea njia. Hii ndiyo sababu kwa nini hadi hii leo, katika kipindi cha takriban nusu karne, malengo Mapinduzi ya kuleta usawa na maendeleo hayakuweza kutimizwa.
Ni jambo lililo wazi kwamba Wazanzibari wamepata hasara kubwa kutokana na mgawanyiko na mfarakano wao. Ubishani na uhasama wa kisiasa uliendelea kwa muda mrefu mno na kama nilivyokwishagusia, uliidhuru sana Zanzibar. Kwa kweli hali hiyo ya kutokuwako suluhu ya kisiasa ndiyo iliyochangia pakubwa kuifanya Zanzibar iwe kama ilivyo hii leo.
Hivi sasa imekuwa ni nchi yenye uchumi uliodidimia kwa vile uchumi huo ulitupwa kwa miaka na mikaka bila ya kushughulikiwa ipasavyo na bila ya kusimamiwa inavyostahiki. Miaka yote hiyo watawala walipuuza kuwa na mikakati endelevu ya kuupanga na kuukuza uchumi. Matokeo yake yakawa kuanguka kwa viwango vya utendaji kazi katika nyanja zote za utawala na uendeshaji wa sera za kijamii.
Tunapoiangalia hali ya zamani ndipo tunapoweza kuiona hasa thamani na tija ya kuwa na Serikali ya Umoja wa Kitaifa katika nchi iliyokuwa imegawika kama Zanzibar. Serikali aina hiyo ni ya mfumo wa kuwa na ubia katika madaraka ya serikali na hivyo kumfanya kila Mzanzibari ahisi kwamba anashirikishwa katika serikali na anakuwa mtiifu kwa serikali hiyo.
Hali kama hii iliyoko sasa Visiwani haijapatapo kuwako kabla ya kuundwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa.
Hakujawahi kuwako utiifu kama huo kwa serikali kabla ya kuundwa kwa hiyo serikali ya ubia kwani tangu siasa za vyama vingi zirejee Visiwani, takriban nusu ya wakazi wa Zanzibar wakinyanyaswa, wakibaguliwa na wakitengwa na serikali au wakionekana kuwa ni ‘maadui wa taifa’ ambao lazima wadhibitiwe na wagandamizwe.
Hali ya mambo hii leo Zanzibar ni tofauti sana na ilivyokuwa zamani. Hii leo Zanzibar ina serikali iliyoviingiza ndani yake vyama vyote vikuu nchini humo yaani Chama cha Mapinduzi (CCM) na Chama cha Wananchi (CUF). Matokeo yake ni kupatikana umoja miongoni mwa Wazanzibari na pia utulivu wa hali ya kisiasa. Yote hayo mawili ni mambo adhimu na yanabidi yaendelezwe, yakuzwe na yaimarishwe ili Wazanzibari waweze kutimiza malengo yao.
Kuna jambo moja ambalo ni muhimu kukumbuka. Nalo ni kwamba hii Serikali ya Umoja wa Kitaifa isingaliweza kuundwa bila ya kupatikana maridhiano yaliyoondosha uhasama baina ya vyama vikuu vya kisiasa Visiwani. Kwa hili, ile Kamati ya Maridhiano ya Wazanzibari sita iliyolisuka suluhisho mwanana la Kizanzibari kwa matatizo ya Kizanzibari inastahiki kupewa sifa maalumu katika historia ya karibuni ya Zanzibar.
Maridhiano haya hayakuwa matokeo ya kauli ya asilimia 65 ya Wazanzibari waliyoyaridhia katika kura ya maoni lakini ndani ya CCM yalipata ‘baraka’, kama isemwavyo siku hizi, za Mwenyekiti wake Jakaya Kikwete.
Bila ya shaka maridhiano hayakuuyayusha kabisa kabisa uhasama wa kisiasa uliokuweko. Kama tukitaraji hayo yatokee katika kipindi kifupi kama hiki basi tukitaraji miujiza. Mabaki ya uhasama huo yangaliko. Lakini juu ya kuzuka kwa mikwaruzano ya kisiasa ya hapa na pale, kwa jumla Wazanzibari hii leo wana umoja wasiowahi kuwa nao kwa muda mrefu sana.
Wengi wao wenye kuuonja uhondo wa amani na utulivu hawakubali tena kubabaishwa au kutiwa fitna na kuletewa tena migawanyiko ya kuwafanya wananchi wawe na utengano. Kadhalika, juu ya rabsha za hapa na pale kwa jumla Zanzibar hii leo ni kisiwa cha amani.
Wazanzibari wanatambua umuhimu wa kuhakikisha kwamba amani na hali ya utulivu inaendelea kudumu ili waweze kufanikisha juhudi zao za kupigania pawepo na mfumo mpya wa ushirikiano kati ya Zanzibar na Tanganyika wakati wa mchakato wa sasa wa kuitunga upya Katiba ya Jamhuri ya Muungano ya Tanzania.
Hawatoweza kamwe kuyapata matlaba yao bila ya kuwa watu wamoja waliosimama pamoja na wenye kuamini kwamba kuwa watiifu kwa nchi yao na kuyapigania maslahi ya nchi yao ni jambo la wajibu na lililo muhimu na adhimu kushinda utiifu kwa chama chochote cha kisiasa au itikadi yoyote ya kisiasa.
Kuhusu suala hili, Wazanzibari wanaelewa vilivyo kwamba ikiwa hali ya amani itachafuliwa basi hali ya ndani ya nchi haitokuwa tulivu wala imara na itaitia nchi yao jina baya ulimwenguni. Kwa hakika, hali hiyo itakwenda kinyume na maslahi ya Zanzibar kwani baadhi ya watu wataanza kuwa na shaka ikiwa Zanzibar yenye mamlaka yake kamili itaweza kuhifadhi amani na hali ya utulivu na wakati huohuo kuwapatia Wazanzibari maendeleo ya kiuchumi na ya kijamii.
Kwa hivyo, katika kuuadhimisha mwaka wa pili wa uundwaji wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa ni muhimu Wazanzibari wa itikadi tofauti za kisiasa wahakikishe tena kwamba wamejitolea kuyatetea Maridhiano pamoja na umoja wao wa pamoja. Hizo ndizo nguzo mbili zitazowawezesha kutimiza lengo lao la kuwa na Muungano wa aina mpya na Tanganyika.
Kwa hili pia Wazanzibari wako macho na wanatambua kwamba kuna vitimbakwiri ndani na nje ya nchi wenye nia ya kuwababaisha wasishiriki kikamilifu katika mchakato unaoendelea wa kulipatia taifa katiba mpya. Zoezi hili ni muhimu kabisa kwa mustakbali wa vizazi vijavyo vya Wazanzibari. Suala hili ni kubwa kushinda masuala yote mengine ambayo hayana manufaa kwa ustawi na ufanisi wa Zanzibar.
Huu si wakati wake lakini nina hakika iko siku hao wenye kuleta chokochoko ama watafichuliwa na Wazanzibari wenzao au watajifichua wenyewe kwa njama zao. Itafika siku umma utachoka na chokochoko zenye lengo la kuubabaisha na kuutoa kwenye mstari wa kupigania pawepo mashirikiano mapya na Tanganyika.
Kuna safu mbili za wenye kuleta chokochoko hizo. Ya kwanza ni ile ya wahafidhina wa CCM/Zanzibar ambo tangu mwanzo walijitokeza wazi kuyapinga maridhiano. Hawa bado wanaendelea na vitimbi vyao.
Safu ya pili ni ya wale wanaojaribu kuihujumu Serikali ya Umoja wa Kitaifa bila ya kutanabahi kwamba nao pia wanaangukia kulekule kwa wahafidhina wa CCM. Wanachofanya hawa ni kuwatia mitegoni vijana wenye jazba nyingi lakini wasio na uweledi wa kisiasa.
Baadhi ya vitendo vya vijana hao tulivishuhudia wiki iliyopita wakati wa siku tatu za machafuko mjini Unguja. Hivi ni vitendo vya kulaaniwa kwani vina hatari ya kuweza kuudhuru umoja uliopo miongoni mwa wananchi. Aidha vitendo hivyo vinawapa nguvu wahafidhina wa CCM wathubutu kujaribu kupendekeza hatua ambazo zitaichafua hali ya amani na utulivu wa kisiasa uliopo na pingine kuudhoufisha msimamo wa kuwa na umoja wa pamoja wa kuipigania Zanzibar.
Hadi sasa dalili zilizopo zinaonyesha kwamba Wazanzibari wamevinjari kuendelea na umoja wao pamoja na Serikali yao ya Umoja wa Kitaifa. Hili ni jambo la kutia moyo. Wazanzibari wote kwa pamoja wana jukumu la jumla la kuidumisha amani na hali ya utulivu wa kisiasa mpaka na baada ya kuupata muradi wao.
chanzo: raia mwema

Sunday 21 October 2012

Omanis of Tanzanian origin maybe eligible for dual citizenship

 A constitutional review that is underway in Tanzania may lead to the passage of a bill that would enable Omanis who have roots in that country avail dual citizenship, according to President Jakaya Mrisho Kikwete, whose visit to Oman concluded on Friday
Speaking at a press conference on Thursday, Kikwete said Oman is the only country in the world whose citizens are related to many in Tanzania.
“I meet somebody from Oman and he says my relatives are in Tanzania. No country I have visited has such a relationship. Oman is a very special country for Tanzania, which is why consolidation and advancing of these relations is the top priority of the diplomacy of Tanzania,” Kikwete said.
He said his country is conducting a constitutional review during which dual citizenship will be considered.
“We are now in the process of doing a constitutional review and dual citizenship is one of the things that will be discussed. We have so many people of Tanzanian origin who have acquired citizenship of other countries. If the dual citizenship bill is passed, Omanis of
Tanzanian origin can now have the liberty to reclaim the citizenship of their ancestral home country.”
On the subject of Omani-Tanzanian relations, Kikwete said that Oman and Tanzania have long-standing and cordial relations with a history of over 100 years.
“Tanzania’s relations with Oman are very special. We are looking at ways to further expand and consolidate relations with the sultanate in trade and other sectors.
“Bilateral trade relations are good, but we can do even better. Currently, Tanzania gets investments of up to US$200mn (approximately RO77mn) from Oman. We need to explore new areas of cooperation in a bid to further strengthen and advance bilateral relations.”
He added that Omani investors should explore the vast investment potential in diverse sectors in Tanzania, which offers a number of tax incentives. “There are a great deal of investment opportunities in oil and gas, infrastructure, agriculture, mining and tourism, and
Tanzania is certainly one of the investment destinations of choice for Omani investors.”
Four agreements and memorandums of understanding to advance bilateral relations were signed during the Tanzanian President's visit.
“We signed an investment promotion and protection agreement that will facilitate Omani-Tanzanian investments such as free transfer of funds and profits, promote exchange of joint investment and protect investments against expropriation.
“We also inked an agreement to set up an Oman and Tanzania Joint Business Council, which was signed by both chambers of commerce.
Source: BBC News

Friday 19 October 2012

Pande zote za shilingi kuhusu Nyerere, kitendawili kigumu

WATAFITI wengi wamejaribu kuelezea kwa kina Julius Nyerere alikuwa binadamu wa aina gani, lakini baadhi yao wanaamini alikuwa ni mtu ambaye ni vigumu kumuelezea kinagaubaga taswira yake na mwenendo wake mzima kwa ujumla. Katika makala hii tutajaribu kumchambua angalau tupate ufunuo kuhusu hilo.
Katika zama zake kileleni Mwalimu, kama wafuasi wake walivyopenda kumwita, msomi huyu mahiri wa Afrika, alinyenyekewa mno kwa heshima na Watanzania wengi huku wengi pia wakimnanga kwa staili ya utawala wake ambao ulikuwa wa kibabe na wenye harufu za kidikteta. Wengine walimpa jina ‘dikteta mrahimu'.
Ukweli ni kuwa Watanzania mara kwa mara wamekuwa wakishindwa kutafsiri yale ambayo Mwalimu aliyasimamia, misimamo yake ya sera zenye misingi ya utu wa binadamu na azma zake za kifilosofia. Kuyajadili mafanikio yake na vilevile makosa yake.
Tumeshindwa kumsoma bila ya ushabiki, sijui ni kwa sababu za uvivu au ni woga. Kwa hakika, kwa yeyote atakaye kupanda ngazi ama ya kijamii au ya kisiasa, basi busara ya kawaida tu itamlazimu akwepe kutaja makosa ya Nyerere hata kama yanafahamika kwa wote. Hii imekuwa kama hulka ya Kitanzania.
Nyerere hayuko nasi leo na hii ni sababu nzuri ya kutaka kukumbuka kuwa hapo zamani alipata kuwapo mwanasiasa aliyeongoza harakati za kutafuta uhuru wa nchi hii; akabahatika kuaminiwa na watu wake; akajaribu kufanya yale aliyoamini kuwa ni ya manufaa kwa nchi yake; akalazimisha majaribio tata ya fikra na sera zake kwa wananchi wake aliowapumbaza, kwa muda wa miongo miwili na nusu na tofauti na watawala wengine wa Kiafrika, hakustaafu kwa kupinduliwa. Lakini mwishowe, kwa msaada wa masharti magumu ya kiuchumi ya Benki ya Dunia (Bretton Wood Institutions) aliachia ngazi, mwaka 1985.
Hivi Nyerere alikuwa ni nani? Je, alikuwa ni mwana wa chifu mmoja asiyejulikana kutoka madongokuinama aliyeamua kuishi maisha ya mtu wa kawaida? Je, alikuwa mkristo mzuri aliyevaa baraghashia ya kiislamu kama vazi lake la kawaida tu? Au, ni mwalimu msomi aliyeacha kufundisha ili ajiunge na siasa? Au, ‘Mkomunisti' aendaye kanisani kila leo na kupata sakramenti? Ama kiongozi aliyejizatiti kuwafikiria wananchi wake na ukombozi wa Afrika tu?
Yawezekana alikuwa muunganishaji aliyetuachia Muungano wenye nyufa tele? Au alikuwa mmajumui wa Afrika aliyekataa katakata kuanzishwa kwa Serikali moja ya Bara la Afrika. Haswa, huyu Nyerere alikuwa mtu wa aina gani?
Mwalimu alikuwa mtu mwenye familia njema na alijaaliwa watoto kadhaa. Ukweli sote tunaujua kuwa, familia yake iliishi maisha ya kawaida bila ya kuonyesha kiburi, fahari au kuwanyanyasa watu wa kawaida. Ukitambua namna Mwalimu akiogopwa, hata mara moja hakufikiria wala kujaribu kuendeleza ‘ufalme' kwa kumtayarisha mwanae au nduguye amrithi. Pengine angetaka, asingekuwapo wa kupinga! Lakini alipinga mchezo huo wa ‘ndugunaizesheni'. Na kwa hilo anastahili heko.
Hata hivyo, Mwalimu aliweza kufanya mengi ambayo hakuna aliyediriki kumzuia. Alifuta mfumo wa uchifu, alifuta serikali za mitaa, ushirika, vyama vya wafanyakazi na hata vyama vya siasa vya upinzani. Alitaifisha mali binafsi za watu, shule, hospitali na kila kilichomkalia sawa. Aliendesha uanzishwaji wa vijiji vya Ujamaa bila ya mpangilio wala ubinadamu, alisweka ndani wapinzani wake, alitekeleza sheria kadhaa kandamizi na kupiga marufuku maandamano na migomo. Sote tunakumbuka zama zile mambo haya yalikuwa ya kawaida kabisa. Mwalimu alifanya atakavyo na hakuna aliyesema fyoko!
Hadharani, Nyerere alijitahidi kuwaunganisha Watanzania kwa dhati kabisa. Watanzania kwa wakati ule walikuwa wachache mno kulinganisha na ukubwa wa nchi. Msimamo wake huu wa umoja ulijidhihirisha zaidi kwa namna alivyokuwa akiulinda na kuutetea Muungano wa Tanganyika na Zanzibar. Muungano ambao uliundwa chapchap, kwa kufumba na kufumbua macho na ukawa, kufuatia mapinduzi yaliyoendeshwa na genge dogo la watu pasipo na silaha za moto wala mafunzo ya kijeshi kumpindua Sultan Jamshid.
Miongo mitano imepita sasa na baada ya nyaraka za siri za Serikali ya Marekani kuwekwa bayana, wachambuzi wamekuwa wakihoji sababu za kweli ambazo ndizo chanzo cha Muungano huo kuundwa.
Pamoja na nia njema ya Nyerere, ukweli ni kuwa Muungano huo uliasisiwa na Serikali za Marekani na Uingereza kwa nia ya kuzuia uwezekano wowote wa ‘wakomunisti' kuteka mapinduzi ya Zanzibar. Hili lingewezekana kwa sababu Serikali ya ASP ilikuwa dhaifu mno na Abdulrahman Babu, kiongozi wa Umma Party na mkomunisti aliyekubuhu, aliwanyima raha Wamarekani, Waingereza na Nyerere. Kwa hiyo, Nyerere akalazimishwa na Wamarekani na Waingereza kupeleka askari kanzu 300 wa Tanganyika kwenda Zanzibar ili wamlinde Karume na Serikali yake, hii ikasaidia muda mfupi baadaye kumtisha Karume akubali haraka kutia sahihi mkataba wa Muungano.
Lakini ni vyema pia kukumbuka kuwa Nyerere mwenyewe alikumbana na zahma adhimu kama miezi miwili kabla Dar es Salaam kutokana na uasi wa kijeshi na yeye kuingia mafichoni kwa siku kadhaa. Akawaomba Waingereza wakaleta manowari na majeshi na kufanikiwa kumrejesha madarakani.
Kwa Mwalimu, tukio la yeye kuwaomba wakoloni msaada lilimuaibisha bila kifani. Kwa hiyo haikuwa vigumu ‘kumminya' Nyerere ili afanye kazi yao ya ‘Muungano' baada ya yeye kufaidi fadhila za Waingereza. Waswahili wana msemo, ‘Fadhila huzaa fadhila'. Hata hivyo, Mwalimu katika miaka yote hii, amekuwa akijitetea kuwa Muungano umesababishwa na sababu za udugu baina ya nchi hizi mbili na kuwa hii ni hatua ya mwanzo ya kufikia ‘Muungano wa Afrika' nzima.
Watanzania wanakumbuka fika kuwa kabla na baada tu ya Uhuru wa Tanganyika, taasisi zetu kama vile kampuni za reli, simu, posta, Idara ya Ujenzi na nyinginezo ziliweza kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi mkubwa.
Mathalan, reli waliweza kuendesha ratiba ya kuaminika ya safari za treni bila ya hitilafu. Barabara ya Dar es Salaam sehemu za Magomeni, Ilala, Kinondoni na Temeke zilikuwa ni za lami. Wazee wetu wanafahamu, hizo ndizo siku za kuzikumbuka kwa tabasamu.
Ilipofika mwaka 1975, miundombinu takriban yote ilikuwa nyang'anyang'a. Hali ilifikia pabaya. Nchi ilikuwa inaporomoka vibaya chini ya usimamizi wa Nyerere. Taratibu za kiutawala za Serikali Kuu zilidorora na nidhamu ilishuka vibaya. Miaka ya mwanzo ya themanini mashirika ya umma karibuni 400, karibuni yote mali ya watu binafsi iliyotaifishwa, yalikuwa yanakaribia kufilisika kutokana na ubadhirifu na wizi usiomithilika. Kwa Nyerere, ilikuwa dhahiri kuwa ‘majaribio' yake yalikuwa yamefeli ile mbaya.
Utaifishaji wa mali za watu binafsi uliofuatia Azimio la Arusha mwaka 1967 uliendeshwa vibaya kiasi cha kufikia hatua hata ya kutaifisha vijiduka vidogo vya rejareja vijijini kutoka kwa watu binafsi. Lakini Nyerere hakusita na zoezi liliendelea. Katika miaka ya kati ya sabini, Ujamaa ulikuwa unafaidi ruzuku na misaada mingi kutoka nchi za Scandinavia na China na ndiyo maana Mwalimu aliweza kuwapa wananchi wake elimu bure, huduma za afya bure na vingine vingi. Watanzania wakalemaa. Mwalimu naye akawa shujaa kwa watu wake angalau kwa muda mfupi. Haikupita muda Shirikisho la Afrika Mashariki likavunjika mwaka 1977 na kuathiri uchumi kwa kiasi kikubwa.
Punde si punde, Vita ya Kagera nayo ikaleta maafa makubwa kwa uchumi wa taifa. Ugumu wa maisha ukakaba taifa. Wachunguzi hata hivyo wanahoji sasa hivi kwa nini Mwalimu hakujaribu kutatua mgogoro ule kwa mazungumzo?
Hivi kweli ilikuwa lazima tupigane vita wakati Umoja wa Afrika (OAU) ulikuwa ukijaribu kusuluhisha? Hivi inawezekana, Mwalimu angetangaza vita kumng'oa Idi Amin kama sahibu wake wa karibu Milton Obote asingekuwa anapanga kunyakua madaraka nchini Uganda? Obote aliweka kambi za kijeshi hapa nchini kwa miaka mingi.
Hatimaye Obote alifanikiwa kurudi madarakani angalau kwa muda mfupi na kupinduliwa tena kwa sababu ya ubadhirifu mkubwa wa mali za umma na kurudi uhamishoni Zambia mpaka alipokufa miaka michache iliyopita. Vyovyote utakavyoangalia, leo hii bado nchi hii inajaribu kujiponya kutokana na athari za kiuchumi ambazo vita ile ilitusababishia. Urafiki wa Nyerere na Obote uligeuka tatizo letu la kitaifa.
Ilipofika hapo, uchumi ukiyumba na sera yake ya Ujamaa ikiwa inayoyoma, Nyerere sasa akawa amefikia ukomo wa safari yake. Amekwama! Manyang'au wa Benki ya Dunia na mafisi wa IMF wakafurahia kutokana na uhaba mkubwa wa chakula nchini. Wakasema, sasa umefikia wakati wa kumkomesha Nyerere kisawasawa. Naam, wakafanya ilivyotarajiwa, wakamwekea Mwalimu masharti magumu ya mikopo ya kunusuru uchumi wa nchi yake.
Kama mbinu ya kuwaliwaza wananchi wake Mwalimu akamruhusu Waziri Mkuu wake, Edward Sokoine (sasa marehemu) awashughulikie ‘wahujumu uchumi'. Akataifisha mali na kuwafunga matajiri. Akaanzisha Mahakama zisizo na uhalali wowote kuwahukumu. Mfano, mtu mmoja alifungwa miaka kadhaa kwa kuwa na televisheni. Na mwingine alienda jela kwa kuwa na kopo la dawa za tetracycline. Chini ya usimamizi wa Mwalimu, maafa makubwa yaliwapata wananchi wa kawaida na wakati mwingine yalisababisha vifo.
Kampeni hii ya uhujumu uchumi ya mwaka 1983 ilifananishwa na ujio mpya wa Azimio la Arusha la mwaka 1967. Utaifishaji huu holela uliojaa dhuluma ulithibitisha kuwa sera za Mwalimu zimeshindwa katika kuitawala nchi kwa ufanisi. Ukweli huu ulijidhihirisha zaidi katika siku zake za mwisho kabla ya kung'atuka. Ili kunusuru uchumi ilibidi akubali kushusha thamani ya sarafu ya nchi kutokana na masharti ya IMF.
Kung'atuka kwa Mwalimu ikawa ni suala la muda tu.
Ilipofika mwaka 1985, aling'atuka huku akiiacha nchi kwenye uchumi mbaya kuliko wakati wowote katika historia ya nchi hii. Hata hivyo, harakati kubwa zikafanywa na propaganda za kisiasa zikatekelezwa ili kumpa kisingizio cha muonekano kuwa, Mwalimu aliamua kustaafu urais kwa hiari yake.
Katika historia, ni vyema tukakumbuka, moja ya nyakati ambazo Nyerere alijikwaa na kuvurunda ilikuwa pale alipounga mkono kujitenga kwa Jimbo la Biafra kule nchini Nigeria. Hiyo ikiwa kinyume kabisa na maazimio ya Umoja wa Afrika ambayo Nyerere aliiasisi. Aliivalia njuga kampeni hii hadi kukusanya michango na misaada isiyo ya hiari nchi nzima, na kuipeleka Biafra. Ilishangaza wengi duniani kuwa Nyerere alikuwa anashadidia kuvunjika kwa taifa huru la Nigeria.
Siri ilikuja kufichuka baadaye ilipothibitika kuwa kumbe mpango mzima ulikuwa ni hila tu za Kanisa Katoliki zikisimamiwa na Nyerere, Houphouet Boigny wa Ivory Coast na Rais Eyadema wa Togo. Hiyo ilishusha kwa kiasi heshima na uadilifu wa Nyerere miongoni mwa Waafrika na vita hiyo ya Biafra ikisababisha vifo visivyo na lazima, takriban milioni moja na maafa makubwa. Kwa bahati, Nigeria kama nchi ikasalimika.
Pamoja na mikenge yote hiyo, Mwalimu alisifika kwa msimamo wake, hususan katika mambo ambayo aliyaamini. Alikuwa hatetereki asilani. Alipiga vita ukabila kwa kuwastaafisha machifu wote nchi nzima baada tu ya Uhuru. Alifanya juhudi za makusudi kuimarisha na kuirasimisha Lugha ya Kiswahili. Aligundua baadaye umuhimu wa lugha hii kama nyenzo ya kuimarisha utawala wake. Alipiga vita rushwa na ufisadi bila ya kuchoka. Alitetea wanyonge mpaka mauti yalipomkuta na hakusita kuwabamiza wale wote walionadi sera za kibaguzi. Na baada ya kustaafu, aligeuka mkosoaji mkubwa wa serikali hadi kuchukiwa kwa uchokonozi wake dhidi ya matumizi mabaya ya madaraka.
Kiukweli kabisa, Mwalimu alikuwa na umahiri mkubwa kama mzungumzaji na ufasaha wake wa lugha ulimbeba. Angeweza kusema chochote wakati wowote. Na wasikilizaji wakasikiliza na kumwelewa. Ni kipaji tu. Alipokuwa akizungumza wasiompenda walikuwa wanaungua kwa ghadhabu, na alipoamua kujibu mapigo ya mahasimu wake ilikuwa ni balaa, watu waliingia mitini. Cha kushangaza zaidi ni kuwa Kiswahili na Kiingereza ni lugha mbili alizozimudu kwa kina lakini zote hizo hazikuwa lugha mama kwake. Alijifunzia ukubwani kwa kujizatiti sana.
Lakini Mwalimu alitambulika kwa tabia yake ya uropozi. Alikuwa hamkopeshi mtu na kwa hiyo tabia yake ilikuwa ni neno kwa neno. Kuna wakati mmoja alikorofishana na Margaret Thatcher, Waziri Mkuu wa Uingereza aliyepita na kumbwatukia ‘Bi Thacher anafanya uhuni na heshima ya taifa lake' au pale alipomnanga Idi Amin na kumuelezea kuwa ‘… Amin ana kichaa kilichosababishwa na kaswende'. Ni kutokana na hulka hii basi haikushangaza kumsikia Ian Smith, Waziri Mkuu dhalimu wa Rhodesia akimwita Mwalimu ‘ibilisi mbunifu'.
Mwalimu, katika uhai wake ameandika vitabu vingi na tenzi na mashairi pia. Hata hivyo, aligoma kabisa kuandika kitabu kuhusu maisha yake yeye mwenyewe. Watu kadhaa wa karibu kwake walimsihi sana lakini wapi. Ni ngumu kuelewa kwa nini basi, Mwalimu ambaye alisikiliza sana dhamira yake katika kila jambo alilotenda lakini kinyume chake aliishi maisha yake yote huku akiwaza namna historia itakavyomkaanga hapo baadaye.
Kisiasa, Mwalimu ametuachia CCM iliyojaa wafuasi maamuma na mbumbumbu wakiongozwa na genge dogo la watu wenye uchu wa madaraka wanaopenda kujilimbikizia mali. Wazoefu wa kuimba nyimbo za kusifiana kwa vigelegele na makofi mengi. Chaguzi za Chama cha Mapinduzi zimegeuka gulio la kuuza na kununua kura mchana kweupe. Na hao wanaojinasibu kuwa ni wafuasi wa Nyerere hutumia nukuu zake na wosia wake pale tu wanapokuwa na maslahi binafsi. Hawa hawakujifunza kitu kutoka kwa Mwalimu.
Hivi sasa kuna fukuto la mvutano wa kidini nchini. Waislamu wanalalama kuwa kwa makusudi Mwalimu alitumia urais wake kunufaisha ukristo na wakristo katika teuzi za uongozi, nafasi za masomo na ugawaji wa keki ya taifa. Mwalimu katuachia tatizo hili na sasa linatishia utaifa wetu.
Na hivi tunavyoadhimisha miaka 13 ya kifo chake, mtu huyu ambaye alionekana kama vile anapiga vita udini, Kanisa Katoliki liko mbioni kumtakasa na kumtawaza kuwa ni ‘mtakatifu'. Hatua hii imezaa utata na maswali mengi. Watu wanauliza je, Kanisa lina ajenda gani?
Nimalize kwa kuangalia utawala wa takriban robo karne Mwalimu akiwa kiongozi wa nchi hii. Mwishoni, Mwalimu alishitushwa sana na namna mambo yalivyokwenda segemnege, hakutarajia kuwa Watanzania wale ambao alidhani wamemuelewa kumbe walimpuuza. Walimsikia lakini hawakumsikiliza. Aliangalia nyuma na kutazama uharibifu aliouacha na mambo yote yalivyoparaganyika. Alisononeka mno.
Mwisho wa siku Mwalimu hakuwa na marafiki wa kweli, familia yake iliathirika kutokana na kukosa malezi yake, umasikini nchini bado umetamalaki, ujinga nao umejikita, huduma za afya zimedorora na hazitoshelezi, Muungano unayumba na rushwa na ufisadi vimeshamiri kila sekta. Kama vile madhila hayo hayatoshi, CCM ilitupilia mbali zile tunu mbili za Nyerere, yaani siasa ya Ujamaa na Azimio la Arusha. Kwa Nyerere huo ulikuwa mithili ya uhaini, aliiona CCM ikimsaliti angali hai.
Kwa vile kila alichosimamia Nyerere hakikusimama badala yake kiliporomoka, Mwalimu alikufa akiwa na usongo mkubwa moyoni, Mwalimu aliaga dunia huku akisononeka kutokana na kuangushwa na watu waliomzunguka.
Nyerere alikuwapo na daima hakutokuwa na Nyerere mwingine. Ni dhahiri, Nyerere alikuwa ni kitendawili.
Chanzo: Raia Mwema

Friday 12 October 2012

Jinsi moyo alivyowasuta wanaojaribu kuuvunja umoja wa Wazanzibari

WIKI iliyopita nilizungumzia kuhusu umuhimu wa nchi kama Zanzibar ya leo kuwa na siasa za umoja badala ya kuwa na siasa za mivutano. Hii ni mivutano yenye kutishia amani ya nchi na hupaliliwa na vyama vya kisiasa.
Niligusia pia juu ya umuhimu wa kuiweka nchi mbele badala ya kuweka sera za chama — kuyapa kipaumbele maslahi ya kitaifa badala ya maslahi ya kichama. Kwa ufupi, nikizungumzia juu ya haja ya kuwa na vuguvugu la umoja wa kizalendo.
Kwa sadfa Jumamosi iliyopita palifanywa kongamano kubwa mjini Unguja, kongamano ambalo ni mfano mzuri wa siasa za umoja, nilizokuwa nikizizungumzia. Kongamano hilo, lililokuwa chini ya uwenyekiti wa Profesa Abdul Sheriff (mmoja wa wanahistoria waliobobea barani Afrika) liliandaliwa na Kamati ya Maridhiano chini ya uwenyekiti wa Hassan Nassor Moyo.
Wajumbe wengine wa kamati hiyo kwa upande wa CCM, ni Waziri asiye kuwa na Wizara Maalum na Mwakilishi wa Kiembe Samaki, Mansour Yusuf Himidi na Eddy Riyami ambaye ni mkereketwa wa CCM. Kwa upande wa CUF walikuwamo Waziri wa Sheria na Mambo ya Katiba, Abubakar Khamis Bakary, Mkurugenzi wa Uenezi wa CUF, Salim Bimani na Ismail Jussa Ladhu, Mwakilishi wa CUF wa Mji Mkongwe ambaye wiki iliyopita alijiuzulu wadhifa wake wa Naibu Katibu Mkuu wa CUF.
Hawa Wazanzibari sita wamekuwa kama gundi inayoishikilia Serikali ya Umoja wa Kitaifa ya Zanzibar na kuhakikisha kwamba mshikamano na umoja wa Wazanzibari unaendelea kwa manufaa ya taifa letu. Kongamano hilo lililofanyika katika Hoteli ya Bwawani, lilikuwa ni la kihistoria. Hapajawahi katika historia nzima ya kisiasa ya Zanzibar kufanywa mjadala wa kitaifa kama uliofanywa kwenye mkusanyiko huo na kuhudhuriwa na watu kutoka vyama tofauti vya kisiasa na kutoka taasisi na jumuiya mbalimbali za Zanzibar zikiwa pamoja na za kidini.
Ijapokuwa kongamano hilo lilikuwa la kwanza la aina yake kuandaliwa visiwani, inasikitisha kwamba vyombo vingi vya habari vya Tanzania Bara vililibeza. Lile tangazo la pamoja la kongomano hilo halikusambazwa na vyombo hivyo vya habari kama inavyostahili. Zanzibar kwenyewe kongomano hilo halikuweza kupuuzika. Yaliyokuwa yakizungumza na kujadiliwa kwenye kongamano hilo, yalirushwa na stesheni za televisheni zisizo za Serikali, na yalitangazwa na steshini za redio zilizo huru na hata kwenye majukwaa mbadala na mitandao ya mawasiliano ya kijamii.
Mada ya kongamano ilikuwa ‘Nafasi ya Zanzibar Katika Mchakato wa Katiba Mpya.’ Jambo lililotia moyo katika mjadala huo ni kwamba hakukuwa na maoni yaliyokuwa yakikinzana wala hakuzuka yeyote aliyetoka kwenye mstari wa maudhui. Hilo pekee lilizidi kuthibitisha jinsi Wazanzibari hii leo wanavyozidi kuwa na umoja wa fikra kuhusu mstakabali wao.
Jengine lililotia moyo ni kuwaona waliokuwa wakichangia kwenye mdahalo huo kuwa ni watu wa itikadi tofauti za kisiasa na kutoka vyama na jumuiya mbalimbali lakini wote wakishikilia uzi mmoja: uzalendo wa Wazanzibari.
Ilifurahisha kumsikia Moyo akiwajibu baadhi ya wazee na viongozi wenzake wa CCM-Zanzibar waliokuwa wakijaribu kumkwaruza na kumvunjia heshima yake kwa sababu ya msimamo wake kuhusu mustakabali wa Zanzibar. Moyo, mwenye kadi namba 7 ya CCM, alizungumzia zaidi juu ya Maridhiano yaliyosaidia kuuleta huu umoja uliopo sasa Visiwani.
Tukimwacha Moyo, mzee mwingine aliyezungumza alikuwa Salim Rashid aliyekuwa katibu wa mwanzo wa Baraza la Mapinduzi, na aliyewahi kuwa waziri na balozi wa Tanzania nchini Guinea na Ethiopia. Alitoa mbiu mpya ya kuwataka Wazanzibari wawe na ‘Umoja wa Pamoja’ kupigania maslahi yao.
Vigogo wengine waliozungumza katika kongamano hilo, walikuwa ni pamoja na Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar, Othman Masoud Othman, Mkurugenzi wa Mashtaka, Ibrahim Mzee, Amiri Mkuu wa Jumiki, Sheikh Msellem Ali Msellem, Mansour Yusuf Himidi, Mwenyekiti wa ZAHILFE Kassim Hamad Nassor, Mwakilishi wa WAHAMAZA, Salma Said, Mwakilishi wa UKUWEM Dk Mohamed Hafidh, Rais wa Zanzibar Law Society, Salim Toufiq na Khalid Gwiji ambaye ni Mwenyekiti wa Vijana wa Umoja wa Kitaifa.
Mwingine aliyeusisimua mkutano huo kwa mchango wake, alikuwa Padri Emmanuel Masoud wa Kanisa la Kianglikana kutoka Pemba, ambaye alisisitiza kwamba aliyokuwa akiyasema yalikuwa maoni yake na hayayawakilishi yale ya Kanisa lake. Kasisi Masoud alisema kwamba yeye ni Mzanzibari kutoka Pemba mwenye kuyaunga mkono Maridhiano ya Rais Mstaafu Amani Abeid Karume na Maalim Seif Sharif Hamadi, Katibu Mkuu wa CUF. Aliongeza kwamba yeye vilevile anaunga mkono Muungano wa Mkataba na anataka Zanzibar iwe na mamlaka yake kamili.
Hamna shaka yoyote kwamba Maridhiano ndiyo yaliyowezesha pakapatikana hali ya amani na utulivu Zanzibar. Na inavunja moyo tunapowasikia baadhi ya viongozi wa CCM na baadhi wakereketwa wakongwe wa chama hicho wakitia fitna ambazo hatima yake itakuwa ni kuirejesha Zanzibar kule ilikotoka kwenye chuki za kisiasa na kikabila, uhasama na umwagaji wa damu.
Bila ya shaka ni kweli kwamba panapokuwako siasa za umoja, haimaanishi kwamba tofauti za vyama zinayayuka na kutoweka moja kwa moja papo kwa papo. La. Tofauti hizo huendelea kuwako, lakini zinakuwa zinawekwa kando na hazitiliwi sana maanani. Kinachotiwa maanani ni maslahi ya nchi. Katika mfumo kama huo, nchi huja mwanzo halafu ndio vinakuja vyama au vivyama.
Inapokuwa lazima tofauti hizo zijitokeze, basi hujitokeza kwa njia za kistaarabu na mazingira ya kuvumiliana.
Lakini hivyo sivyo wanavyofanya baadhi ya wapinzani wa Maridhiano. Daima kunakuwa na hatari kwamba siasa za umoja zinapochezwa, huenda pakazuka vidudumtu au vitambakwiri vitakavyotaka kuuvunja huo umoja uliopo. Potelea mbali nchi iteketee au iangamie, madhali wao wanapata maslahi yao. Kuhusu Serikali ya Umoja wa Kitaifa ya Zanzibar, tunaiona hatari hiyo ikitoka kwa wahafidhina wa CCM-Zanzibar.
Wote hao wanakuwa wanafanya dhambi kwa sababu wanakuwa wanakwenda kinyume na mkondo wa kihistoria. Kwa wakati huu tulio nao sasa, historia ya Zanzibar inashurutisha kwamba lazima pawepo na siasa za umoja. La sivyo basi, visiwa vya Zanzibar vitaangamia.
Katika hali iliyoko Zanzibar, siasa za umoja si jambo linalohitajika tu, bali siasa hizo zinakuwa ni kama silaha ya kutumiwa kupigania haki katika vuguvugu la kidemokrasia. Aidha, siasa za aina hiyo zinakuwa zinazitoa kasumba za kiitikadi zinazoshadidiwa na uchama. Kasumba hizo hutumiwa na viongozi wakorofi kuwalewesha wafuasi wa vyama vyao.
Kwa kweli siasa za umoja zinakuwa na uwezo wa kuwafungua huru wananchi na kuwafanya wasifungwe tena na pingu za kichama. Lengo lao linakuwa kupigania tu nchi yao na maslahi ya nchi yao na ya vizazi vyao. Faida nyingine ya siasa za umoja, ni kwamba zinaweza kuwafungua macho na kuwazindua wananchi waliozugwa kwa itikadi za kichama. Wanaowazuga hao wananchi aghalabu huwa ni wanasiasa wanaofanya hivyo kwa makusudi ili wafuasi wao wasiweze kujiamini na kuwa na msimamo wa kuiweka nchi mbele.
Wanasiasa hao wanapowaona wafuasi wao wamesimama kidete na hawateteleki, basi huanza kupapatika. Na wakianza kupapatika, ndipo wanapotumia vitisho kuwatisha wafuasi wao. Tumeyashuhudia hayo yakitokea Zanzibar pale baadhi ya viongozi wa CCM wenye msimamo ulio kinyume na ule wa wafuasi wao, wanapoanza kuwatishia baadhi ya wenzao wenye msimamo tofauti na wao kwamba watawafukuza chamani. Hawaishii hapo, bali wanauvua ustaarabu wao na wanaanza kuwatupia wenzao kila aina ya matusi.
Hiyo ni ishara ya kwamba viongozi hao wanaojiona kuwa ni wababe, kwa kweli wamekuwa muflisi wa kisiasa. Si hayo tu, bali wanajiona kuwa wanazama baharini na hawajui washike nini ili wajiokoe; ndipo wanapovamia vitisho na kuanza kuvitumia dhidi ya wenzao. Na wanapotumia hivyo vitisho ndipo wanapozidi kujikashfu na kuonekana kuwa si chochote bali ni ‘chui wa karatasi’ chambilecho Mwenyekiti Mao.
Kongamano la Jumamosi iliyopita, limethibitisha kwamba siasa za umoja zinaweza zikatumiwa kwa mafanikio kuwaunganisha wananchi na kuwafanya wajipange kupigania maslahi yao. Kadhalika siasa za aina hiyo, zinapokuwa zinaanza kuiva na kupevuka kama zilivyo sasa Zanzibar, huwavutia wananchi wengi zaidi. Hata wale wasiokuwa zamani wakijihusisha na siasa, huanza kujiingiza uwanjani kupigania maslahi ya taifa lao.
Hiyo ndiyo sababu ya kwa nini ukumbi uliofanyiwa kongamano ulifurika umati, wengi wao wakiwa vijana. Kwamba wengi waliohudhuri kongamano hilo walikuwa vijana ni jambo jingine lenye kutia sana moyo kwa vile mustakabali wa nchi yao, umo mikononi mwao.
Juu ya hayo yote, hali tuliyonayo Zanzibar ni tata. Ina mazongezonge mengi na si sahali au nyepesi hata kidogo. Hivyo, vijana lazima watambue kwamba mapambano yoyote ya kuleta mageuzi huwa na hatua nyingi za kupitia. Kwanza huanzia na fikra za kutaka kuleta mageuzi katika jamii fikra ambazo hutokana na shauku ya umma ya kutaka kuwa huru. Fikra kama hizo, daima huwachemsha wananchi wenye kuipenda nchi yao. Kwa taratibu watu huanza kushawishika na kujitolea kuchukua hatua nyingine za kusonga mbele na mapambano.
Kwa sasa Zanzibar imekwishaipita hatua hiyo. Muhimu ni kwamba vijana wasipoteze dira wala wasijiachie wakayumbishwa na wanasiasa wanaotaka kuyarejesha ya kale na kuitokomeza nchi.
Raia mwema

Sunday 7 October 2012

Seif asema Tunataka Zanzibar yetu

“Mimi sitafuni maneno kwamba ni muumini wa Zanzibar yenye mamlaka kamili kitaifa na kimataifa itakayofuatiwa na mashirikiano kati yake na Tanganyika kupitia Muungano wa Mkataba. Namshangaa leo anakuja kiongozi wa Zanzibar anasema tuna bendera na muhuri na wimbo wa taifa, hayo yanatosha. Hivi huyu anajua anachokisema au anatumikia maslahi ya waliomtuma? Una bendera gani hii ambayo mwisho wake Chumbe? Mimi nataka niione bendera ya Dola ya Zanzibar inapepea Umoja wa Mataifa, New York pale. Nataka tuwe na Paspoti ya Zanzibar, nikisafiri nitoe Paspoti ya nchi yangu. Nataka tuwe na Ofisi za Kibalozi za Zanzibar katika nchi za nje.
Leo hata mamlaka ya kiuchumi hatuna. Tumeamua rasilimali yetu ya mafuta na gesi asilia yasiwe mambo ya Muungano, mpaka leo Tanganyika wamekwamisha, wanatuzuia tusinufaike na rasilimali zetu tukajenga uchumi wetu. Wanasema tuna viwango na mfumo mmoja wa kodi lakini bidhaa zikitoka Zanzibar wanazitoza ushuru tena. Lengo ni kuua uchumi wetu ili hatimaye tudhoofike na tusalimu amri kwao. Yaguju! Wasahau hilo. Leo hata katika mikutano ya kimataifa, viongozi wetu wa Zanzibar hawapewi heshima ya uwakilishi wa nchi yetu.
Inafika mahala hata Naibu Waziri tu wa Bara anaongoza ujumbe wa Tanzania wakati kuna Waziri kamili kutoka Zanzibar lakini haheshimiwi. Tutarejesha mamlaka yetu kamili. Tuwe na Benki Kuu, tuwe na sarafu yetu ya Zanzibar, tupange uchumi wetu kwa maslahi ya watu wetu. Tunataka tuwe na uanachama katika jumuiya na mashirika yote ya kimataifa. Tuwe na Waziri wa Mambo ya Nje wa Zanzibar. Tuwe na uwezo wa kuingia mikataba na nchi za kigeni. Hayo ndiyo tunayoyataka. Tukisema hivi hatuna maana tunataka ugomvi na Tanganyika. Hapana! Tunataka tuwe majirani wema na Tanganyika kama tutakavyokuwa na ujirani mwema na Kenya. Hayo yatafikiwa kupitia Muungano wa Mkataba wa Madola mawili huru kamili.”
Chanzo: Mzalendo

MWONGOZO KUHUSU UTARATIBU WA WATANZANIA WANAOISHI UGHAIBUNI KUSHIRIKI KUTOA MAONI YAO KUHUSU UPATIKANAJI WA KATIBA MPYA

Kwa kuwa mchakato wa kupata Katiba Mpya ni utaratibu unaosimamiwa na Sheria ya
Mabadiliko ya Katiba, Sura ya 83; tunashauri kuwa Watanzania wote wanaotaka kushiriki
katika mchakato huo ni vizuri kuzifahamu Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya
mwaka 1977 na Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, Sura ya 83 ambazo zote zinapatikana
katika tovuti ya Tume ambayo ni www.katiba.go.tz
Kusoma Sheria hizo kutasaidia kuielewa Katiba ya sasa ubora na upungufu wake na
kuelewa utaratibu na masharti yanayoainishwa kisheria kuhusiana na mchakato wa
upatikanaji wa Katiba Mpya.
1. MAMBO YA KUZINGATIA
Kwa kuwa uratibu na ukusanyaji wa maoni unatawaliwa na kusimamiwa na Sheria, Tume
inaelekeza mambo yafuatayo yazingatiwe:
(a) Nani Mwenye Haki ya Kushiriki:
Mtu yeyote ambaye ni Mtanzania kwa uraia wake anayo haki ya kushiriki katika
mchakato huu. Mtu ambaye kwa asili yake ni Mtanzania, lakini amepoteza uraia wa
Tanzania hatoweza kushiriki; na akifanya hivyo atakuwa ametenda kosa chini ya
Sheria.
(b) Utaratibu wa Utoaji Maoni:
Njia tatu za ukusanyaji wa maoni zitatumika. Njia hizo ni kama zifuatazo:
(i) utoaji wa maoni kupitia mitandao ya kijamii, tovuti (www.katiba.go.tz) barua
pepe ya Tume, (katibu@katiba.go.tz), nukushi + 255-22-2133442 begin_of_the_skype_highlighting FREE + 255-22-2133442 end_of_the_skype_highlighting na
+255-224-2230769 na
(ii) utoaji wa maoni kupitia nyaraka na barua zitakazotumwa kwa Tume kutumia
anwani ya Tume, ambao ni: Katibu, Tume ya Mabadiliko ya Katiba, S.L.P.
1681 DSM au Ofisi ndogo ya Tume, S.L.P. 2775 Zanzibar.2
Endapo Mtanzania anayeishi Ughaibuni atabahatika kuwepo Tanzania wakati wa
ukusanyaji wa maoni, anaweza kushiriki katika mchakato huo kama Watanzania
wengine walioko nchini kwa kuhudhuria mikutano ya kukusanya maoni iliyoandaliwa
na Tume.
(c) Utambulisho wa Mtoa Maoni:
Kila mtu atakayetoa maoni yake Tume anapaswa kubainisha mambo yafuatayo:-
(i) majina yake matatu;
(ii) namba ya pasi yake ya kusafiria na mahali ilipotolewa;
(iii) nchi na mji anaoishi;
(iv) endapo atatumia nyaraka au barua, ataambatanisha kivuli cha pasi yake
(ukurasa unaoonyesha maelezo ya mtu mwenye pasi hiyo).
Tume inapenda kuwakumbusha tena Watanzania kuwa utoaji wa maoni ni jambo la uhuru
na hiari ya mtu na kwamba mchakato wa kupata Katiba Mpya unawahusu raia wa Tanzania
pekee.
“TOA MAONI, TUPATE KATIBA MPYA”

Saturday 6 October 2012

HOTUBA YA MAKAMU WA KWANZA WA RAIS WA ZANZIBAR

HOTUBA YA MAKAMU WA KWANZA WA RAIS WA ZANZIBAR, MHE. MAALIM SEIF SHARIF HAMAD KWA WAANDISHI WA HABARI KATIKA UTARATIBU WA VIONGOZI KUKUTANA NA WAANDISHI KILA BAADA YA MIEZI MITATU KUZUNGUMZIA UTENDAJI SERIKALINI HUKO HOTELI YA GRAND PALACE MALINDI MJINI ZANZIBAR TAREHE 6 OKTOBA 2012
Waheshimiwa Waandishi wa habari
Kwanza kabisa sina budi kumshukuru Mwenyezi Mungu Mtukufu kwa kutuweka katika hali ya uzima hadi kukutana tena leo kuzungumzia utendaji na majukumu yetu tuliyokabidhiwa na wananchi wa Zanzibar katika serikali yetu ya awamu ya saba ya uongozi ambayo imetimiza takriban miaka miwili sasa.
Pili natoa shukurani zangu za dhati kabisa kwenu nyinyi wanahabari mliotenga muda wenu kuja kuhudhuria kwa wingi kuitikia wito wetu wa kutusikiliza, na baadaye kupata fursa ya kuomba ufafanuzi wa masuala mbali mbali yanayohusu maendeleo ya nchi yetu katika nyanja za kiuchumi, kijamii, kisiasa na mambo yote yanayogusa jamii ya Wazanzibari kwa jumla.
Waheshimiwa Waandishi wa habari
Nianze sasa, kuzungumzia mafanikio kwa jumla tuliyoweza kuyapata na changamoto tunazokabiliana nazo katika kipindi hichi cha mwaka wa pili wa serikali ya awamu ya saba. Waheshimiwa katika nchi yetu tunaendelea kujivunia hali ya amani na utulivu katika nchi yetu ya Zanzibar. Wananchi wote wanapata fursa na uhuru wa kufanya shughuli zao za kujiletea maendeleo na kuendeleza mshikamano miongoni mwao. Hali hii hatuna budi kudumisha kwa kuenzi misingi ya maridhiano ya kisiasa yaliyofikiwa Novemba 5, mwaka 2009 na baadaye kuwa msingi wa kupatikana serikali hii shirikishi yenye Muundo wa Umoja wa Kitaifa.
Kutokana na nchi yetu kuendelea kudumu katika hali ya amani, utulivu na maelewano, wananchi wamekuwa wakiitumia kikamilifu fursa na neema hiyo kushiriki katika shughuli za kujieletea maendeleo, ambapo pia serikali inaendelea kusimamia majukumu ya wananchi kikamilifu, ikiwemo kukuza uchumi wake kwa mintaarafu ya kuwapunguzia wananchi ugumu wa maisha yao.
Katika mwaka 2011 uchumi wetu ulikuwa kwa asilimia 6.8 huku matarajio katika mwaka huu wa 2012/2013 yakionesha dalili njema kutokana na tulivyojipanga, ambapo uchumi huo unatarajiwa kukuwa kwa asilimia 7.5. Vile vile pato la Mzanzibari limekuwa kutoka T.SHS 782,000 kwa mwaka hadi kufikia TSHS 960,000 ambazo ni sawa na dola za Marekani 615 kutoka 560 mwaka 2010.
Kwa vyovyote vile, bila ya kuwepo hali ya amani na utulivu na maelewano miongoni mwetu tusingeweza kujenga imani kwa wawekezaji vitegauchumi ambao hadi sasa wanaendelea kujitokeza kwa wingi na kutuunga mkono kwa kuwekeza miradi yao. Bila shaka hali hiyo inatokana na kuridhishwa kwao na amani na utulivu uliopo.
Hata hivyo, lazima tukiri kuwa bado tunayo kazi nzito mbele yetu ya kuzidisha bidii kwa kila mmoja wetu, kuiunga mkono serikali katika kuhakikisha nchi inaendelea kubaki katika hali ya amani na utulivu na kusaidia kukuza kasi ya kuimarika uchumi wetu.
Kwa kufanya hivyo ndipo tutaweza kuyafikia malengo ya Milenia, ambapo nchi zote zinatakiwa ifikapo mwaka 2015 pato la wananchi wake liwe limefikia T.SHS 884,000. Hata hivyo tunapaswa kuzidi kuwajengea matumaini wananchi wetu, ambao wanaamini hali ya kukua kwa uchumi wa nchi, haina budi kuambatane na fedha kuonekana mifukoni na sio kwenye makaratasi.
Sekta za Kilimo, Biashara na Huduma zimeendelea kupewa msukumo mkubwa na kuendelea kuchangia kwa kiasi kikubwa uchumi na mapato ya wananchi wetu. Kwa mfano katika Huduma, utalii umeendelea kutoa mchango wa kipekee katika uchumi wa Zanzibar. Sekta hii inachangia asilimia 80 ya fedha za kigeni na asilimia 70 ya wananchi wetu wanafaidika katika sekta hii kwa njia moja ama nyengine.
Mwelekeo wa Serikali yetu ni kuzidi kuiimarisha sekta hii ya Utalii, ili iendelee kutoa mchango mkubwa zaidi kwa wananchi. Na katika kuhakikisha lengo hilo tunalifikia, hivi sasa serikali imekuja na mkakati mpya wa “Utalii kwa Wote”. Mkakati huu tayari umezinduliwa rasmi, na lengo la kuanzishwa kwake ni kuhakikisha kila mwananchi Mzanzibari popote pale alipo Unguja na Pemba ananufaika na sekta hii ya utalii.
Waheshimiwa Waandishi wa Habari
Kama nilivyogusia hapo awali mafanikio ya mikakati na malengo yote hayo tuliyoyaeleza yatatokana na nchi yetu kuendelea kudumu katika hali ya amani, utulivu na maelewano miongoni mwa wananchi wake.
Katika nchi yetu ni ukweli uliowazi kwamba wapo baadhi ya wananchi ama hawajaelewa, au wameamua kukataa hali hii ya maridhiano na maelewano miongoni mwetu. Watu hao wakiwemo miongoni mwa baadhi ya watendaji serikalini wamekuwa na mwenendo ambao matokeo yake yanaweza kuleta mgawanyiko na kuvuruga hali hii ya mshikamano na amani tunayojivunia.
Serikali itaendelea kuchukua juhudi kubwa kuwaelimisha juu ya umuhimu wa maridhiano yetu na kuwafahamisha kwamba wananchi walio wengi hivi sasa hawako tayari kurudi nyuma tulikotoka kwenye hali ya mifarakano na chuki miongoni mwa jamii.
Waheshimiwa Waandishi wa Habari
Katika mkutano kama huu na waandishi wa habari mwaka jana, nilijikita zaidi kuzungumzia changamoto za kiuchumi ambazo zimesababisha ugumu wa maisha kwa Wazanzibari walio wengi, zikiwemo mfumuko mkubwa wa bei za bidhaa muhimu kama vile, mchele, sukari, unga wa ngano na nyenginezo na kueleza mipango tuliyokuwa tumejipangia. Leo nimepanga nizungumzie zaidi kwa kifupi changamoto za ndani zinazojitokeza katika utendaji wa kila siku serikalini.
Waheshimiwa
Katika utendaji wetu serikalini katika kipindi hiki cha miaka miwili, bado tunakabiliwa na changamoto nyingi. Kati ya hizo ni kudhibiti matumizi holela ya fedha za umma miongoni mwa watendaji wetu. Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali mwaka 2010/2011 inaonesha bado kuna watendaji ambao wamedhamiria kujinufaisha binafsi kupitia fedha za serikali. Wanafanya hivyo, licha ya hatua na juhudi kubwa zinazochukuliwa kuwakataza na kuhimizana kujali misingi ya Utawala Bora.
Pamoja na marekebisho katika baadhi ya maeneo lakini bado kila zinapotoka ripoti za Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu, zinaonesha suala la matumizi yasiyofuata taratibu linaendelea kujitokeza.
Kuna udhaifu mkubwa wa kukosekana baadhi ya vielelezo muhimu katika ukusanyaji na matumizi ya mapato. Aidha, kumegundulika kujitokeza udanganyifu katika utayarishaji wa mafao ya baadhi ya wastaafu.
Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ameanza utaratibu wa kukagua miradi ya maendeleo na kujiridhisha kuwa kazi iliyofanyika inalingana na thamani ya fedha zilizotumika. Imegundulika katika baadhi ya miradi, fedha zilizolipwa ni nyingi sana ikilinganishwa na kazi iliyofanyika pamoja na ubora wa kazi wenyewe kuwa haulingani kabisa na fedha zilizolipwa.
Napenda kutoa wito maalum kwa watendaji serikalini kuacha tabia ya udokozi wa fedha za wananchi, na wahakikishe wanafuata taratibu na kanuni za matumizi ya fedha za umma. Aidha, serikali haitavumilia kuona baadhi ya watendaji wanaendelea kukiuka sheria zilizopo na kuchukua fedha za wananchi kujinufaisha wao binafsi.
Sote tunaelewa ni kwa kiasi gani serikali inavyojibana katika matumizi, ili kuhakikisha mapato hayo kidogo yanayopatikana yanatumika katika shughuli za maendeleo na za kijamii.
Hivi sasa serikali inafanya kila linalowezekana kuhakikisha inapata usafiri wa uhakika wa baharini, kwa azma ya kuwaondolea usumbufu wananchi na wageni wanaohitaji kusafiri kati ya Unguja na Pemba na Tanzania Bara. Jambo hilo linahitaji fedha nyingi katika kufanikiwa kwake; fedha ambazo zitatoka katika mfuko wa serikali. Sasa pale wanapojitokeza watendaji wa serikali kurudisha nyuma juhudi kama hizo kwa kufanya udanganyifu kwa kweli hilo si jambo zuri na si jambo la kuvumiliwa.
Serikali inachukua bidii kutafuta meli kubwa ya kisasa au za kisasa kwa kuamini kwamba hatua kama hiyo ndiyo itakayotuwezesha kuwa na usafiri wa uhakika na kuepuka maafa ya baharini, kama yaliyotokea mwezi Julai mwaka huu kwa kuzama meli ya MV. Skagit katika eneo la Chumbe na Septemba mwaka jana, yalipotokea maafa kama hayo ilipozama meli ya MV. Spice Islander katika eneo la Nungwi.
Changamoto nyengine ya muda mrefu inayotukabili ni baadhi ya watendaji wetu kulalamikiwa kuviza kwa makusudi haki za wananchi. Hali hiyo imejitokeza zaidi katika suala la utoaji wa Vitambulisho vya Mzanzibari Mkaazi (ZANID).
Pamoja na ahadi na kauli mbali mbali za watendaji na viongozi kuahidi kila mwananchi aliyefikia umri wa miaka 18 na mwenye sifa zote za kupata kitambulisho hicho kuwa atapatiwa, bado malakamiko ni mengi katika jamii kuwa kuna watu wananyimwa haki hiyo kwa makusudi kabisa.
Serikali inajitahidi kutafuta ufumbuzi wa haraka changamoto hii kwa kutambua kuwa vitambulisho hivyo ndio utambuzi wa Wazanzibari Wakaazi na vinahusika moja kwa moja katika upatikanaji wa huduma na haki mbali mbali za msingi.
Kuwa na kitambulisho hicho ni jambo la lazima la kisheria na kwamba kumkosesha mtu au mtu kushindwa kuwa nacho ni kosa ambalo mhusika anaweza kuhukumiwa kifungo na faini. Na kwa umuhimu huo huo, napenda kuwanasihi wananchi ambao vitambulisho vyao viko tayari, lakini bado wamekuwa na ajizi kwenda kuvichukua wakavichukue haraka.
Kwa upande mwengine kutokana na umuhimu wa kitambulisho hicho na kwa kuwa kimehusishwa moja kwa moja katika upatikanaji wa huduma na haki za msingi, kumejitokeza mahitaji makubwa ya watu kuvitafuta na hata wasiohusika, yaani baadhi ya wageni wanavitafuta kwa udi na uvumba.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduizi Mhe. Dk. Ali Mohammed Shein kwa kuendelea kuwasisitiza wahusika wanaolalamikiwa kuwanyima wananchi vitambulisho hivyo kuacha tabia hiyo. Kwa mara ya mwisho Rais Shein alitoa wito wiki iliyopita kule Pemba wakati wa semina maalum kwa watendaji wa Serikali za mitaa. Ni imani yangu kwamba watendaji na viongozi wa serikali za Mitaa, Wilaya na Afisi ya Msajili wa Vitambulisho, watatii agizo hilo la Rais.
Waheshimiwa Waandishi wa Habari
Nimelazimika kulizungumza kwa kirefu kidogo suala hili la vitambulisho vya Ukaazi kutokana na umuhimu wake kwa wananchi. Lakini pia tumeona namna baadhi ya watu na vikundi wanavyoweza kutumia udhaifu wa utoaji vitambulisho hivyo kuuhusisha na masuala mengine muhimu ya Kitaifa.
Tumeona wakati wa zoezi la Sensa ya Kuhesabu watu na Makaazi hivi karibuni, baadhi ya watu walivyo tumia udhaifu wa utoaji vitambulisho hivyo kukaidi amri ya kuhesabiwa. Wamefanya hivyo, licha ya kuwa jambo la kuhesabiwa lina umuhimu wa kipekee katika maendeleo na ustawi wa wananchi. Hivyo basi ni vyema hatua zichukuliwe kila mwenye haki ya kitambulisho hicho asiwekewe kikwazo chochote, ili kuziba mianya kama hiyo inayotumiwa na baadhi ya watu kurejesha nyuma maendeleo na umoja wetu.
Waheshimiwa Waandishi
Jambo jengine ambalo napenda kuwahimiza tena wananchi, ni juu ya umuhimu wa kushiriki kutoa maoni yao kuhusu mabadiliko ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Tume ya Mabadiliko ya Katiba inayoendelea kufanya shughuli za kuratibu maoni ya wananchi nchi nzima tayari imefanya kazi hiyo katika mikoa ya Kusini Unguja na Kusini Pemba kwa hapa Zanzibar. Na katika mikoa hiyo wananchi waliweza kujitokeza vizuri kutoa maoni yao.
Nawasihi wananchi wote wa mikoa ya Kaskazini Unguja, Kaskazini Pemba na Mjini Magharibi wajitokeze kwa wingi kwenda kutoa maoni yao, wakati tume hiyo itakapofika katika maeneo yao. Hatua hiyo ndiyo itakayotuwezesha kupata Katiba tunayoitaka yenye maslahi kwa Zanzibar.
Hii ni fursa adhimu ambayo tumekuwa tukiililia kwa siku nyingi juu ya haja ya Watanzania kupata fursa ya kutoa maoni yetu, juu ya masuala yote yanayohusiana na Muungano. Wananchi wawe huru kutoa maoni yao kwa uwazi na pawepo na uvumilivu. Hata kama mtu hakubaliani na maoni, hoja zinazotolewa na mwengine, inabidi asikilize kwa uvumilivu. Naye akipata fursa aseme yake kwa uwazi pia.
Na mwisho wa yote hayo, ni kama ambavyo tunatarajia, maoni ya wengi ndiyo yatakayo heshimiwe baada ya wale wachache kupewa haki yao ya kusikilizwa kwa kikamilifu. Na sisi viongozi tunawajibu wa kusimamia hilo.
Waheshimiwa Waandishi wa Habari
Sasa naona tugusie masuala ambayo imekabidhiwa Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais.
Kama ambavyo mnafahamu ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais pamoja na mambo mengine, imekabidhiwa majukumu mazito, majukumu ambayo kwa lugha ya siku hizi yanaitwa Masuala Mtambuka (Cross Cutting issues), yakiwemo; Masuala yanayohusu Watu Wenye Ulemavu, Mapambano dhidi ya Madawa ya Kulevya, Uhifadhi wa Mazingira pamoja na Ugonjwa wa Ukimwi.
Waheshimiwa Waandishi wa Habari
Katika suala la mapambano dhidi ya UKIMWI, Wazanzibari tunapaswa sote tufahamu kuwa ukimwi bado upo na unaendelea kuwaathiri watu wetu. UKIMWI ni tatizo linalotugusa sote, wanawake, wanaume, vijana na watoto na ni janga ambalo linasababisha matatizo makubwa katika ngazi za familia hadi serikali.
Serikali kwa ushirikiano na wadau mbali mbali inachukua hatua kubwa katika kuweka mazingira mazuri ya kupiga vita janga hili, lakini bado kuna maambukizi mapya ya UKIMWI yanatokea.
Pia wale walioathiriwa na maambukizi bado wanakabiliwa na vikwazo vingi, ikiwemo kunyanyapaliwa na baadhi ya wanajamii. Aidha wanakumbana na hali ya umasikini na uhaba wa dawa na huduma nyengine wanazozihitaji.
Kiwango cha maambukizi ya ukimwi miongoni mwa watu wenye umri wa miaka 15 hadi 49 kimeendelea kusimama kwenye 0.6, ikiwa ni sawa na watu 7,200 wanaokadiriwa kuishi na virusi vya UKIMWI. Visiwani humu hali ya maambukizi ni mbaya zaidi kwa watu wa makundi maalum, ambayo inakadiriwa kupita kiwango kilichopo katika jamii nzima.
Kwa Zanzibar makundi maalum yanajumuisha; Watu wanaojidunga sindano za madawa ya kulevya, Wanawake wanaouza miili yao, Wanafunzi katika vyuo vya Mafunzo na Wanaume wanaofanya mapenzi ya jinsia moja.
Hata hivyo, tafiti mbali mbali ndogo ndogo hivi sasa zinaendelea, ili kujua hali halisi ya maambukizi ya UKIMWI Zanzibar, pamoja na mwenendo mzima wa maradhi hayo na kuweza kuandaa mikakati thabiti kwa mujibu wa hali ilivyo katika kudhibiti maambukizi mapya, na kuwasaidia wale ambao tayari wameambukizwa.
Aidha, Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais imeweza kufuatilia na kutathmini program mbali mbali za UKIMWI. Mwaka jana jumla ya vikundi 24 vyenye miradi 36 ya kujiongezea kipato vilifuatiliwa. Jumla ya shilingi milioni 15 kwa mfano walipatiwa jumuiya ya ZAPHA+ kwa ajili ya kutekeleza shughuli zao mbali mbali zinazolenga utekelezaji wa Mkakati wa Pili wa Taifa wa UKIMWI Zanzibar.
Waheshimiwa Waandishi wa Habari
Nadhani bado mnakumbuka Disemba Mosi mwaka jana tulizindua Mkakati wa Pili wa Taifa wa UKIMWI wa Zanzibar. Mkakati huo umeandaliwa maalum kuongoza muitikio wa kitaifa wa mapambano dhidi ya ukimwi kwa mwaka 2011/2016. Lengo kuu ni kuzuia kuenea maambukizi ya virusi vya UKIMWI miongoni mwa Wazanzibari, kukabiliana na athari mbaya za kiafya, ustawi na za kiuchumi zinazompata mtu mmoja mmoja , familia zao, makundi maalum na Taifa kwa jumla.
Aidha, Sera ya Taifa ya UKIMWI ya 2005 imejenga msingi mzuri wa kufanikisha mapambano dhidi ya ukimwi. Sera hiyo imeweka mfumo wa utawala wa kisheria kwa ajili ya mipango na harakati zote zitakazofanywa, ikiwemo kuzuia maambukizi mapya, kutibu, kutunza na kuwasaidia walioambukizwa pamoja na kuimarisha uwezo wa taasisi katika kutayarisha na kutekeleza program za ukimwi kwa kuzingatia jinsia na haki za binaadamu wote.
Katika kufanikisha mapambano dhidi ya UKIMWI Zanzibar tunaendelea kutoa wito kwa jamii, wakiwemo wazazi na viongozi wa kidini waendelee kutoa nasaha na kuwakataza vijana wetu na jamii kwa jumla, kuepuka matendo ambayo yatasababisha watu kuambukizwa virusi vya UKIMWI.
Vijana katika umri wao huiona dunia kama mahali pa uwezekano usiomalizika. Vijana waliopewa miongozo na malezi mazuri ndio wenye mwelekeo mzuri wa kusalimika na matatizo kama haya. Familia hazina budi kuwapa mawaidha vijana wao wa kike na kiume tena kwa uwazi mkubwa kabisa juu ya ukimwi, ili wajiepushe.
Waheshimiwa Waandishi wa Habari
Kuhusu Masuala ya Watu Wenye Ulemavu, katika jamii ya Wazanzibari kama zilivyo jamii nyengine, miongoni mwetu kuna Watu Wenye Ulemavu. Aidha, katika harakati za kimaisha za siku hadi siku kuna sababu tafauti zinazopelekea idadi ya watu wenye ulemavu kuongezeka. Kutokana na ukweli huo pamoja na wajibu wetu wa kibinaadamu, hatuna budi kuwa na mipango na mikakati imara ya kuwasaidia watu wenye ulemavu. Kujitolea kwetu kuwasaidia watu wenye ulemavu ndipo tutawawezesha wenzetu hawa kuishi kwa furaha na kuondokana na vikwazo vingi vinavyowakabili hivi sasa.
Watu wenye ulemavu wana haki sawa na watu wengine katika jamii. Wenzetu hawa wana kila haki ya kushirikishwa katika mipango yote ya kimaendeleo, pamoja na huduma za kijamii. Lakini kwa bahati mbaya sana hadi sasa watu wenye ulemavu wana kilio kikubwa cha kutopatiwa haki zao stahiki ipasavyo, pia wana malalamiko mengi ya kunyanyaswa na kudhalilishwa ikiwemo kijinsia.
Lakini pia katika jamii zetu tunaona ni namna gani hata mwamko juu ya watu wenye ulemavu ulivyo mdogo. Hadi leo kuna watu bado wanawaficha watoto na ndugu zao kwa sababu tu wana ulemavu. Kutokana na hali hiyo ndio maana tukaamua kuanzisha zoezi la makusudi kabisa kushajiisha jamii kuwafichua na kuwasajili watu wenye ulemavu.
Katika zoezi hilo linaloendelea ambalo lilitanguliwa na mafunzo kwa Masheha na wakusanyaji taarifa, tumeweza kusajili jumla ya watu 6,445 wenye ulemavu katika mikoa yote miwili kisiwani Pemba. Awali zoezi hilo lilifanyika kwa majaribio katika Mkoa wa Kaskazini Unguja, ambako jumla ya watu wenye ulemavu 3,002 walisajiliwa.
Aidha, katika kukuza na kuendeleza mwamko juu ya masuala ya watu wenye ulemavu, Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais imefanya kazi kubwa kuhakikisha masuala ya watu wenye ulemavu yanaingizwa katika mipango ya taasisi za za Serikali. Hadi sasa ofisi imeweza kusimamia uanzishwaji wa mpango huo na Maafisa Waratibu 16 tayari wapo katika wizara mbali mbali kwa ajili ya hatua hizo na tayari wamepatiwa mafunzo maalum.
Kwa upande mwengine, Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais imehakikisha inajenga uwezo kwa Idara ya Watu wenye Ulemavu pamoja na Baraza la Watu Wenye Ulemavu Zanzibar, kwa kununua vifaa vya ofisini pamoja na vifaa vya utendaji kwa wafanyakazi wake. Vile vile jumuiya tisa za Watu wenye Ulemavu zimeweza kupatiwa ruzuku pamoja na visaidizi, yaani viti vyenye magurudumu mawili kwa watu 31 Unguja na Pemba, ili kuwasaidia katika harakati zao za kimaisha.
Waheshimiwa Waandishi wa Habari
Wajibu wetu kwa watu wenye ulemavu ni mkubwa, lakini wakati ukweli ndio huo uwezo na nyenzo zetu hazitoshi kuweza kuwajengea uwezo kikamilifu kwa mujibu wa mahitaji yao. Lakini kwa kuthamini maisha na maendeleo yao, haki, fursa na usawa kwa watu wenye ulemavu, wajibu wetu wa kuwawezesha kukabilina na umasikini uliokithiri na upatikanaji mdogo wa huduma za afya tumeona kuna haja kuanzisha Mfuko wa Maendeleo ya Watu Wenye Ulemavu.
Mfuko wa Maendeleo ya Watu wenye Ulemavu Zanzibar umeanzishwa kama Sheria No. 9 ya mwaka 2006 inavyoagiza. Kama ambavyo waandishi wa habari ni mashihidi, Mfuko huo tayari umezinduliwa rasmi wiki iliyopita na Mheshimiwa Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohammed na kwakweli naona fahari kusema tumeanza vizuri.
Tunawashukuru mwananchi mmoja mmoja, mashirika, jumuiya, taasisi za kiserikali na watu binafsi, kwa namna walivyojitokeza na kuonesha moyo wao wa dhati kuwasaidia watu wenye ulemavu Zanzibar. Moyo wao huo umewezesha mfuko huo kuanza na kiasi cha T.SHS milioni 285. Tunaendeela kukuhimizeni wananchi na taasisi mbali mbali kuendelea kuchangia mfuko huu kwani uchangiaji wa mfuko unaendelea.
Matumaini yetu Mfuko huu utaweza kutoa mchango mkubwa kusaidia utatuzi wa changamoto nyingi ambazo baadhi tumesha zianisha.
Waheshimiwa Waandishi wa Habari
Kwa upande wa Madawa ya Kulevya, Suala hili pia ni changamoto nyengine kubwa inayotukabali katika nchi yetu. Na ukweli ni kwamba tatizo hili sio tu kwa Zanzibar, bali kwa Dunia nzima. Kutokana na ukubwa wa tatizo la madawa ya kulevya mataifa yanaungana kupambana na wazalishaji, wafanyabiashara na walanguzi wa madawa haya ambao nao wamejidhatiti vilivyo. Katika baadhi ya nchi tunashuhudia hata nguvu za kijeshi zikitumika kukabiliana na tatizo hili.
Athari za madawa ya kulevya zipo wazi na Zanzibar tunashuhudia hilo. Maisha ya watu wetu hasa vijana ambao ndio nguvu kazi ya Taifa yamekuwa hatarini. Lakini kwa upande mwengine madawa ya kulevya yamekuwa chanzo kikuu cha maambukizi ya maradhi ya ukimwi, ambayo nayo yanachukua nafasi kubwa kuteketeza maisha ya binaadamu na kudhorotesha uchumi wa nchi.
Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais imekuwa ikifanya kazi kubwa ya kuratibu na kudhibiti utumiaji, biashara na usafirishaji wa madawa hayo. Kazi hizo zimekuwa zikifanywa kwa karibu na wananchi pamoja na wadau mbali mbali katika mapambano dhidi ya madawa ya kulevya, vikiwemo vyombo vya ulinzi na usalama, azma yetu ikiwa ni kuinusuru Zanzibar kuwa kituo cha madawa ya kulevya na wananchi wake kuathirika na madawa hayo.
Mikakati yetu juu ya jambo hili imelenga zaidi kuwa na sheria zinazokwenda na wakati ambazo zinakidhi haja ya kudhibiti madawa ya kulevya kwa wakati uliopo.
Katika utekelezaji wa hatua hiyo tayari sheria Nam. 9 ya mwaka 2009 ilipitiwa na wadau mbali mbali na baadaye kuwasilishwa katika kikao cha Baraza la Wawakilishi na kurekebishwa. Aidha, uandaaji wa Sera ya Madawa ya Kulevya Zanzibar inaendelea na hivi sasa kazi za kukusanya maoni ya wadau inafanyika.
Waheshimiwa Waandishi wa Habari
Juhudi kubwa katika kudhibiti madawa ya kulevya Zanzibar tumezielekeza katika kutoa taaluma kwa jamii juu ya madhara yake, lakini pia kuwasaidia vijana walioingia kwenye matumizi ya madawa haya, kwa kuwanasihi waache, pamoja na kuwashauri na kuwasaidia njia zitakazowawezesha kupata kazi za kujiongezea vipato na kuondokana na tabia ya kukaa bila ya kazi, tabia ambayo huwapa msongo wa mawazo na kuwafanya waendelee kutumia madawa hayo.
Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais katika mwaka wa fedha uliomalizika, iliweza kutoa ushauri nasaha kwa familia 984 za watumiaji wa madawa ya kulevya, wakiwemo wanawake 510 na wanaume 474, ambapo kati yao, 97 walikuwa watumiaji wa madawa ya kulevya.
Aidha, ahadi ya kuzisaidia angalau fedha kidogo taasisi zinazotoa huduma za makaazi ya vijana wanaoacha kutumia madawa ya kulevya (Sober Houses) ilitekelezwa na shilingi 9,900,000 zilitolewa, pamoja na televisheni na redio Unguja na Pemba.
Rasimu ya muongozo wa nyumba za marekebisho za makaazi ya vijana wanaoacha matumizi ya madawa hayo imekamilika. Aidha, suala la taaluma kwa jamii juu ya kupiga vita madawa ya kulevya limeendelea kupewa umuhimu wa kipekee kwa kuandaa vipindi mbali mbali vilivyoweza kurushwa hewani kupitia televisheni na redio. Vile vile Shehia mbali mbali zilifanyiwa ziara za uhamasishaji na taaluma juu ya athari za madawa hayo Unguja na Pemba.
Waheshimiwa Waandishi wa Habari
Kuhusu suala la Kuyahifadhi na kuyalinda mazingira yetu, pia hili nalo ni muhimu katika kudumisha Uhai na Ustawi wa nchi yoyote ile. Hata hivyo changamoto inayojitokeza katika nchi nyingi, ikiwemo Zanzibar ni uharibifu na uchafuzi mkubwa na wa makusudi wa mazingira yetu. Kasi tunayoishuhudia ya ukataji ovyo wa misitu na uchimbaji wa mchanga na mawe, kwa ajili ya kutengeneza matofali ni ya kutisha na iwapo haitadhibitiwa nchi yetu ya Zanzibar kipindi kifupi kijacho itakabiliwa na janga kubwa la kimazingira.
Aidha, upoteaji wa bioanuwai za nchi kavu na baharini kwa jumla, utupaji ovyo wa taka na maji machafu, uvunaji usioridhisha wa maliasili zisizojirejesha, hali inayosababisha kuachwa kwa mashimo mengi, pamoja na ile tabia ya kuingizwa kwa wingi nchini vifaa chakavu vya elektroniki, umeme na mifuko ya plastiki inaongeza ukubwa wa hatari hiyo ya kimazingira.
Kwa upande mwengine suala la mabadiliko ya tabianchi limekuwa ni tishio kubwa kwa dunia, na nchi zinazoathirika zaidi ni zile za visiwa vidogo kama vyetu vya Zanzibar. Hali inayojitokeza katika baadhi ya maeneo ya visiwa vyetu ambako maji ya bahari yamevamia mashamba ya kilimo cha mpunga inatosha kuwa onyo kali kwetu na kufanya kila linalowezekana kuyalinda mazingira.
Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais katika kukabiliana na changamoto hizo za kimazingira, ikiwemo suala la athari za mabadiliko ya tabianchi bado inaamini utoaji wa elimu na kuzidi kukumbushana ndio njia muafaka na yenye umuhimu wa kipekee.
Hata hivyo hatua za kisheria zimeendelea na zitaendelea kuchukuliwa kwa wananchi au miradi ya kiuchumi ambayo inaonekana kwa makusudi kupinga au kudharau sheria na kanuni za uhifadhi wa mazingira.
Waheshimiwa Waandishi wa Habari
Miongozi mwa hatua zinazoendelea kuchukuliwa ni kutoa taaluma kwa njia ya semina, vipindi vya televisheni na redio, pamoja na kuandaa ziara za kimasomo katika maeneo mbali mbali, ili wananchi, viongozi wa maeneo na wanachama wa jumuiya zisizokuwa za kiserikali, waweze kujifunza na baadaye kusaidia jamii kukumbusha na kuhamasisha suala zima la kulinda, kutunza na kuhifadhi mazingira ya nchi yetu.
Hatua hizo zinajumuisha mafunzo juu ya mabadiliko ya Tabianchi na mwelekeo wa Zanzibar katika kusimamia jambo hilo, yalitolewa kwa Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi. Aidha wafanyakazi 12 kutoka Idara ya Mazingira, Baraza la Manispaa Zanzibar, Halmashauri za Wilaya ya Magharibi na Mabaraza ya Miji ya Chake Chake, Mkoani na Wete na baadhi ya wawakilishi wa Jumuiya zisizokuwa za kiserikali waliwezeshwa kufanya ziara za kujifunza huko Moshi na Arusha, ili waweze kupata uzoefu juu ya usimamizi wa taka.
Ziara za kujifunza za aina hii, pia ziliwahusisha viongozi 10 wa Kamati za Machimbo ya Uwandani waliokwenda Mjini Mombasa Kenya kujifunza njia bora za shughuli za uchimbaji na urejeshwaji wa maeneo yaliyochimbwa na kuepusha athari za kimazingira.
Hatua hizo zilichukuliwa kwa makusudi, ili kudhibiti kasi ya uchafuzi wa maeneo na kuyaweka katika hali ya usafi, pamoja na kudhibiti athari za uchimbaji mawe kwa ajili ya kazi za uchongaji matofali, maeneo ambayo yanahatarisha sana hali ya mazingira hapa Zanzibar.
Eneo jengine ambalo linaonekana ni sugu katika uharibifu wa mazingira yetu ni kwenye fukwe na miradi ya hoteli za kitalii. Katika siku za hivi karibuni miradi 110 ya kitalii ilifanyiwa ufuatiliaji kuona inavyozingatia masuala ya kimazingira. Taarifa ya ufuatiliaji huo si ya kufurahisha kwa sababu kati ya miradi mingi ambayo ilionekana kukiuka kanuni ya kudhibiti matumizi ya ardhi kwa ajili ya uwekezaji ya mwaka 2006.
Miradi hiyo ilitakiwa kubomoa sehemu zilizojengwa kinyume na kanuni, lakini ni mradi mmoja tu wa hoteli ya Zanzibar Ocean View ambao umetii amri hiyo.
Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais ilichukua hatua ya kuwasilisha majina ya miradi hiyo iliyoshindwa kufuata agizo hilo, Idara ya Mipango Miji na Vijiji kwa ajili ya hatua za kisheria kwa mujibu wa kanuni.
Hata hivyo, lazima tukiri kwamba ipo haja kubwa ya kuimarishwa Sheria na kanuni zetu za Mazingira, ili ziweze kukidhi haja kwa mujibu wa wakati.
Kuhusu usimamizi wa marufuku ya mifuko ya plastiki, baada ya Kanuni kufanyiwa marekebisho, mafanikio makubwa yameweza kupatikana ambapo hadi unakamilika mwaka wa fedha uliopita, watu 192 walikamatwa na kushitakiwa mahakamani na jumla ya shilingi 7,650,000 zilizotokana na faini ziliingia katika mfuko wa serikali.
Ni dhahiri changamoto ya kimazingira ni kubwa, hivyo ni jukumu la kila mmoja wetu kutekeleza wajibu wake wa kulinda na kuyahifadhi Mazingira yetu ambayo ni muhimu kwa maendeleo ya kijamii na kiuchumi kwa kizazi cha sasa na kijacho.
Waheshimiwa Waandishi wa Habari
Baada ya kusema hayo natanguliza shukurani zangu nyingi, kwa viongozi na watendaji wa Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais, akiwemo Waziri wangu wa Nchi mchapakazi na muadilifu, Mheshimiwa Fatma Abdulhabib Fereji.
Vile vile shukurani hizo ziende kwa Katibu Mkuu makini mwenye uzoefu na ujuzi wa taratibu za serikali ambaye ndiye anayenishauri mimi na Waziri wa Nchi kuhusu masuala ya kitaalamu, mbali kuwa Mtendaji Mkuu wa shughuli zote zilizochini ya ofisi hii. Huyo ni Dk. Omar Shajak akisaidiwa na Naibu Katibu Mkuu, Dk. Islam Seif Salum, pamoja na Wakurugenzi na Watendaji Wakuu wa Kamisheni zilizo chini ya ofisi hii. Wote hao nawashukuru kwa msaada mkubwa wanaoendelea kunipa kwa muda wote huu.
Ahsanteni sana.

TAMKO LA PAMOJA LA KONGAMANO LA KITAIFA

TAMKO LA PAMOJA LA KONGAMANO LA KITAIFA LA KUZUNGUMZIA NAFASI YA ZANZIBAR KATIKA MJADALA WA KATIBA MPYA, UKUMBI WA SALAMA, HOTELI YA BWAWANI, TAREHE 06 OKTOBA, 2012
Sisi washiriki wa Kongamano la Kitaifa la Wazanzibari tuliloliitisha kuzungumzia Nafasi ya Zanzibar katika Mjadala wa Katiba Mpya leo hii Jumamosi, tarehe 06 Oktoba, 2012 katika Ukumbi wa Salama, Hoteli ya Bwawani, mjini Zanzibar tunatambua kwamba fursa iliyopo mbele yetu katika Mjadala huu wa Kitaifa ni fursa adhimu ambayo inapaswa kukumbatiwa na kila Mzanzibari Mzalendo katika kuamua Mustakbali wa Zanzibar na watu wake.
Katika kuikumbatia fursa hii, tunatambua, kuheshimu na kuthamini hatua iliyofikiwa ambapo Wazanzibari kutoka makundi na taasisi tofauti wameungana na kuja pamoja katika kusimamia na kuendesha harakati zenye lengo la kuirejesha Zanzibar yenye mamlaka kamili kitaifa na kimataifa itakayofuatiwa na mashirikiano ya Muungano wa Mkataba kati yake na Tanganyika.
Hata hivyo, tunaelewa pia kuwa zimekuwepo jitihada za makusudi za kujaribu kuuvunja umoja huu wa Wazanzibari kwa kutumia hoja dhaifu zenye lengo la kutuondoa katika mstari ili kuzima vuguvugu la Wazanzibari.
Hatua ya leo ya kuwa na wasemaji na washiriki kutoka makundi na taasisi tofauti ni kudhihirisha kwamba njama za kutugawa tutazishinda kwa njia za amani na za kidemokrasia.
Kutokana na hali hiyo, ndiyo leo hii tumeamua sisi Wazanzibari tunaotoka makundi na taasisi tofauti lakini tunaounganishwa na UZANZIBARi na imani yetu kwamba wakati umefika wa ZANZIBAR kurejesha mamlaka kamili kitaifa na kimataifa, kutoa tamko LIFUATALO.
KWAMBA umoja wetu ndiyo nguvu yetu na ngao yetu, hivyo tumeamua kuunganisha nguvu zetu katika kusimamia madai halali ya Wazanzibari na kwamba tunakataa njama zote za kutaka kutugawa ili kuendeleza mipango ya wasioitakia mema Zanzibar ya kutaka kuendelea kuidhibiti.
KWAMBA tutaendeleza harakati hizi za Wazanzibari kwa njia za amani na za kidemokrasia.
KWAMBA hatutositisha harakati zetu za amani na kidemokrasia hadi lengo la ZANZIBAR yenye mamlaka kamili kitaifa na kimataifa litimie, na kwamba juhudi zozote za kutaka kubadilisha matakwa ya Wazanzibari kwa kuwakisia na kuwakadiria cha kuwapa hazitokubalika. Tunachokisimamia ni HAKI yetu na si OMBI au fadhila kutoka kwa yoyote.
KWAMBA tuna imani na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar yenye muundo wa Umoja wa Kitaifa chini ya Raisi Muheshimiwa Dk. Ali Mohammed Shein na pia tunaimani na viongozi wetu. Na tunaamini Serikali yetu na viongozi wetu hao ni wazalendo wa Zanzibar na kwamba ridhaa yao imetoka kwa wananchi wa Zanzibar. Hivyo basi, tunaamini na kuwategemea kuwa kama wanavyoendelea kutuahidi watasimamia na kutetea matakwa na maamuzi ya Wazanzibari walio wengi.
KWAMBA tunatoa wito kwa Jumuiya ya kimataifa kufuatilia kwa kina mchakato wa katiba mpya na kufuatilia matakwa ya Wazanzibari wanayoyatoa katika mijadala mbali mbali inayoendelea. Tunaitegemea jumuiya ya kimataifa hatimae iunge mkono matakwa ya Wazanzibari yanayotolewa kwa njia ya amani na kidemokrasia.
KWAMBA Zanzibar tunayotaka kuiona ni Zanzibar itakayojengwa chini ya misingi YA UHURU, USAWA, DEMOKRASIA, UVUMILIVU, HAKI ZA BINAADAMU, AMANI NA UJIRANI MWEMA, NA YENYE MAISHA YA NEEMA KWA WATU WAKE WOTE.
ZANZIBAR KWANZA
Limetolewa leo
Tarehe 06 oktoba 2012
ZANZIBAR.

Friday 5 October 2012

Jussa atangaza kujiondoa uongozi wa juu CUF

Salma Said, Zanzibar na Elias Msuya
NAIBU Katibu Mkuu wa Chama Cha Wananchi (CUF) Zanzibar, Ismail Jussa Ladhu jana amemuandikia barua rasmi Mwenyekiti wa chama hicho, Profesa Ibrahim Lipumba kutaka kujiuzulu wadhifa wake huo chamani.
Kwa mujibu wa barua hiyo ya Oktoba 5 mwaka huu iliyosambazwa kwa vyombo vya habari nchini iliyotiwa saini na yeye mwenyewe, Jussa amesema amemuomba mwenyekiti wake kuwa utekelezaji wa maamuzi ya kujiuzulu uanze kutekelezwa rasmi Oktoba 10, 2012.
“Nimechukua uamuzi huu baada ya kuzungumza na kushauriana na viongozi wangu wa juu wa Chama ambao ni Mwenyekiti, Profesa Lipumba, Makamu Mwenyekiti Mheshimiwa Machano Khamis Ali na Katibu Mkuu Maalim Seif Sharif Hamad takriban miezi miwili iliyopita. Nawashukuru baada ya kunitaka niwape muda wa kulitafakari walinikubalia lakini wakaniomba nibakie hadi tutakapokamilisha baadhi ya shughuli muhimu za Chama katika kipindi hichi,” alieleza.
Akitaja sababu za kutaka kujiuzulu, Jussa alisema, “Sababu kubwa zilizonisukuma kukiomba Chama kiniruhusu niachie nafasi hii ni kwa kuwa muda mrefu sasa kuhisi kwamba majukumu niliyo nayo ya kuwa msimamizi mkuu wa utendaji wa Chama kwa upande wa Zanzibar na wakati huo huo kuwa Mjumbe wa Baraza la Wawakilishi wa jimbo la Mji Mkongwe hakunipi fursa ya kujifaragua na kutumikia nafasi zote mbili kwa ufanisi unaotakiwa,” alisema Jussa.
Hata hivyo alkizungumzana Mwananchi kwa njia ya simu Jussa alisema kuwa lengo la kujiuzulu ni kupata nafasi zaidi ya kushiriki kwenye operesheni hizo kwani kuwa katika cheo hicho kunamnyima nafasi hiyo.
“Lengo langu ni kupatikana kwa mtu atakayekuwa ofisini wakati wote ili wengine washughulike na operesheni kama hizo. Kwa sababu katika chama chetu ukiwa naibu katibu mkuu unakuwa mtendaji wa chama kwa wakati wote. Lakini mimi kwa shughuli za majukwaani au kwenye operehseni nitakuwepo wakati wote.
Aidha Jussa alisema, “Nataka kuona kazi ya kuibana Serikali ndani na nje ya Baraza ili iwajibike zaidi kwa wananchi inaimarika zaidi.”
Sababu nyengine ya kutaka kujiuzulu Jussa alisema, “Nimekusudia kutumia muda mwingi zaidi kutoa mchango mkubwa zaidi katika harakati za wananchi wa Zanzibar zinazoendelea za kuhakikisha kuwa Zanzibar inarejesha mamlaka yake kamili kitaifa na kimataifa itakayofuatiwa na kuwepo kwa Muungano wa Mkataba kati yake na Tanganyika yenye mamlaka kamili kitaifa na kimataifa.”
Alisema harakati zinazoendelea hivi sasa Zanzibar kwa njia za amani na za kidemokrasia kwa kutumia mchakato wa Katiba Mpya zinahitaji kuungwa mkono na kupewa msukumo wa dhati na Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi waliochaguliwa na wananchi wa Zanzibar.
Naibu Katibu Mkuu huyo alisema lengo lao kama wawakilishi ni kwenda kusimamia maslahi ya wananchi ndani ya vikao vya Baraza la Wawakilishi hivyo baada ya kutafakari kwa kina ameona ni vyema akiachia ngazi ili apate muda mzuri wa kufanya kazi hiyo ya kuwasaidia wananchi wa Zanzibar.
Jussa ambaye ni Mwakilishi wa Jimbo la Mji Mkongwe ambaye kwa kiasi fulani amekuwa akitoa changamoto kubwa kwa Serikali katika uwajibikaji tokea kuingia kwake katika chombo cha kutunga sheria, ametetea uamuzi wake huo kwa kusema, “Nikiwa sina majukumu mengine ya kiutendaji nitakuwa na muda kutosha wa kulifanya hili mimi na Wawakilishi wenzangu tunaotoka CUF na CCM, vyama viwili vya siasa vilivyomo Barazani”.
Wakati huo huo, leo kumeandaliwa kongamano kubwa la kitaifa ambalo pamoja na mambo mengine linatuzungumzia mchakato wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania unaoendelea nchini na kutoa fursa ya wananchi mbalimbali kushiriki na kutoa mawazo yao katika kongamano hilo ambalo limetayarishwa na kamati ya maridhiano ambayo Jussa ni mjumbe.
Kwa mujibu wa taarifa iliyosambazwa kwa vyombo vya habari na kutiwa saini na Mwenyekiti wa Kamati ya Maridhiano Zanzibar, Mzee Hassan Nassor Moyo alisema kongamano hilo litakalofanyika katika ukumbi wa Salama Bwawani litatoa fursa ya wazanzibari kutoa maoni yao juu ya mustakabali wa nchi yao ndani ya Muungano.
Mwenyekiti wa kongamano hilo litakalowashirikisha watu mashuhuri, wasomi na wanasiasa wa vyama mbalimbali ni Professa Abdul Shareef huku wazungumzaji ni pamoja na aliyekuwa Katibu wa mwanzo wa Baraza la Mapinduzi Zanzibar, Salum Rashid, Mzee Hassan Nassor Moyo, Mwanasheria Mkuu Othman Masoud Othman, Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) Ibrahim Mzee.
Wengine ambao wamepangiwa kuzungumza katika kongamano hilo ni Amiri Mkuu wa Jumuiya ya Uamsho na Mihadhara ya Kiislamu Zanzibar (Jumiki) Sheikh Msellem Ali Msellem, Waziri asiye na Wizara Maalum na Mwakilishi wa Kiembe Samaki Mansoor Yussuf Himid, Mwenyekiti wa ZAHILFE Ndugu Kassim Hamad Nassor, Mwenyekiti wa Vijana wa Umoja wa Kitaifa Ndugu Khaleed Said, Rais wa Zanzibar Law Society (ZLS) Salim Toufiq.
Jussa ni miongoni mwa wanasiasa na viongozi waliojitokeza hadharani ya kuonesha msimamo wa kutaka Zanzibar yenye mamlaka kamili ndani ya Muungano huku wakitaka suala la Muungano wa Mkataba badala ya Muungano wa katiba kama ulivyo sasa.
Jusa
Jussa ameongeza kuwa anataka kutumia muda mwingi zaidi kutoa mchango mkubwa katika harakati za wananchi wa Zanzibar zinazoendelea za kuhakikisha kuwa Zanzibar inarejesha mamlaka yake kamili kitaifa na kimataifa itakayofuatiwa na kuwepo kwa Muungano wa Mkataba kati yake na Tanganyika yenye mamlaka kamili kitaifa na kimataifa.
“Harakati zinazoendelea Zanzibar kwa njia za amani na za kidemokrasia kwa kutumia mchakato wa Katiba Mpya zinahitaji kuungwa mkono na kupewa msukumo wa dhati na Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi waliochaguliwa na wananchi wa Zanzibar kwenda kusimamia maslahi yao na ya nchi yao. Nimetafakari na kuona kwamba nikiwa sina majukumu mengine ya kiutendaji nitakuwa na muda kutosha wa kulifanya hili mimi na Wawakilishi wenzangu tunaotoka CUF na CCM, vyama viwili vya siasa vilivyomo Barazani,” alisema.
Vuguvugu hilo la kudai Zanzibar huru linaungwa mkono baadhi ya viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar huku watu wachache wakiwakataa kuunga mkono maamuzi ya wazanzibari wengi ambapo limeanza zamani lakini katika siku za hivi karibuni tokea kuanza kwa mchakato wa katiba limeubuka upya ambapo kwa kiasi kikubwa wazanzibari wamekuwa wakitumia muda wao mwishi kujadili suala hilo.
Kufuatilia kujiuzulu wadhifa wake huo Jussa kutampa nafasi ya kushughulikia suala zima la kuitetea Zanzibar ndani ya muungano katika kipindi hiki cha mchakato ukusanyaji wa maoni ya katiba lakini bado Jussa atabaki kuwa Mjumbe wa Baraza Kuu la Uongozi la Taifa na Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa Taifa katika chama.
Akiwatoa khofu wafuasi na viongozi wenzake wa chama katika uamuzi wake wa kujiuzulu Jussa alisema “Nawahakikishia viongozi na wanachama wenzangu wa CUF kwamba tutaendelea kushirikiana pamoja katika shughuli nyengine zote za kisiasa za Chama na kwa pamoja tutafanya kazi kuyatimiza malengo tuliyojiwekea. Naahidi kumpa ushirikiano kikamilifu mwanachama yeyote atakayeteuliwa kujaza nafasi ninayoiwacha” .
Jussa amekitumikia chama hicho kwa muda mrefu tokea kuanzishwa kwake wakati akiwa shule ya sekondari ambapo wakati wa ukusanyaji wa maoni ya kutaka kurejeshwa mfumo wa vyama vingi Jussa alikuwa ni kijana pekee katika Jimbo la Mji Mkongwe aliyesimama mwanzo na kutoa maoni yake akitaka kurejeshwa kwa mfumo wa vyama vingi.
Baadae Jussa alijiunga na CUF na kuanza kupanda ngazi moja baada ya nyengine akiwa karibu sana na Katibu Mkuu wa Chama hicho, Maalim Seif Sharif Hamad ambapo alishika nafasi mbali mbali ikiwemo ile maarufu ya Mkurugenzi wa mambo ya nje na ushirikiano na kimataifa ambayo kwa kiasi kikubwa ndio iliyompa umaarufu ndani na nje ya nchi kwa kuwasiliana moja kwa moja na mabalozi mbali mbali nchini.
Nafasi ya Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho Jussa amekabidhiwa tokea Disemba 2010 ambapo kabla ya hapo aliwahi kushika nafasi mbali mbali katika chama hicho.
Chanzo: Mwananchi

Dr Shein Apokea Waya Mpya wa Umeme

Dr Shein akikagua waya mpya wa umeme
 HATIMAE waya mpya wa umeme utakaolazwa baharini kutoka Ras Fumba Zanzibar hadi Ras Kiromoni Dar-es-Salaam umewasili Zanzibar na kupokewa rasmi pamoja na kukaguliwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein, huko katika bandari ya Malindi mjini Unguja. Waya huo utakaotumika katika mradi wa uwekaji wa waya wa pili wa umeme kutoka Ras-Fumba hadi Ras Kiromoni Dar-es-Salaam, shughuli zake za ulazaji zinatarajiwa kuanza siku ya Juamatatu majira ya asubuhi. Akitoa maelezo yake huku akionesha furaha kubwa Dk. Shein alitoa pongezi kwa Kampuni iliyotengeza waya huo pamoja na Wakandarasi waliotengeza waya huo alieleza kuwa licha ya kuwa kazi hiyo ni ngumu lakini imefanywa vizuri. Dk. Shein alisema kuwa kuja kwa waya huo kutapunguza usumbufu wanaoupata hivi sasa wananchi wa kupata umeme kwa mgao kwani waya huo utakuwa na umeme wenye megawati 100 ambazo zitatosheleza kwa kiasi kikubwa na nyengine kubakia.
Alisema kuwa matumizi ya umeme kwa kisiwa cha Unguja ni megawati 45 tu kwa hivi sasa lakini waya una megawati 100 ambazo zitasaidia kutoa huduma hiyo pamoja na kuweza kujipanga vizuri kwa shughuli nyengine za maendeleo hapo baadae. Aidha, Dk. Shein alisema kuwa waya huo ambao pia, utasaidia kutoa huduma nyengine za mawasiliano yakiwemo mtandao wa intaneti utawezesha kutoa huduma za e- Government pamoja na huduma za mkonga wa taifa kama ulivyo kwa waya uliolazwa kisiwani Pemba. Rais Dk. Shein anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika uzinduzi wa ulazaji wa waya huo katika hafla itakayofanyika siku ya Jumaatatu asubuhi. Akipata maelezo kutoka kwa jopo la wakandarasi wa waya huo Kampuni ya VISCAS, na mhandisi mdogo pamoja na Mhandisi Mshauri kutoka Kampuni ya ESB International pamoja na Msaidizi Mtendaji Mkuu wa MCA-T kwa upande wa Zanzibar Bwana Ahmed Rashid, walieleza kuwa shughuli hizo za ulazaji wa waya zitafanywa si zaidi ya siku 12 kwa kutumia meli na vifaa walivyonavyo kwa kushirikiana na meli nyengine. Walieleza kuwa waya huo wenye urefu wa kilomita 37 na uzito wa tani 2000, shughuli za ulazaji pamoja na zile za kuunganisha katika vituo maalum vilivyopo Mtoni na vile vya Dar-es-Salaam zinatarajiwa kumalizika na kutoa huduma ya umeme unatokana na waya huo mpya mnamo mwanzoni mwa mwezi wa Novemba. Aidha, uongozi wa MCA-T ulitoa shukurani kwa uongozi wa Mkoa wa Mjini Magharibi kwa mashirikiano makubwa ya mazungumzo na viongozi wa dini katika mchakato mzima wa kuvunjwa nyumba, madrasa na baadhi ya nyumba za ibada kwa lengo la kupitisha waya mpya wa umeme kutoka Fumba hadi Mtoni. Uongozi huo wa MCA-T pia ulieleza kuwa kuna hakiba ya waya upatao mita 450 ambao utawekwa katika kituo cha Mtoni kwa ajili ya dharura pale itakapohitajika na kusisitiza kuwa tayari nguzo maalum za ardhini zimeshawekwa katika baadhi ya sehemu. Walieleza kuwa waya huo mpya utalazwa sambamba na waya huu uliopo hivi sasa na kusisitiza kuwa shughuli hizo za ulazaji zinatarajiwa kuanza siku ya Jumatatu asubuhi. Nae Mkurugenzi wa Shirika la Umeme Bwana Hassan Ali Mbarouk alisema kuwa waya huo unauwezo wa kuishi zaidi ya miaka 30. Mradi wa waya huo wa umeme umenza miaka mine iliyopita ambao umetengenezwa na Kampuni ya VISCAS kutoka Japan ambao mbali ya kutengeneza pia, watakuwa na jukumu la ulazaji wa waya huo ambao utasimamiwa na Wahandisi washauri wa Kampuni ya ESB International kutoka Ireland. Mradi huo unafadhiliwa na Shirika la Changamoto la Milenia (MCC) kutoka Marekani. Baadhi ya wananchi ambao walikuwepo katika hafla hiyo fupi huko katika bandari ya Malindi mjini Unguja wakizungumza na mwandishi wa habari hizi walieleza kufarajika kwao na juhudi zinazochukuliwa na Serikali yao inayoongozwa na Dk. Shein katika kuwatatulia kero zao. Walieleza kuwa kukamilika kwa mradi huo kutasaidia kwa kiasi kikubwa kuongeza huduma za maendeleo kwa wananchi sambamba na kuimarisha sekta za maendeleo zikiwemo mawasiliano pamoja na sekta ya utalii ambayo ndio sekta inayoipatia fedha nyingi serikali.

CCM na changamoto za siasa za umoja

Barazani kwa Ahmed Rajab
KUNA zama ambapo Zanzibar ilikuwa haikugawika kisiasa. Bila ya shaka kulikuwa na matabaka ya kijamii na watu walikuwa na tofauti zao za kimaisha, lakini kwa jumla Wazanzibari wote wakijihisi kuwa ni watu wamoja, kitu kimoja.
Hizo zilikuwa nyakati kabla ya kuzuka kwa siasa za vyama vyama ambavyo baadhi yao vilitumiwa na watawala wa kikoloni wa Kingereza kuwagawa Wazanzibari.
Zama hizo, badala ya vyama vya kisiasa, Wazanzibari wakijishughulisha na vyama vingine kama vile vya densi, ngoma, muziki na michezo ikiwemo soka. Badala ya kuwako ushindani wa vyama vya kisiasa kulikuwako na ushindani wa vyama vya burdani.
Siku hizo Zanzibar ilikuwa ni nchi iliyojaa amani na utulivu. Si siasa wala si dini zilizowagawa Wazanzibari. Ndiyo pakazuka ule usemi wa ‘Zanzibar ni njema atakaye naaje.’ Nadhani hiyo hali ya amani, utulivu na umoja uliokuwapo ndiyo iliyosababisha Zanzibar ya siku hizo kubandikwa lakabu ya ‘Visiwa vya Peponi.’
Nakumbuka utotoni mwangu wakati timu ya soka ya Zanzibar ilipokuwa ikishiriki katika mechi za Afrika ya Mashariki kama zile za kuwania Kombe la Gossage, Wazanzibari wote walikuwa pamoja wakiishangiria timu yao ya taifa. Uzalendo waliokuwa nao ulikuwa wa hali ya juu.
Kwa bahati mbaya uzalendo huo ulitoweka Visiwani kwa muda wa takriban miaka 50 iliyopita. Uzalendo huo umeibuka tena hivi karibuni tu baada ya kuanza mchakato wa kuitunga upya Katiba ya Jamhuri ya Muungano ya Tanzania.
Kuna sababu kwa nini uzalendo huo ufufuke sasa. Na sababu yenyewe ni kwamba hili suala muhimu la katiba limewafanya Wazanzibari kwa jumla waamke na wawe tena wamoja, kitu kimoja, wakizicheza ‘Siasa za Umoja.’ Hizi ni siasa za kuwa na vuguvugu la umoja. Si siasa za vyama bali ni siasa zinazowaunganisha wazalendo walio wafuasi wa vyama vyote na hata wasio wafuasi wa vyama kwa lengo au malengo fulani.
Kile ambacho wengi wa Wazanzibari wanachokifanya wakati huu ni kuyapa kipaumbele maslahi ya kitaifa na kuyapa kisogo maslahi ya kichama. Ni wazi kuwa Wazanzibari hao wametanabahi kwamba cha kufikiriwa kwanza na cha kupewa uzito wakati wa kutoa maoni yao juu ya katiba mpya ni nchi yao na si chama cha kisiasa kinachotawala au cha upinzani. Cha kupiganiwa ni matilaba ya nchi na si sera za chama. Kwa hilo hawakwenda kombo wala hawajapoteza dira kwani mtu kuitakia kheri nchi yake ni sehemu ya imani ya mtu hata ya kidini.
Kuna sababu nyingine nzito zilizowafanya Wazanzibari wazikumbatie hizo Siasa za Umoja. Kwa kweli siasa za aina hiyo ndiyo dawa mujarab kwa jamii iliyokuwa imegawika kama ya Zanzibar na iliyokuwa na ugonjwa wa kisiasa kama iliokuwa nao hadi hivi karibuni.
Hii ni jamii ambayo kwa muda mrefu sana iligawika kisiasa nusu kwa nusu na hivyo kuwafanya Wazanzibari wasiweze kukubaliana kuhusu masuala nyeti yanayohusu mustakbali wao na wa vizazi vyao vijavyo.
Ule mzozano wa kisiasa baina ya vyama vya ZNP (Hizbu) na ASP uliopamba moto tangu 1957 hadi 1964 uliweza kuzimwa kwa kuanzishwa mfumo wa kuwa na chama kimoja tu cha kisiasa hatua ambayo iliikandamiza migawanyiko ya kisiasa.
Hata hivyo, mzozano huo ulifufuka uliporuhusiwa tena mfumo wa vyama vingi vya siasa na ulisababisha uhasama mkubwa na hata vifo vya kisiasa katika jamii. Mzozano na mgogoro huo wa kisiasa uliendelea hadi 2010 pale Amani Karume na Seif Sharif Hamadi walipopiga mbizi katika bahari iliyochafuka ya kisiasa kwa niaba ya vyama vyao (CCM na CUF) na wakaibuka na yale yaitwayo Maridhiano.
Maridhiano yaliukomesha kwa kiasi kikubwa ule uhasama mkongwe wa kisiasa nchini Zanzibar. Kadhalika Maridhiano yalisababisha kupatikana kwa umoja. Huu umoja wa Wazanzibari ulioimarika sasa ulianzia huko kwenye Maridhiano na ni umoja wa wale wenye matumaini mema kuhusu mustakbali wa nchi yao.
Kwa kuchomoza kwa Ajenda ya Zanzibar katika muktadha wa Siasa za Umoja Wazanzibari hao hii leo wanaamini kwamba wataweza kuupata muradi wao ilimradi waendelee kuwa na umoja na watumie njia za amani na za kikatiba kulifikia lengo lao. Lengo hilo si siri tena; ni la kutaka nchi yao irejeshewe tena mamlaka yake kamili, uhuru wake na adhama yake.
Yote hayo yasingaliwezekana bila ya kuwako siasa zinazowaunganisha wengi. Hii dhana au fikra ya Siasa za Umoja si ngeni. Haikuanza leo na wala si kwamba inatumika Zanzibar pekee. Imekwishatumiwa zamani na itaendelea kutumiwa na mataifa mengi yanayokabiliwa na upeo wa matatizo ya kisiasa, kiuchumi na kijamii. Aghalabu migawanyiko ya kisiasa isiyo na maana ndiyo huyazidisha matatizo kama hayo.
Kingine kinachoyapalilia moto hayo matatizo ni uadui baina ya vyama vya kisiasa. Na si viongozi tu wa vyama tofauti vya kisiasa wanaohasimiana bali uhasama unakuwako hata miongoni mwa wanachama wa kawaida wa vyama hivyo. Huku kwetu ilifika hadi ya wanaojiita viongozi kuamini kuwa mpinzani wa kisiasa ni adui ambaye lazima anyamazishwe, akandamizwe na hatimaye auawe.
Hii leo mazingira ya kisiasa ya Zanzibar ni tofauti kabisa na yale ya kipindi cha takriban nusu karne iliyopita. Tofauti hiyo inajidhihirisha wazi hasa tunapowaangalia wenye kutaka pafanywe mageuzi makubwa katika mahusiano kati ya Tanganyika na Zanzibar na wenye kupendekeza kwamba mahusiano hayo yawe juu ya msingi wa Mkataba.
Watu hao hawatoki kwenye chama kimoja tu cha kisiasa, si watu wa rika moja tu na wala si wa jinsia moja. Hawa ni watu wanaotoka katika makundi yote ya Zanzibar, ni wanachama wa vyama vyote vya kisiasa, wamo kwenye jumuiya za kidini na za vijana na wengine ni watu binafsi wasiojihusisha na jumuiya zozote au vyama vyovyote.
Si hayo tu bali Wazanzibari hao wanaungwa mkono na viongozi wa ngazi za juu wa sasa na wa zamani kutoka vyama vyote vikuu vya huko na si kutoka chama kimoja tu cha kisiasa.
Miongoni mwa hao waliojitokeza wazi hadi sasa kuunga mkono Muungano wa Mkataba ni Seif Sharif Hamadi, Hassan Nassor Moyo, Mansur Yusuf Himidi, Hamza Hassan Juma na Ismail Jussa Ladhu. Huu ni mseto wa aina ya pekee; mchanganyiko maalumu wa wakongwe na vijana. Unadhihirisha kuchomoza kwa vuguvugu la umoja wa kizalendo, vuguvugu lisilojali itikadi za kichama pale mstakabali wa nchi unapojadiliwa.
Tunapoyachambua maoni ya Wazanzibari kuhusu fikra mbalimbali zinazotolewa kuhusu mustakbali wa Muungano hitimisho tunalolipata ni kwamba wengi wa Wazanzibari hawautaki muundo wa sasa wa Muungano. Wao wanasema kwamba wanataka mabadiliko na wanatoa hoja mbalimbali za kuunga mkono matakwa yao ya kutaka Muungano huu uwe wa Mkataba baina ya nchi mbili zilizo huru, yaani Tanganyika na Zanzibar, na nchi zozote nyingine zitazotaka baadaye kujiunga na Muungano huo.
Kama nilivyowishadokeza wiki za hivi karibuni Tume ya Katiba inatazamiwa kurudi Zanzibar mwezi huu na kuanza tena mchakato wake wa kukusanya maoni ya wananchi wa mikoa ya Kaskazini Unguja na Kaskazini Pemba. Tume hiyo imekwishakusanya maoni mikoa ya Kusini Unguja na Kusini Pemba ilipozuru Zanzibar mara ya kwanza. Nadhani safari hii ya pili maoni ya Wazanzibari wanaotaka Muungano wa Mkataba yatazidi kuongezeka na hoja watazozitoa Wazanzibari hao zitazidishwa nguvu na umoja wao utaimarika zaidi.
Juu ya yote hayo kuna haja ya vyama vyote vya kisiasa kuendesha shughuli zao kwa uangalifu mkubwa na hadhari kuu. Vyama hivyo lazima viwe vivumilivu na visijaribu kuwakandamiza wanachama wao wenye kwenda kinyume na misimamo rasmi ya chama kuhusu Muungano, misimamo ambayo hivi sasa imepitwa na wakati na haiwavutii tena wengi wa Wazanzibari.
Nafikiri chama cha CCM kinahitaji kupewa indhari mahsusi. Chama hicho kina wajibu wa kuhakikisha kwamba hakitochafuliwa jina kwa kulaumiwa kwamba kinaziminya haki za binadamu kwa kuwanyima wanachama wake haki yao ya kimsingi ya uhuru wa kusema na wa kueleza imani zao za kisiasa.
Itakuwa ni aibu kubwa endapo chama hicho kitawakaba roho wanachama wake wasiweze kujieleza bila ya pingamizi zozote hasa kwa vile kuna jukwaa la hadhara kama la Tume ya Katiba lenye kuwahimiza wananchi wawe huru wanapotoa maoni yao kuhusu mustakbali wa nchi yao.
Labda chama cha CCM kiuigize mfano wa CUF ambacho sasa kimeitupilia mbali ile sera yake kuhusu Muungano iliyo kwenye ilani yake rasmi. Sera hiyo ikitaka pawepo ‘Muungano wa Serikali Tatu.’ Sasa chama hicho kinasema kinataka ‘Muungano utaokubaliwa na wananchi’ na viongozi wake wawili Seif Sharif Hamadi na Ismail Jussa Ladhu wamekwishatamka kwamba wao wanapendelea pawepo Muungano wa Mkataba. Kuna ushahidi kwamba hilo ndilo chaguo la wananchi wengi wa Zanzibar.
Kelele za Wazanzibari wanaouhiari muundo huo wa Muungano zimepaa na kusikika kote lakini kelele hizo hazitoshi. Ni muhimu pia kwamba Wazanzibari wajitokeze kwa wingi katika shehia zao na wajieleze bila ya pingamizi zozote, wakiongozwa tu na maslahi ya nchi yao na ya vizazi vijavyo. Wajiepushe kuwafuata wale wachache wanaoziona ‘amri za chama’ kuwa ni adhimu kushinda uzalendo na maslahi ya nchi.
Chanzo: Raia Mwema

Wednesday 3 October 2012

JUSSA: ZANZIBAR HURU HAINA MJADALA

“Wakati tunaelekea India wiki iliyopita tukiwa Uwanja wa Ndege wa Dubai wakati tunabadilisha ndege, tulikutana na mmoja wa Makamishna wa Tume ya Katiba kutoka upande wa Tanganyika ambaye ni msomi wa hali ya juu.
Katika majibu ya kustaajabisha wakati nilipomuuliza vipi hali ya utoaji maoni inaendelea, alitujibu kuwa inaendelea vizuri na pamoja na kwamba upande mmoja (nna hakika alikusudia Zanzibar) unatoa madai makubwa, yeye haimpi tabu kwa sababu anajua wanaofanya hivyo wanajipa nafasi kubwa ya kuja kupatana (alitumia neno la Kiingereza ‘bargaining’) ili kupata muafaka wa kati na kati.
Bahati mbaya mawazo kama haya ya Kamishna huyu ndiyo mawazo mgando ya watunga sera na sheria wengi wa Tanganyika wanaojiona kama ni watawala au wamiliki wa Zanzibar na hivyo kujipa matumaini kuwa Zanzibar tunaposema tunataka kurejesha mamlaka yetu kamili kitaifa na kimataifa tukiwa na kitu chetu Umoja wa Mataifa huwa tunatafuta ‘kupatana’ au kwamba hatuna uwezo huo mpaka Tanganyika waridhie.
Wanapaswa wajue sasa kabla hawajachelewa kwamba mamlaka kamili ya Zanzibar (Sovereign Zanzibar) siyo ombi ni matakwa ya Wazanzibari na tutayasimamia kwa nguvu na uwezo wetu wote. Na katika kulifikia lengo hilo hakuna wa kutuzuia isipokuwa Mwenyezi Mungu. Pamoja Daima!”
JUSSA @FACEBOOK WALL.

Monday 1 October 2012

Azam yaleta meli mpya Zanzibar

KAMPUNI ya Azam Marine inayomiliki boti ziendazo kasi hapa nchini, imeingiza meli mpya na ya kisasa itakayochukua zaiidi ya abiria 1,500 na magari 200.
Meneja Mkuu wa Kampuni ya Azam Marine, Hussein Mohammed Saidi, amesema hayo mjini Zanzibar jana kuwa meli hiyo ambayo itafanya safari zake kati ya Dar es Salaam, Zanzibar na Pemba itatoza nauli nafuu kwa abiria wake.
Alisema meli hiyo inatarajiwa kuanza safari zake mara baada ya kukamilisha taratibu za mamlaka mbalimbali.
Meli hiyo inayoitwa Azam SeaLinki ni ya kisasa katika ukanda huu wa mwambao wa nchi za Kusini na Pembe ya Afrika.
Hussein alisema, meli hiyo ambayo imetengenezwa nchini Ugiriki, inatayarishiwa eneo maalumu litakalotumika kwa kupakia na kushusha abiria na mizigo yakiwemo magari.
Alisema meli hiyo itasafiri kwa muda wa saa tatu kutoka Dar es Salaam hadi Zanzibar na saa nne kutoka Zanzibar hadi Pemba ama saa 7 kutoka Dar es Salaam hadi Pemba.
Meneja huyo aliongeza kuwa pamoja na kuwasili kwa meli hiyo, Kampuni ya Azam pia inatarajia kuleta meli nyingine ya abiiria inayojulikana kama Kilimanjaro namba 4.
Kwa upande wao, baadhi ya wananchi wa visiwa vya Zanzibar walipongeza ujio wa meli hiyo, lakini wakaitaka serikali kuendelea kudhibiti uingizwaji wa meli chakavu na kukuu ili kuepuka uwezekano wa kutokea ajali za mara kwa mara.
Rajabu Khamisi, mkazi wa Pemba na Rehema Omari wa mjini Zanzibar, walisema kuna haja ya serikali kusimamia ukomo wa nauli ili kila mwananchi aweze kusafiri kutoka sehemu moja hadi nyingine kwani vipato vyao havilingani.
Chanzo: Nipashe