MAPENDEKEZO YA KAMATI YA MARIDHIANO ZANZIBAR KUHUSU UPI UWE MWELEKEO
WA WAZANZIBARI KATIKA KUIJADILI RASIMU YA KATIBA YA JAMHURI YA MUUNGANO
WA TANZANIA ITAKAYOTOLEWA NA TUME YA MABADILIKO YA KATIBA
UTANGULIZI:
… Baada ya wananchi wa Zanzibar kutoa maoni yao juu ya vipi Muungano wa
Zanzibar na Tanganyika unapaswa kuwa, hatimaye Tume ya Mabadiliko ya
Katiba inatarajiwa kutoa rasimu ya awali ya Katiba Mpya ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania kati ya mwishoni mwa mwezi Mei na mwanzoni mwa
mwezi Juni 2013.
Wakati tunaisubiri kwa hamu rasimu hiyo itolewe na kujua kilichomo,
sisi wajumbe wa Kamati ya Maridhiano Zanzibar tumekaa na kutafakari juu
ya upi unapaswa kuwa mwelekeo wa Wazanzibari katika kuijadili rasimu
hiyo pale itakapotoka.
Baada ya mashauriano ya kina kati ya wajumbe wa Kamati ya Maridhiano
na pia kwa kuwahusisha watu wengine mashuhuri hapa Zanzibar, tumekuja na
mapendekezo yafuatayo ambayo leo hii tunayawasilisha kwa wananchi wa
Zanzibar kupitia Kongamano hili. Haya si maagizo bali ni mashauri yenu
na pindi mkiyakubali basi tutakuombeni tuyafanyie kazi kwa pamoja kwa
kuyatumia katika kuipokea na kujadili rasimu pale itakapotolewa.
Mapendekezo yetu ni kama ifuatavyo:
1. Jina la Muungano:
Muungano huu umetokana na Jamhuri mbili kuungana kwa hiyari. Jamhuri
hizo ni Jamhuri ya Watu wa Zanzibar na Jamhuri ya Tanganyika. Jina la
awali lililotajwa katika Mkataba wa Muungano la muungano wa jamhuri hizi
mbili lilikuwa ni Jamhuri ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar. Jina
hili baadaye mwezi Oktoba 1964 lilibadilishwa na kuitwa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania.
Ukiangalia mifano ya nchi nyingine zilizoungana, jina la muungano
huweka bayana kwamba zilizoungana ni zaidi ya nchi moja, zaidi ya falme
moja au zaidi ya jamhuri moja. Kwa mfano, muungano wa nchi (states) za
Marekani unaitwa kwa kiingereza United States of America (USA), ule
uliokuwa muungano wa jamhuri za kisovieti ukiitwa Union of Soviet
Socialist Republics (USSR) na ule muungano wa falme za kiarabu unaitwa
United Arab Emirates (UAE).
Ili kuondosha dhana iliyojengeka kwamba muungano wa jamhuri zetu
mbili umeunda nchi moja na kuzifuta nchi zetu, Katiba Mpya inapaswa
kuweka jina linalotambua msingi huo na historia hiyo. Hivyo basi, jina
jipya liwe ni Muungano wa Jamhuri za Tanzania na kwa kiingereza United
Republics of Tanzania.
Jina hili litasaidia utambulisho wa nchi wanachama katika uwanja wa
kimataifa pale litapoambatanishwa katika nyaraka zote rasmi pamoja na
jina la nchi husika. Kwa maana hiyo katika uwanja wa kimataifa na katika
pasi za kusafiria utaweka wazi na kuwa na “UNITED REPUBLICS OF TANZANIA
– REPUBLIC OF ZANZIBAR” na “UNITED REPUBLICS OF TANZANIA – REPUBLIC OF
TANGANYIKA”.
2. Mipaka ya Zanzibar na Tanganyika:
Wakati zinaungana, Zanzibar na Tanganyika zilikuwa tayari ni nchi
zenye mamlaka kamili zikiwa ni wanachama wa Umoja wa Mataifa na hivyo
kila moja ilikuwa na mipaka yake inayoeleweka. Katiba na sheria za nchi
mbili hizi ziliweka bayana mipaka hiyo na mipaka hiyo ilitambuliwa chini
ya sheria za kimataifa.
Rasimu ya Katiba Mpya ni lazima itamke kwa uwazi kabisa na kutambua
na kuheshimu mipaka ya nchi mbili hizi kama ilivyokuwa kabla ya siku ya
Muungano tarehe 26 Aprili, 1964.
Baada ya hapo, Katiba ya Zanzibar na Katiba ya Tanganyika
(itakayotungwa baada ya kupata Katiba mpya ya Muungano) kila moja iweke
wazi mipaka yake.
3. Uraia:
Uraia ndiyo msingi wa ujananchi. Kwa vyovyote vile Katiba Mpya
isijumuishe suala la Uraia kuwa la pamoja kupitia Muungano. Kila nchi
mwanachama katika muungano ibakie na uraia wake na iratibu masuala yote
yanayohusu uraia wake na raia zake. Kwa kufuata mfano kama wa Muungano
wa Ulaya (European Union), unaweza kuwa na haki inayotambulika kikatiba
ya uhuru wa raia wa nchi moja mwanachama kwenda katika nchi nyengine
mwanachama kupitia utaratibu maalum utakaowekwa (free movement of
people). Hata hivyo, kila nchi mwanachama iwe na haki ya kuweka
utaratibu wa vipi raia hao watafaidi haki na fursa za nchi mwanachama
nyingine.
Hili ni la muhimu hasa kwa nchi ndogo kama Zanzibar ambayo ina
rasilimali ndogo ya ardhi na hasa ikizingatiwa kuwa ardhi ilikuwa
mojawapo ya sababu kuu za kufanyika Mapinduzi. Katika hali kama hiyo,
Zanzibar ina sababu nzito za kuona inadhibiti na kusimamia wenyewe Uraia
wake na utambulisho wa raia hao.
Hivyo basi, suala la Uraia lisiwemo katika mambo ya Muungano na badala yake kila nchi isimamie yenyewe masuala ya Uraia.
Hata hivyo, kunaweza kukawepo chombo cha pamoja kinachojumuisha nchi
mbili hizi cha kuratibu masuala ya Uraia na haki na fursa ambazo raia
wanaweza kuwa nazo kwa kila upande.
4. Uhamiaji:
Kutokana na sababu tulizozitaja hapo juu kuhusiana na suala la Uraia
inapelekea wazi kuwa kila nchi mwanachama idhibiti na kusimamia wenyewe
mambo ya Uhamiaji. Hivyo basi, rasimu ya Katiba Mpya isijumuishe suala
la Uhamiaji kuwa ni suala la Muungano.
Kila nchi mwanachama kati ya Zanzibar na Tanganyika iwe na paspoti
yake yenyewe yenye kubeba jina la nchi yake na nembo yake ya Taifa na
yenye kudhamini usalama wa raia wake nje ya nchi kupitia uhakikisho
unaotolewa na Serikali ya nchi husika.
Ili kuonesha sura ya kuwepo muungano wa kisiasa, paspoti za nchi
mbili hizo zinaweza kuwa na jina la Muungano juu na kufuatiwa na jina la
nchi mwanachama likiambatana na nembo ya Taifa ya nchi hiyo. Kwa mfano,
“UNITED REPUBLICS OF TANZANIA – ZANZIBAR PASSPORT” na “UNITED REPUBLICS
OF TANZANIA – TANGANYIKA PASSPORT”.
Kwa upande mwengine kunaweza kukawa na mamlaka ya kuratibu masuala ya
uhamiaji wa nchi hizi mbili (Union immigration regulatory authority)
kwa lengo la kuweka na kuratibu mfumo mzuri wa mawasiliano kati ya
mamlaka za uhamiaji za nchi mbili hizi.
5. Mambo ya Nje:
Mamlaka juu ya mambo ya nje na uwezo wa nchi kuingia mikataba na nchi
nyingine na mashirika ya kimataifa ndiyo roho ya nchi yoyote duniani
kutambulika kimataifa na kuweza kusimamia mamlaka yake ya ndani
yanapohitaji mashirikiano na nchi nyengine.
Ili nchi iweze kutambulika kimataifa inapaswa kuwa na mambo manne yafuatayo:
(a) eneo la ardhi lenye mipaka inayotambulika;
(b) watu wanaoishi kwenye eneo hilo wanaojitambulisha na eneo hilo;
(c) serikali inayotekeleza majukumu yake; na
(d) uwezo wa kuingia katika mahusiano ya kimataifa na nchi nyengine.
Kwa msingi huo, Wazanzibari wanahitaji kuona kuwa Mambo ya Nje
haijumuishwi katika orodha ya mambo ya Muungano na badala yake kila nchi
isimamie yenyewe mamlaka yake juu ya mambo ya nje.
Hata hivyo, uratibu wa sera ya mambo ya nje (foreign policy
coordination) inaweza kuwa ni suala la muungano lakini utekelezaji wake
kila nchi ikausimamia kupitia Wizara yake ya Mambo ya Nje. Uratibu wa
sera ya mambo ya nje unaweza kufanywa kupitia chombo cha pamoja
kitakachoundwa na Wizara za Mambo ya Nje za nchi mbili hizi kwa mfano
kuwa na Council on Foreign Policy.
Kutokana na hoja hizo hapo juu inabaki kuwa kila nchi iwe na
uanachama na kiti chake katika Umoja wa Mataifa na jumuiya nyengine za
kimataifa. Hayo si ajabu katika miungano. Umoja wa Jamhuri za
Kisoshalisti za Kisovieti (USSR) ulikuwa na uanachama na kiti chake
Umoja wa Mataifa lakini miongoni mwa nchi wanachama, Jamhuri tatu za
Ukraine, Belarus na Georgia ziliamua kuwa na uanachama na viti vyao
katika Umoja wa Mataifa na hilo liliwezekana.
Kwa msingi huo huo, Zanzibar iwe na uanchama wake katika Umoja wa
Mataifa, Umoja wa Afrika, Jumuiya ya Madola, Jumuiya ya Afrika
Mashariki, Jumuiya ya SADC na jumuiya nyengine za kikanda na za
kimataifa.
6. Sarafu, Benki Kuu, Mikopo na Biashara ya Nchi za Nje, Ushuru wa Forodha, Kodi ya Mapato na Kodi ya Mashirika:
Uchumi si suala la Muungano hata katika Katiba inayotumika sasa. Hata
hivyo, nyenzo za kuendeshea na kusimamia uchumi wa nchi kwa maana ya
sera za fedha na uchumi (fiscal and monetary policies) zimeendelea
kudhibitiwa kupitia Serikali ya Muungano.
Vyombo vikuu vinavyosimamia sera hizo ambavyo ni Benki Kuu (BOT),
Mamlaka ya Kodi Tanzania (TRA) na Wizara ya Fedha ya Serikali ya
Muungano vimekuwa vikifanya maamuzi na kuyatekeleza bila ya kuzingatia
kuwa kwa maumbile uchumi wa Zanzibar ambao ni uchumi unaotegemea utoaji
wa huduma (service oriented economy) hauwezi kuwa sawa na uchumi wa
Tanganyika ambao unategemea rasilimali (resource based economy). Sera za
fedha na uchumi zikiwemo zile zinazohusu udhibiti wa sarafu na viwango
vya kodi, ushuru na riba katika mabenki zimekuwa zikitungwa bila ya
kuzingatia msingi huo wa chumi mbili zilizo tofauti na badala yake mara
zote zimeegemezwa kwenye kulinda maslahi ya uchumi wa Tanganyika.
Sarafu ya pamoja imekuwa ikishuka thamani kwa kasi kila uchao
kutokana na sababu nyingi lakini miongoni mwake zaidi zinatokana na
uendeshaji mbaya wa uchumi wa Tanganyika. Serikali inapochapisha sarafu
zaidi ili kudhibiti mfumko wa bei athari zake zinaikumba pia Zanzibar.
Zanzibar inahitaji kujikomboa kiuchumi ili iweze kutekeleza malengo
ya Mapinduzi kwa wananchi wake na hivyo inahitaji kuwa na mamlaka yake
kamili katika kusimamia masuala ya sera za fedha na uchumi yakiwemo
masuala yote yanayohusu sarafu, viwango vya kodi na ushuru pamoja na
riba katika mabenki, mikopo na biashara ya nchi za nje.
Kutokana na hali hiyo, masuala ya sarafu, benki kuu, mikopo na
biashara ya nchi za nje, ushuru wa forodha, kodi ya mapato na kodi ya
mashirika kila nchi inapaswa iyasimamie yenyewe.
7. Polisi:
Pamoja na kuwemo katika mambo ya awali ya Muungano lakini uendeshaji
wa Polisi umekuwa na matatizo yake katika muungano. Miaka yote Polisi
Zanzibar imekuwa ikilalamika kuwa inachukuliwa kama vile ni Mkoa tu na
hata bajeti na mahitaji yake mengine yanachukuliwa hivyo hivyo na makao
makuu ya Polisi yaliyopo Dar es Salaam.
Katika nchi nyingi duniani Polisi ambayo inashughulika na usalama wa
raia na mali zao imekuwa ikiendeshwa chini ya Serikali za Manispaa na
hata Majimbo seuze kwa nchi kama ilivyo Zanzibar.
Ukiondoa mishahara na bajeti ndogo ya uendeshaji inayotolewa na makao
makuu ya Polisi, gharama nyengine za uendeshaji wa polisi kwa Zanzibar
zimekuwa zikichangiwa na mamlaka za Zanzibar ikiwemo Bodi ya Mapato
Zanzibar (ZRB).
Hivyo basi, wakati umefika kuona mamlaka kuhusu Polisi yanaondolewa
katika orodha ya mambo ya Muungano na kila nchi ishughulikie yenyewe
Polisi yake.
8. Mafuta na Gesi Asilia (pamoja na maliasili nyengine zote):
Baraza la Wawakilishi la Zanzibar kwa niaba ya Wazanzibari
lilishafanya maamuzi mwezi Aprili 2009 kuyaondoa masuala ya mafuta na
gesi asilia kutoka kwenye orodha ya mambo ya Muungano. Mbali na maazimio
ya Baraza la Wawakilishi, masuala ya mafuta na gesi asilia yanahusu
uchumi ambalo si suala la Muungano.
Katiba Mpya haipaswi kuyajumuisha masuala hayo mawili (pamoja na maliasili nyengine kwa ujumla) kuwa mambo ya Muungano.
Hivyo basi, rasimu yoyote itakayoyajumuisha masuala hayo ya Mafuta na
Gesi Asilia (pamoja na maliasili nyengine zote kwa ujumla) kuwa masuala
ya Muungano haitakubalika kwa Wazanzibari.
9. Vyama vya Siasa:
Muungano uliundwa na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar na Jamhuri ya
Tanganyika kupitia serikali zao. Mazungumzo yaliyopelekea muungano huo
na hata utekelezaji wa hatua za kuunganisha nchi mbili hizi katika
muungano hayakuhusisha vyama vya siasa vya wakati huo, ASP kwa upande wa
Zanzibar na TANU kwa upande wa Tanganyika. Ndiyo maana kwa miaka 13 ya
Muungano (kuanzia 1964 hadi 1977) kila nchi kati ya nchi mbili hizi
iliendelea kuongozwa na chama chake cha siasa.
Moja kati ya dhoruba kubwa dhidi ya makubaliano ya asili ya muungano
huu ambayo ni Mkataba wa Muungano ilikuwa ni kuunganisha vyama vya siasa
vya ASP na TANU na kuunda CCM ambacho kilijitangazia kushika hatamu na
kuwa juu ya vyombo vyengine vyote vya nchi zikiwemo Serikali. Utaratibu
huo uliingizwa ndani ya Katiba za nchi na hivyo kuuhalalisha kisheria.
Tokea wakati huo, Zanzibar imekosa mamlaka ya kisiasa ya kufanya maamuzi
yake kwa mambo yanayoihusu. Na pale ilipofanya hivyo ilifanya kwa
kutegemea na kujiamini kwa uongozi uliopo Zanzibar ingawa majaribio ya
kutumia nguvu ya vyama kuzuia maamuzi kama hayo yamekuwa yakifanyika na
baadhi ya wakati kufuzu.
Maongozi ya nchi yoyote yanategemea historia, mila na utamaduni wa watu wa nchi husika.
Kwa msingi huo basi, na ili Zanzibar iweze kurejesha mamlaka yake ya
kisiasa katika kufanya na kusimamia maamuzi kwa mambo yake, rasimu ya
Katiba haipaswi kujumuisha suala la vyama vya siasa kuwa ni jambo la
Muungano. Zanzibar na Tanganyika kila moja iweze kuandikisha vyama vyake
vya siasa.
10. Utaratibu wa uendeshaji wa Mambo ya Muungano:
Kwa yale mambo yatakayokubaliwa kubaki katika Muungano kama vile:
- Katiba ya Muungano wa Jamhuri za Tanzania;
- Serikali ya Muungano wa Jamhuri za Tanzania;
- Uratibu wa Sera ya Mambo ya Nje;
- Ulinzi;
- Usalama;
- Mamlaka juu ya mambo yanayohusika na hali ya hatari;
- Utumishi katika Serikali ya Muungano wa Jamhuri za Tanzania; na
- Mahkama ya Rufani ya Muungano wa Jamhuri za Tanzania.
Utaratibu wa uendeshaji wake uwekwe wazi katika Katiba kwamba maamuzi
yote yatafanywa kwa mashauriano na makubaliano kati ya nchi mbili
zinazounda Muungano huu na yatakuwa halali tu iwapo yatafuata msingi
huu.
HITIMISHO:
Haya kimsingi ndiyo mapendekezo yetu Kamati ya Maridhiano. Tunayaleta
kwenu muyapokee, muyajadili na kuwaomba muyaridhie ili yawe ndiyo msingi
wa mwelekeo wa wananchi wa Zanzibar ambao wengi wao waliojitokeza mbele
ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba walitaka nchi yao iwe na mamlaka
kamili.
Kwa mapendekezo haya, tunadhani Zanzibar na Tanganyika zitaendelea
kuwa na mashirikiano ya kidugu kupitia mfumo mpya wa Muungano na wakati
huo huo kila nchi mwanachama wa muungano ikibaki na mamlaka yake kamili
katika yake maeneo ya msingi ambayo kila nchi hupenda kuwa nayo.
Imetolewa:
Zanzibar
25 Mei, 2013
Source: Jussa’s Wall on facebook
No comments:
Post a Comment