Sports

ZFA YAUMBUKA

 Moja kati ya udhaifu na kasoro kubwa ya mwanadamu ni kutojijuwa yaani kwa lugha ya kitaalamu, kutokuwa na ‘self concept’. Mtu asiejijua hafaidi raha wala utamu wa dunia kwani maisha yake huwa ni mfululizo wa mikasa, majanga, nuhusi, fedheha na muadhara usiokwisha.
Kujijua ni silaha kubwa kwa mwanadamu ukitoa ile hazina aliyotupa mola ya akili. Kujijuwa ni uwezo wa kujitambuwa wewe kama wewe, uwezo wako, maumbile yako, hulka yako, ufahamu wako, nguvu na pumzi yako, nafasi yako katika jamii, na mamlaka uliyonayo na mipaka ya mamlaka hayo. Hivi ndio kujijuwa.
Mwanadamu anapojijua hadhi yake, hali yake na alivyo hapati tabu. Maana watu husema muungwana hafedheheki. Na muungwana ni mtu anaejijuwa, akajua alivyo, alipo. Kwa mfano, kuna mambo kadhaa huwafika watu hapa Zanzibar kwa kutokijijuwa kwao.
Kama mna kumbukumbu nzuri mwaka 1997, Serikali ya Dr. Salmin Komandoo iliwatia ndani wanachama 18 wa chama cha wananchi CUF kwa tuhuma za uhaini. Ya kwamba walitaka kumpindua Rais na serikali yake. Wakawekwa ndani mpaka wakaambiwa si mapapai, kuwa yangeoza.
Lengo la komandoo kuwatia watu wale ndani kwanza ilikuwa ni kuuonesha umma kama alikuwa Rais wa kikweli na sio wa udongo kama alivyoimbwa na wapinzani. Hivyo, alitaka kuonesha nguvu na uwezo wake kwa kuwatia adabu watuhumiwa wale wa kesi hewa ya uhaini.
Kwa kutokujijuwa kuwa yeye hakuwa Rais wa kweli, alijikuta akiumbuka pale mahakama kuu Tanzania ilipoamuru kuwa watu wale waachwe huru kwani Zanzibar sio nchi na kwa hivyo haiwezi kufanyiwa uhaini wa kimapinduzi tena. Komandoo akawa na uso mdogo kama mahamri yaloumka kisha yakafulia kabla ya kuchomwa. Hasara ya kutokujijua hii.
Nina mfano mwengine wa mtu aliekuwa hakujijuwa pia. Enzi za ujana wetu, tulikuwa na chama cha kupiga samba/beni. Ikifika siku za mialiko ya kupiga ngoma kila mtu akivaa vizuri na wakati mwengine hata kuazima nguo ya mtungini lakini shoti mtu avae mpya tu.
Katika chama cha ngoma kulikuwa na wanawake idadi sawa na wanaume. Kwa hio tukenda ngoma tukifatana sote wake kwa waume. Siku moja tunavuka mto, kuna mwenzetu alikuwa mfupi mno, lakini akipenda sifa sana mbele ya wanawake.
Tulipofika pale kwenye mto watu hawakutaka kuvua nguo zao kuvuka kwani maji yalikuwa mengi. Ikabidi watu wachupe kutoka upade mmoja kwenda wa pili wa mto bila kugusa maji. Wanawake walivuka kwa miguu. Na baadhi ya wanaume walivuka kwa miguu.
Bwana mfupi, alipoona watu wanaruka nae akajivuta. Karuka juu mara kaanguka kati kati ya mto. Karoa na mabuga yake yote, huku wanawake wakianguka kwa vicheko. Huu ni mfano wa mtu aliekuwa hakujijuwa na yaliyomfika kwa huko kutojijuwa kwake.
Hivi majuzi, ZFA wakaja na kali ya kufungia mwaka pale walpoamuwa kuwafungia kucheza mpira wachezaji wa timu yetu ya Taifa heroes dumu daima popote duniani. Tukasema sana hapa kuwa wangeyamaliza mambo yale ndani likapita. Hatukusikika. ZFA ikazidi kuonesha kiburi na jazba. Ikawafungia akina Nadir Haroub, Aggrey Morris, na Mcha Vialli.
Bila kujijuwa hadhi na nafasi yao duniani, ZFA waliamini kuwa wamewaumbuwa wachezaji hao wa kimataifa ambao ni tegemeo sio kwa Zanzibar tu, bali taifa na hata vilabu vyao. ZFA haitambuliki licha ya kuwa haijitambui yenyewe. Na hili labda hawalijui. Ndio huko kutokujijuwa.
Kwa vile ZFA ni garasa mbele ya TFF, wale wachezaji wameitwa rasmi katika kikosi cha watu 22. Na niliwahi kusema, wale ni lazima wataitwa maana ‘bata akikataa kuchokora karo, atakula nini’? Kwa Tanzania hatuna wachezaji kiivyo wa kusema huyu afungiwe maisha na apatikane mwengine, ndio hao kwa hao. Na ndio hao wameitwa. ZFA, kimya!
Nionavyo, ZFA wameumbuka. Tena wameumbuka kama mrembo aliyetapika dagaa, au mrembo aliemwagiwa tindikali ya uso. Wameumbuka hawana haiba maana wamedharauliwa na wenzao wa TFF. Wamedharauliwa kwani barua yao haikusomwa, kama ilisomwa hakuna aliejali kwani hawana ubavu wowote wa kufanya maamuzi makubwa ya soka hapa nchini.
ZFA mwisho Chumbe, na hili hawataki kulikubali. Hawajijui kama wao ni makinda ya FUFU hayana mbawa za kuruka wala miguu ya kukimbia mbio. Hawajui, wanajiona na nguvu lakini masikini roho zao, kioo kimewacheza.
Wamewafungia wachezaji kwao kumbe kwa jirani wanatakiwa. Mkosi gani huu? Amkeni ZFA Zanzibar si nchi ijekuwa ZFA? Yaguju! Bila shaka huu ni ujumbe kwa wengine wanaojifanya na vyeo hapa Zanzibar. Labda huenda wakatanabahi kuwa mambo hayako hivyo kwa kujifunza kwa wenzao kama hawa ZFA waliobwagwa kwa vijibwa!
Chanzo: Mzalendo


Zanzibar Kujitupa uwanjani leo Misri

TIMU ya Taifa ya Zanzibar ‘Zanzibar Heroes’ leo inatarajiwa kucheza na timu ya NB nayoshiriki Ligi Kuu ya Misri mchezo wa kirafiki utakaofanyika Uwanja wa 16 October jijini Cairo.

Ofisa Habari wa Chama cha Soka Zanzibar ( ZFA), Munir Zakaria alisema jana kuwa huo utakuwa mchezo wa pili wa kujipima nguvu kwa timu hiyo nchini Misri, ambapo wa kwanza
Zanzibar ilifungwa mabao 2-0 na timu ya Ghazel Suez.

Alisema baada ya kupoteza mchezo wa kwanza, kutokana na uchovu wa safari na kutozoea hali ya hewa, timu hiyo iliamua kufanya mazoezi ya nguvu na sasa ipo tayari kwa mchezo huo.

Munir alisema kuwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo Zanzibar, Abdillahi Hassan Jihad yupo Cairo tangu mwishoni mwa wiki kwa ajili ya kuongeza nguvu na hamasa kwa timu hiyo.

Alisema timu hiyo itacheza mchezo wake wa tatu dhidi ya timu ya taifa ya vijana ya Misri chini ya umri wa miaka 18 Ijumaa.


Zanzibar Heroes Nchini Misri
Timu ya taifa ya Zanzibar Zanzibar heroes wakifanya mazoezi nchini Misri kwa ajili ya kujiandaa na mashindano ya challenge: Source: Zanzinews


Udhamini ligi kuu ya Zanzibar Mashakani

Udhamini wa ligi kuu ya soka ya Zanzibar uliokuwa ufanywe na kampuni ya usafiri wa baharini ya Seagull umeingia wasiwasi baada ya hatua ya serikali kuisimamisha meli hiyo ya abiria.

Ligi kuu ya Zanzibar iliyokuwa ianze mwezi agosti ilichelewa kwa kukosa wadhamini na ilipoanza wiki iliyopita ikapigwa stop kwa sababu ya shauri la timu ya malindi katika mahakama ya Zanzibar.

Sasa Malindi wamefuta kesi yao baada ya kununua daraja kwa kuichukua timu ya Miembeni United na chama cha soka kilikuwa kimepanga ligi hiyo ianze rasmi siku ya Ijumaa.

Lakini vilabu vikijipanga imedhihirika kuwa dau la mnyonge haliendi joshi pale serikali ilipoilima barua kampuni ya Seagull iliyojitwisha jukumu la kudhamini ligi hiyo kwa mamlaka za usafiri wa bahari kuisimamisha meli ya Seagull.

Serikali imesema kwa sababu za kiusalama meli hiyo inasimamishwa kwa muda usiojulikana na kampuni hiyo tayari imeshaiarifu ZFA juu ya hali hiyo ambapo inaelekea udhamini utaota mbawa.

Katibu mkuu wa ZFA Mzee Zam alithibitisha hali hiyo na kusema imewavunja moyo ingawa alikiri kuukubali uamuzi wa serikali kwa kuzingatia hadhari inayochukuliwa kutokana na ajali ya MV Spice Islander ya septemba 10 iliyouwa mamia ya abiria.

Kwa hivyo ligi itakua ya pangu pakavu na Mwandishi wa BBC Zanzibar, Ally Saleh anasema hali hiyo itaziwia vigumu timu 12 zinazoshiriki ligi hiyo kwa ukosefu wa fedha za kujikimu.

Udhamini huo ulikuwa ugharimu Tanzania shilingi milioni 75 ulipokewa vyema na vilabu kwa vile iliaminika ingeifanya ligi hiyo kuwa na ushindani.

Mara ya mwisho Ligi ya Zanzibar kupata udhamini ilikuwa ni kupitia kampuni ya simu za mkononi ya ZANTEL kwa misimu ya 2006/2007 na 2007/2008.




Serikali kuipigania Z'bar uanachama Fifa
   
  Ijumaa, 11 November 2011

SERIKALI imesema itashirikiana na Shirikisho la Soka Tanzania, TFF pamoja na Chama cha Soka Zanzibar, ZFA, kuelekeza nguvu Shirikisho la soka la Kimataifa, Fifa, ili Zanzibar ipate uanachama wa shirikisho hilo.

Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Vijana na Michezo, Fenella Mukangala aliliambia Bunge mjini Dodoma jana wakati akijibu swali la Kheri Ameir (Matemwe) aliyetaka kujua hatua zinazochukuliwa kuhakikisha Zanzibar inakuwa mwanachama wa Fifa.

Dk. Fenella alisema kuwa Wizara yake kwa kushirikiana na TFF na ZFA zitaunganisha nguvu kudai uanachama wa Fifa licha ya kuwa Fifa ilikwishakusema Zanzibar haiwezi kuwa mwanachama wake.

Alisema, awali ujumbe mzito wa Tanzania ulikwenda Makao Makuu ya Fifa mjini Zurich, Uswisi na kukutana na Rais wa Fifa, Sepp Blatter aliyeahidi kulitolea ufafanuzi baadaye. 

Itakumbukwa Oktoba mwaka jana, Mjumbe wa Fifa anayesimamia Maendeleo ya soka Ukanda wa Kusini mwa Afrika, Ashford Mamelodi alikutana na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam na kusema Zanzibar haiwezi kuwa mwanachama wa Fifa.

Alisema kuwa Zanzibar iko ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na haiwezi kuwa mwanachama na inaweza kupata sifa hizo endapo itakuwa nchi inayojitegemea.

Hata hivyo, Dk Fenella alisema, licha ya Fifa kutoa taarifa hiyo, iliahidi kuisaidia Zanzibar kwa hali na mali kupitia TFF ikiwemo kutoa mafunzo kwa makocha na waamuzi kwa maendeleo ya soka Zanzibar.

Zanzibar ilianza kampeni za kuutaka uanachama wa Fifa tangu 1998 wakati wa Fainali za Kombe la Dunia zilizofanyika Ufaransa, lakini mkutano wa Fifa uliitaka Zanzibar kuanzia maombi yake Cecafa na Caf.

Baada ya kujieleza Caf, ilipata uwakilishi ngazi za klabu, lakini bado timu ya taifa inaunganishwa na Bara kwa Fainali za Afrika na mechi za Kombe la Dunia kwa Kanda ya Afrika.

Source: Mwananchi

No comments:

Post a Comment